Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Bajeti yetu. Awali ya yote, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini pia naomba nitoe pongezi nyingi kwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita, hasa kwa mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi ambavyo ameweza kusimamia uendelezaji wa miradi yote mikubwa ambayo imeanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pia nampongeza sana kwa jinsi ambavyo ameweza kutusimamia na kutupelekea miradi mikubwa hasa ya vituo vya afya na ujenzi wa miundombinu ya madarasa. Kwa kweli wananchi wanashukuru sana na hili limepunguza adha na maswali mengi kwetu sisi Waheshimiwa Wabunge. Kwa kiasi kikubwa imeturahisishia kazi, hasa tunapojiandaa kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwezi Januari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa bajeti iliyopita michango mingi sana ilijikita kwenye ujenzi wa miundombinu, hasa barabara. Kwenye mapendekezo ambayo tumeyasoma kupitia Mpango huu wa Serikali tumeona kwamba kuna barabara nyingi ambazo zilikuwa zimeshafanyiwa upembuzi yakinifu na nyingine zilishatangazwa, bado ujenzi haujaanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya barabara hizo ni ya kutoka Kilosa kupitia Ulaya kwenda Mikumi, barabara ambayo ni muhimu sana kiuchumi na naamini kuna barabara nyingi za aina hiyo. Sasa ombi langu ni kwamba mipango hii inapokuja mipya inapaswa kuzingatia barabara zile ambazo zilikuwa kwenye mpango uliopita zinakamilika kabla haijajikita katika maeneo mapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, Mpango huu haujazungumza kilio cha Wabunge wengi hasa kuhusiana na hii service road ambayo inahudumia ujenzi wa barabara ya SGR. Barabara hii ambayo kazi yake ni ujenzi na kusafirisha vifaa vya ujenzi kwa ajili ya SGR imefungua vijiji vingi sana vya nchi hii kuanzia Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Tabora mpaka kule Mwanza. Kuna maeneo ulikuwa huwezi kufika hata kwa pikipiki, lakini kwa sababu ya ujenzi wa reli yetu barabara hii imefungua vijiji vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na yote hayo, lakini hatujaona mpango wa uhakika wa Serikali, unakwenda kuihudumia vipi barabara hii kuwa moja ya njia za uhakika ambazo zitapitika mwaka mzima bila kujali masika au kiangazi. Tunajua kwamba reli hii inakwenda kukamilika, lakini nini future ya barabara ambayo inahudumia reli hii? Itaendelea kutumika kwa wananchi; Serikali inaichukua au ina mpango gani na hii barabara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu moja ya vitu ambavyo tunavizungumzia ambavyo Bunge letu hili limejipa jukumu ni kwenda kufanya mapinduzi ya kilimo. Barabara hii inasaidia sana katika mapinduzi haya ya kilimo kwa kuunganisha vijiji vyetu na barabara kuu na masoko. Kwa hiyo pamoja na mpango mzuri, naomba kupata uhakika ni kwa jinsi gani Serikali inakwenda kuichukulia barabara hii kama maeneo ya vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu maendeleo vijijini. Vijiji vyetu vingi ambavyo vinajikita kwenye kilimo havihitaji barabara ya lami, vinahitaji kufikika mwaka mzima, masika na kiangazi. Shughuli zinazofanyika kule ni nyingi na ni kubwa na ni muhimu kwa uchumi wetu. Kikwazo chao ni kimoja tu; wana uwezo wa kuzalisha, lakini hawana uhakika wa kufikisha bidhaa zao sokoni kwa sababu tu barabara hazifikiki. Kwa hiyo naomba huu Mpango wa Maendeleo au Mpango wa Bajeti ujikite katika kuhakikisha barabara zetu za vijijini ambazo zinakwenda kwenye maeneo ya uzalishaji zinapitika mwaka mzima, siyo kwa lami, kwa kiwango cha changarawe tu kwa kuanzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mchango wake ni mkubwa sana kwenye uchumi wa hii nchi na tukifanya hivyo naamini kilimo chetu kinakwenda kuongeza thamani yake, lakini pia umuhimu wake katika kuzalisha ajira za vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kulizungumzia hap ani umuhimu wa kilimo chetu na hasa kuweka