Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametupa afya na uzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa hakika anafanya kazi kubwa sana ndani ya nchi yetu. Mheshimiwa Rais wetu anakidhi matarajio ya Watanzania, Watanzania ambao wana matarajio makubwa sana, lakini wanatuombea sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru wale waliotengeneza Wimbo wa Taifa, kila siku asubuhi watoto wetu wakijipanga mstari pale wanasema wabariki viongozi wote, maana yake na sisi tunaombewa. Sasa utaratibu wa kubarikiwa maana yake na wewe ufanye mambo mema, usipofanya mambo mema maana yake ni kinyume chake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Rais anafanya mambo mema kwa hakika na wale ambao ni wasomaji wa Biblia ukienda kwenye Mathayo 25 kuanzia mstari ule wa 40 utaona kuna jamaa pale waliambiwa: “…nilikuja kwako nikiwa na kiu hukunipa maji, nilikuja kwako nikiwa na njaa hukunipa chakula…”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mama Samia kwa kweli haya yote sisi watu wa Hai tunasema anastahili baraka maana kama ni maji ametuletea mradi wa bilioni 3.5, lakini kama kwenye upande wa chakula ametupa, tumepata fedha za skimu, tumepata fedha za maji. Kwa kweli, anafanya kazi kubwa sana, nimpongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Hapa kwa Waziri Mkuu niseme jambo; nilikuwa nahangaika sana masuala ya ushirika hapa, lakini kupitia yeye na Wizara ya Kilimo na Naibu Waziri leo nasema Ushirika wa Hai umeanza kufufuka. Ile mikataba ya hovyo iliyokuwepo tulienda na Naibu Waziri tukazungumza, mengine tukayavunja tukaweka utaratibu mzuri kwa vile vyama 20 ambavyo tumeanza navyo bado vingine 20. Sasa haya ni mafanikio mazuri ya kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajielekeza kwenye mchango wa leo, naomba nitumie nafasi hii pia kuwashukuru watumishi wote wa Serikali wanaomsaidia Mheshimiwa Rais kuanzia ngazi ya juu mpaka ya chini. Hawa watu wakati mwingine tunawasahau, wanatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upekee, watumishi wa afya ambao wametuvusha kwenye kipindi kigumu sana cha corona. Wametuhudumia vizuri, hawakuogopa, hawakurudi nyuma, naomba niwapongeze leo na ikae kwenye kumbukumbu kwamba, tunawashukuru sana kwa kazi nzuri waliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu niipongeza pia, Kamati yetu. Kamati hii imefanya kazi kubwa sana na kama Mheshimiwa Waziri atachukua maoni haya tunaenda kutoboa, tunaenda kuinua kilimo chetu na tunaenda kubadilisha nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niboreshe eneo moja tu na niwaombe kama wanaweza kwenda kufanya review ili iingie kwenye kumbukumbu, fedha zile walizosema ziongezwe milioni 450 hazitoshi. Kama kweli tunataka kubadilisha uchumi wa nchi hii kwa sababu, formular ya uchumi ni rahisi sana, hapa ili uchumi ukue tunatakiwa kuongeza uzalishaji, productivity. Sasa tunaongeza uzalishaji wapi, lazima twende kwenye kilimo, hatuna ujanja mwingine. Sasa hii milioni 400 waliyopendekeza, nasema iende kwenye trilioni moja, ikishindikana bilioni 800. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe na bahati nzuri leo umekuwa ukiweka chumvi vizuri sana kwenye michango yetu. Naomba na hili tuisimamie, isipungue bilioni 800 ili kweli haya yote tunayoongea yaweze kutekelezeka fedha hii iongezwe. Kwa hiyo, niombe ile Kamati itafute namna nzuri ya kusahihisha au wewe Mwenyekiti wetu utuongoze fedha hiyo iongezwe ili ikafanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi zenyewe tunazozisema, kama tunataka kilimo, lazima hatua ya kwanza tuupime udongo wetu. Kwa sababu, wananchi wanalima, lakini wanalima kienyeji wanapata shida; tujue kuna calcium kiasi gani, kuna