Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikikupendeza Bunge lako Tukufu liweze kuagiza Serikali ituletee taarifa sahihi ya miradi yote ya kimkakati inaendeleaje. Kwa sababu unakuta miradi mingi either tunajenga kwa pesa zetu mwenyewe au kwa mikopo ambayo mwisho wa siku Watanzania ndiyo wanakuja kulipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wewe unajua kwenye miradi mingi ya barabara Mkandarasi anapochelewa kukamilisha mradi, I mean Serikali inapochelewa kumlipa Mkandarasi na kusababisha mradi kuchelewa unakuta Serikali inalipa mabilioni ya shilingi kwa sababu mradi umechelewa kukamilika. Sasa nilikuwa nataka nijue status ya mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ikoje, tuliambiwa ngonjera ngonjera nyingi tu, lakini kwa habari nilizonazo sasa hivi mradi uko asilimia 45 na ulipaswa mpaka sasa hivi uwe asilimia 99 ambayo leo ni siku ya 834 mradi unapaswa kukamilika Juni 14, 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukienda kwenye vipengele vingine unakuta kukamilika kwa ujenzi wa tuta kwenye bwawa ni asilimia 43 ambayo leo ilitakiwa iwe asilimia 88, kukamilika njia ya kupokelea maji kwenye mitambo sasa hivi ipo asilimia 57, wakati ilipaswa kuwa asilimia 94, kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kazi mpaka sasa hivi ni asilimia 50 ilipaswa kuwa asilima 99, kuna mwingine kuna upande mwingine asilimia 29 ilitakiwa kuwa asilimia 98, hii ni kinyume na mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lazima tuambiwe na kuna taarifa mradi huu ukaenda mbele zaidi kuliko mkataba, lazima tuambiwe kwa kuchelewa kukamilika kwa mradi huu kinyume na mkataba Serikali yetu itamtoza Mkandarasi kiasi gani kwa siku kwa sababu hizi pesa ni za Watanzania na mkopo...

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ester Bulaya ni taarifa unapewa.

T A A R I F A

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango mzuri wa msemaji anayeongea ningependa kumpa taarifa kwamba mradi huu ulichelewa kwa sababu nyingi mbalimbali, lakini moja ya sababu ilikuwa ni sababu za kimazingira ambazo zilipelekea kuwekana sawa na wadau wetu mbalimbali wa mazingira ili mradi ule uweze kutekelezwa katika eneo lile, lakini sababu ya pili ni uwepo wa COVID-19 ambayo ilichelewesha baadhi ya mitambo kuingizwa nchini kutokana na viwanda vingi duniani kufungwa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei taarifa yake.

MWENYEKITI: Sijakuruhusu Mheshimiwa Ester Bulaya. Sasa Mheshimiwa Ester Bulaya unapokea taarifa hiyo?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya kuchelewa yote yalikuwa ndani ya miezi sita ulitakiwa ukamilike kwa miezi 36, umeenda 44 na ndiyo mpaka hiyo Juni 14, 2022.

Kwa hiyo, walizingatia huku na deadline iko pale pale kwa hiyo tunachotaka tujue tutamtoza kiasi gani kwa kuchelewesha huu mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye kazi yenyewe, wewe unajua tangu niingie kwenye Bunge hili kila taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali imekuwa ikielezea hali mbaya ya mifuko yetu kujiendesha, kuweza kulipa mafao, lakini hii yote ni kutokana na Serikali kukopa bila kulipa madeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimesoma ukurasa wa 29 wa Mheshimiwa Waziri amesema atalipa Trilioni Mbili kwa non-cash bond, nikukumbushe Kamati yako ya PAC baada ya Serikali huwa inasema hatudaiwi kiasi hiki, hatudaiwi kiasi hiki, Kamati yako ya PAC Report ya 2014 iliunda kikosi kazi kuchunguza deni na ikaleta ripoti tarehe 10 mwezi wa Kwanza 2015 ikaonesha deni la 1999 ni Trilioni 7.1 mwaka 2014. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa mbwembwe zote baada ya miaka 22 bila aibu fedha za watumishi tunaanza kupewa Trilioni 22. Sasa nikija kwenye deni kuu la mifuko mnalipa Trilioni Mbili, nikija kwenye deni kuu la mifuko ambayo ni Trilioni 19 mnahitaji miaka mingapi mkamilishe kulipa, deni la Mifuko Hifadhi ya Jamii ambayo huku ndiyo kuna hatma ya watumishi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu hivi kwanini tukikopa mikopo ya kibiashara nje mnakimbilia kulipa haraka kwa sababu mnawaogopa wale mabeberu, lakini pesa za wazawa wanazokatwa kwa ajili ya akiba baada ya maisha yao ya kulitumikia Taifa lao kwa muda mrefu kwenye 1999 tu baada ya miaka 22 mnatoa trilioni mbili mnadaiwa trilioni saba, bado huku kwenye Trilioni 19 kwa deni la ujumla sijui mtalipa kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikwambie, kwa taarifa nilizonazo, maana hapa tulikuwa tunaambiwa biashara ya actuarial, najua ya mwisho iliyofanyika 2016 ndiyo tumeambiwa Serikali inadaiwa shilingi trilioni 19. Inawezekana mambo hapa yameongezeka zaidi ndiyo maana mifuko inashindwa kujiendesha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa taarifa nilizonazo, consultant amemaliza kazi tangu mwezi wa Tano, imebaki Serikali kutoa maoni, wanaficha nini? Wanaogopa kusema mifuko ina hali mbaya au deni limeongezeka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Juni, 2020 inaonesha Mfuko wa PSSSF ilikusanya ili michango shilingi trilioni 1.3. Ilikuwa inatakiwa kuwalipa wastaafu shilingi trilioni 1.5, yaani cash walikuwa nayo kidogo kwa mahitaji ya kuwalipa wastaafu kwenye Taifa letu. Walichofanya, walienda kwenye government Security wakachukua shilingi bilioni 300, wakaongezea shilingi bilioni 190 wakalipa wastaafu na nyingine ndiyo wakaenda kuwekeza. Aibu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,…

