Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante awali ya yote napenda kuipongeza sana Wizara ya Fedha na Kamati yake ya bajeti kwa Mpango huu ambao sasa umetuletea na sisi tuuchakate na kuongeza mawazo yetu. Kwa dhati kabisa kwanza napenda kumpongeza Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kutimiza mwaka mmoja, lakini pia napenda kumpongeza kwa hotuba yake nzuri sana aliyotoa wakati wa sherehe zile ambayo inaleta maono na mwanga mkubwa kwa maisha ya Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla pia kuinua uchumi wa nchi na uchumi wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea natoa pongezi sana kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan kwa ukakamavu wake na ushupavu wake na uthubutu wake katika kuliongoza Taifa letu na kutuletea sisi wananchi wa Tanzania maendeleo katika kukamilisha miradi iliyoanzishwa na kuibua miradi mipya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najielekeza kwenye sekta ya kilimo, katika kuimarisha na kuinua sekta ya kilimo kwa maana ya kupata mazao bora na mazao yenye tija na kuinua uchumi wa nchi na kuongeza ajira ndani ya nchi nashauri Serikali iwekeze kwenye viwanda vya mbolea ndani ya nchi. Kama majirani zetu wanakuja kuwekeza viwanda hapa nchini malighafi za uzalishaji zinatoka hapa ndani ya nchi kwanini sisi wenyewe tusiwekeze kwanini wao waweze wana nini sisi tushindwe tuna nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini uwezo huo tunao wa kujenga viwanda vya mbolea kwa sababu tumewekeza miradi mikubwa sana ya kimaendeleo na ya kimkakati na sasa hivi yako ukingoni kukamilika. Naamini tukiwekeza kwenye viwanda vyetu vya mbolea kwa sababu tutakuwa tunaangalia nini mahitaji ya ardhi yetu na udongo wa nchi yetu tutajua afya ya udongo wa nchi yetu kwa kutumia wataalamu wetu kwenda kupima afya ya udongo na kujua ni mbolea gani ambazo zinahitajika kwa mahitaji ya nchi zikiwemo hizo UREA, MPK, mbolea ya samadi tutajua tunahitaji mbolea gani kwa mahitaji ya wananchi wetu katika kuinua kilimo chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hapo hapo kilimo tuwekeze pia kwenye viwatilifu bora kwa sababu kuna hatari ya kuingiza viwatilifu ambavyo viwatilifu vile vinakwenda kuathiri mazao ya wananchi baada ya kutumia nguvu kubwa ya uwekezaji matokeo yake baada ya kuvuna wanaharibu mazao yote na hili nimelishuhudia kuna kijana mmoja alijitokeza kulima mipapai, mipapai kaimwagilia imekubali lakini ikafanya ukungu mweupe akaenda kutafuta dawa baada ya kupata dawa mipapai yote imegeuka dume hakupata hata papai moja. Sasa hapo tunaona kwamba tunahitaji viwatilifu bora ambavyo vitasaidia wakulima wetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bashe sijui kama yuko hapa mipapai imegeuka dume yaani baada ya kiatilifu! Mheshimiwa Khadija endelea. (Kicheko)

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili nishalizungumza mara nyingi ambalo mimi binafsi linaniuma sana tunasema tunakwenda kusomesha wataalam wabobezi wa uzalishaji wa mbegu bora ubobezi wa mbegu unahitaji taaluma kubwa na inachukua muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa tuna wataalamu wetu wabobezi na walishafanyakazi na research kubwa na wakazalisha mbegu lakini wamestaafu. Matokeo yake wazalishaji mbegu bora wale wamechukuliwa mataifa jirani wanazalisha mbegu na zinarudi Tanzania tunazinunua tena sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali katika hili hebu tuangalie kwenye hiki kipengele cha ajira kwa hawa wataalamu wenye ujuzi maalum na adimu tunafanyaje ili waendelee kutusaidia kwa sababu kama wanaweza kuzalisha nje ya nchi mbegu inamaana tayari akili zao zinafanyakazi na hawajachoka wanaweza wakaendelea nchini kuzalisha zile mbegu na mbegu zikatapakaa kwa wananchi wetu bila ya kupata hasara ya kutumia mbegu ambazo hazina uhakika na hazina ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kilimo cha kukidhi mahitaji yetu kwa maana ya sisi wenyewe lakini akiba ya chakula na kuwekeza pia kwenye uzalishaji wa nje kupata fedha za kigeni. Nashauri Serikali kilimo biashara kianzie sokoni kwa maana tutizame soko linahitaji nini na mazao ya ubora wa kiwango gani ili sasa wakulima wetu wanaotaka kujiingiza kwenye kilimo biashara wajue wanalima mazao gani? Kwa ubora gani? Uhifadhi wa mazao pale ghalani na vifungashio kwa ubora gani? Ili hilo soko liweze kupatikana kwa urahisi. Kwa sababu tusilime tu bila kujua soko linahitaji nini na kwa wingi gani na kwa ubora gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kidogo nakuja kwenye mabadiliko ya tabianchi na upande wa mazingira kwa sababu na mimi mwenyewe ni mdau wa mazingira kwa sababu na mimi nahifadhi uoto wa asili kule Tabora. Masuala ya mabadiliko ya tabianchi liwe suala la kitaifa pamoja na kutegemea fedha ambazo zitatoka kwa wafadhili, lakini tuwe na bajeti yetu wenyewe ndani ya nchi ambayo tutaitumia kwa mabadiliko ya tabianchi kipindi hicho yatakapotokea majanga na maafa mbalimbali. Kwa sababu mabadiliko ya tabianchi yatakwenda kuathiri hata hicho kilimo ambacho tunakipigania, uvuvi pamoja na uzalishaji wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango umesema watahamasisha matumizi ya nishati mbadala na mimi naunga mkono matumizi ya nishati mbadala hasa kwa wakaushaji wa tumbaku kule Tabora, wapatiwe nishati mbadala kukaushia tumbaku kwa sababu wanakata miti mingi na wanaharibu mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huo huo wa kuhifadhi mazingira naomba Wizara zote za Serikali ambazo zinakuwa na miradi mikubwa ya kimkakati wanaharibu sana ikolojia na mazingira mfano, anapoweka umeme kuna ukataji wa miti mingi, kwenye mawasiliano, kwenye barabara kuna uharibifu mkubwa wa ikolojia, vyanzo vya maji na mambo mengine.

Nashauri kila Wizara inapokuwa na miradi yake ya kimkakati naya kimaendeleo itenge fedha kwa ajili ya kurejesha uharibifu wa mazingira ambao waliharibu kwa kukata miti na kuharibu ikolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamesema hapa wataongeza upandaji miti, tunashauri kwamba tusiwe tunapanda miti sasa tugeuze msamiati tuwe tunaotesha miti kwa maana ukisema kupanda miti tunaipanda baadaye mingine inaachwa haikui, lakini tukiiotesha ina maana tuishughulikie mpaka ile miti ikue.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)