mafungamano na sekta binafsi. Benki Kuu imejitahidi, imetoa fedha zaidi ya trilioni moja kwa mabenki ya biashara na lengo hapa ilikuwa ni kusisimua sekta binafsi, na hasa sekta ya kilimo. Hata hivyo, tunaona kwamba pamoja na fedha zote hizi ambazo zimewekwa kwenye mabenki ya biashara kusisimua kilimo chetu, bado ukuaji wa kilimo ni wa kusuasua kwa maana hakikui zaidi ya asilimia tatu mpaka nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii siyo ishara nzuri katika nchi ambayo zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wake wamejiajiri katika sekta ya kilimo. Hii ni mbaya zaidi ukilinganisha na ukuaji wa sekta nyingine kama ujenzi ambayo inakuwa kwa zaidi ya asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu; kwanza tusiishie tu kuzungumza kwamba, kilimo ni uti wa mgongo, kilimo kwanza, kilimo ni siasa; hizi slogans haziwezi kutufikisha tunakotaka. Kilimo chetu kinahitaji mkakati wa kweli, kwanza wa kuboresha miundombinu kwa maana ya barabara, lakini pia pembejeo, viuatilifu, mbegu na mwisho uhakika wa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukivifanya hivi vyote kwa uhakika naamini mkulima wa Kitanzania hahitaji kuamshwa asubuhi, atakwenda kulima, atajituma kwa sababu ana uhakika wa kupata pembejeo kwa wakati, ana uhakika wa kupata viuatilifu kwa wakati na ana uhakika wa kupata masoko ya bidhaa zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kwamba kuna maeneo mengi tumefanikiwa kwenye uwekezaji, lakini eneo la pembejeo za kilimo siyo eneo ambalo tunapaswa kujisifia. Naomba mapendekezo ya Mpango wetu yaje na mkakati ni namna gani tunakwenda kuhamasisha wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa katika uzalishaji mkubwa wa mbolea na viuatilifu ndani ya nchi na makampuni binafsi ya uzalishaji wa mbegu. Haya yakifanyika yatasaidia katika kuhamasisha kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la usalama wa chakula. Waswahili wanasema adui yako mwombee njaa, kwa sababu tumbo lenye njaa huwa mara nyingi halina busara. Katika hilo wakati Taifa letu tunasema kwamba tunaweza kwenda kukutana na ukame mwakani, ni vyema tukajiandaa kuhakikisha kwamba tuna hifadhi ya kutosha ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili tumezungumza kwenye mapendekezo kwamba tunahitaji kuiwezesha NFRA. Naomba kusema kwamba hatuhitaji kuiwezesha NFRA, tunahitaji kuilipa madeni yake. Serikali inadaiwa na NFRA, ni lini inakwenda kulipa madeni haya kwa NFRA ili itumie fedha hizi katika kuwekeza maghala na kuwekeza katika ununuzi wa mazao ya wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naomba kulizungumzia ni suala zima la Serikali kuwekeza kwenye innovation kwa maana ya vijana wetu kujiajiri katika kuendeleza technology ndogondogo, lakini pia kuwekeza kwenye viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawekeza sana kwenye viwanda vikubwa, lakini wananchi wetu hawana mitaji mikubwa, wanahitaji msaada wa Serikali ku-facilitate kuwekeza katika viwanda vidogovidogo ili viwanda vikubwa viwe facilitator wa viwanda vidogo, viwanda vikubwa vitegemee viwanda vidogo katika uwekezaji wake. Najua hili liko ndani ya uwezo wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nazungumzia maendeleo ya kilimo, ni lazima tuzungumzie sekta ya maji. Hifadhi yetu ya maji siyo nzuri, vyanzo vyetu vinateketea. Wakati tunazungumzia maendeleo yetu ni vyema tukaja na mkakati wa Kitaifa kuona ni jinsi gani tunakwenda kulinda vyanzo vya maji yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ingawa siyo kwa umuhimu, Jimbo la Mikumi ni jimbo la giza, halina mawasiliano. Sisi tunaomba minara midogo kwa kimo cha Mheshimiwa Mchungahela ambayo hatuna. Afadhali ya yeye ana minara mifupi, sisi hatuna kabisa kule katika Jimbo la Mikumi, kwa hiyo ikiipendeza Serikali wakati tunakwenda katika mapinduzi ya tano ya viwanda ni vizuri wakafikiria umuhimu wa mawasiliano katika kuwezesha wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)