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Pokea taarifa Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tu nimwambie Mheshimiwa Ester Bulaya, kama Serikali iliweza kupata fedha na kuwalipa wastaafu, nadhani angepasa kupongeza kwamba kumbe Serikali ilipata fedha na ikawalipa wastaafu. Hilo ni suala la kupongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Ester ni kwamba Serikali wala haina nia ya kuficha hiyo ripoti na siyo kweli kwamba Serikali inaficha hiyo ripoti ambayo Mtathmini Mkuu ameshamaliza kufanya utathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti inapokuwa tayari ina utaratibu wake katika kuiweka wazi. Naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu, ripoti hii ni mali ya wafanyakazi, mali ya waajiri, mali ya Serikali na Watanzania wote kwa ujumla, wala siyo ripoti ya Serikali. Sasa kwa taarifa yake, baada ya mtathmini kumaliza hiyo kazi, sasa hivi ndiyo tuko kwenye vikao vya utatu; wafanyakazi, waajiri na Serikali, ili kuitathmini hiyo ripoti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu kumpa taarifa kwamba hayo maneno siyo kweli Mheshimiwa Ester Bulaya, kwamba Serikali inaficha hiyo ripoti. Nadhani ni lazima tuwe tunaweka mambo wazi na tuyazungumze kwa msingi wake. (Makofi)

MWENYEKITI: Unapokea taarifa Mheshimiwa Ester Bulaya?

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siipokei kwa sababu hili goma limeisha siku nyingi, huu ni mwezi wa sita wanakaa na taarifa yao, wanaficha nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumza hapa kwamba mfuko uko hohe hahe, lakini mbali na yote na kutokulipa madeni, wanaendelea kuwapa kuwapa mizigo ya kuendelea kuwekeza kwenye viwanda 35. Wakati hawalipi madeni, bado wanawatwika mzigo, wenyewe wanachokusanya wanakosa, leo mifuko imetoa shilingi bilioni 339 kwenda kuwekeza kwenye viwanda 12, wakati huku mifuko yenyewe inakosa fedha ya kwenda kuwalipa watumishi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi hapa uliongelea kitu kizuri tu, ukaelezea ni namna gani Sheria ya Kikokotoo kuwa mbovu mpaka ongezeko la watu wanaostaafu kwa hiari limeongezeka. Nikaenda kutafuta; sasa nikwambie, baada ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutangaza kusitisha kile kikokotoo cha mwanzo na ile sheria kupita, ongezeko la watu wa fao la kujitoa limeongezeka na ongezeko la watumishi wanaostaafu kwa hiari imeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kikokotoo kipya, watu waliokuwa wakistaafu kwa hiari ni 2,562; baada ya kikokotoo kipya watu 4,730 wa fao la kujitoa walikuwa wamelipwa shilingi bilioni 21. Baada ya sheria, wamelipwa shilingi bilioni 53. Wastaafu kwa hiari kabla ya kikokotoo walilipwa shilingi bilioni 158; baada ya kikokotoo, wamelipwa shilingi bilioni 352. Walikuwa wanawahi wachukue chao mapema kwa sababu wanajua Serikali hamtabiriki, hawajui mtakuja na hatima gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna haja kubwa sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili hiyo Mheshimiwa Ester.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna haja kubwa sana ya kulinda maslahi ya watumishi wa Taifa hili. Tuacheni bla bla, tutimize wajibu wetu. Hakuna mgomo mbaya kama wa watumishi kwa sababu hawaoni wala hawezi kujisemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)