potassium, sijui vitu gani, udongo wetu tupime. Tukitoka hapo tuwe na maji ya hakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mama Samia Suluhu ametuambia tunaletewa magari yale. Magari haya yawekwe kwenye mfumo mzuri, tuna skimu za kutosha ambazo zikijengwa tunaweza kupata maji, kwa hiyo, fedha hizi tunazoziomba zielekezwe kwenye maji. Tukitoka hapo tuhamie kwenye hatua nyingine ya kuwa na mbegu sahihi, za kwetu. Hawa Maprofesa wanaosemwa ni kweli wamejaa pale Wizara ya Kilimo wa kutosha na wameandika mavitabu kibao, ukienda pale kilimo utakuta lundo la mavitabu. Tunataka yale mavitabu yatoke Wizarani yaje huku tuyaone, watusaidie, wafanye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ifike mahali suala la mbegu liwe ni suala la kiusalama wa nchi yetu. Kwa nini nasema hivyo? Ni kwa sababu mbegu hizi wanazonunua wananchi hatuna uhakika nazo. Sawa zinafanyiwa utafiti, ile movement ya mbegu kwenda kumfikia mlaji wa mwisho hatuna ulinzi nazo. Mtu anaweza kutengeneza mbegu fake hapa, hebu fikiria mtu analima shamba eka 10, lakini anaenda kupanda mbegu fake, kwa nini mbegu fake? Sawa imefanyiwa utafiti, kule mlaji wa mwisho nani anayejua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani mbegu hizi zipite kwenye mkondo wa Kamati zetu za Usalama, zilinde mbegu yetu ifike kule kwa mlaji ikiwa ile mbegu iliyokusudiwa. Ukishakuwa na mbegu sahihi tunaendelea maeneo mengine ya kuongeza ubora wa mazao yetu. Nilitembelea nchi jirani hizi za kwetu hapa, nikakuta mazao yetu, hizi mbogamboga zinakwenda nchi Jirani, zinaongezewa thamani ya mazao na wanauza kwa fedha nyingi, sisi kwetu tunauza kabla ya kuongeza thamani ya mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana sisi pale Hai tume-design soko letu tofauti kidogo. Kwenye soko letu tukasema hapana, sisi tunataka kuwe na viwanda vidogo kama mtu analeta bidhaa yake sokoni, akinunua kwa bei ya jumla kuwe na viwanda vya kufanya sorting, kuwe na viwanda vya kufungasha, ili bidhaa ikitoka hapa iende sokoni kwenye soko la kimataifa ikiwa imekamilika, maana yake imefungashwa vizuri. Ndio maana tunaiomba sana Serikali itusaidie fedha za kusaidia soko la Kwa Sadala ambalo litakuwa ni soko la mfano. Sisi hatujaweka sijui maeneo ya saluni, sijui maeneo ya ukumbi, tumesema hapana tunataka soko letu limsaidie mkulima na huu ndio uwekezaji mzuri ambao nauzungumza hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumza kuhusu habari ya mbolea. Hili ifike mahali tuamue, tulisimamie kabisa kama ni kutafuta wawekezaji, kama ni Serikali kuingilia ndani. Hizi fedha ninazoziomba bilioni 800 au trilioni moja zifanye kazi ya kuwa na kiwanda hiki. Wameshafanya study ukiwauliza watakwambia, ukienda vizuri unauliza enhee, hivi kwani kutengeneza kiwanda cha mbolea ni shilingi ngapi? Wanazo analysis vizuri, wameandika kwenye vitabu, lakini sasa nani afanye?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ifike mahali tukishindwa kupata mwekezaji Serikali ifanye kwa maslahi mapana ya kuinua uchumi wetu. Hii asilimia tunayoambiwa asilimia 65 kwamba, hawa ndio wamepata ajira. Kama asilimia 65 ndio wamepata ajira, pengo linatokea wapi kwenye pato la Taifa tunabaki na asilimia 26? Maana yake kuna watu wanatoroka hapa. Wanatoroka kwa nini, hatuwawezeshi. Tuwawezeshe warudi ili uwiano uliopo kwenye ajira uwe ndio uwiano ulioko kwenye pato la Taifa, hapo tutakuwa tumeinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze hapa wakati wa bajeti iliyopita, wakati tunajadili Mpango uliopita tuliambiwa kutakuwa na Bodi ya Uwagiliaji. Niombe Waziri atakaporudi hapa atuambie mchakato wa kuanzisha hii Bodi ya Umwagiliaji ambayo naamini itaenda kuhakikisha wakulima wetu wana vyanzo vya kutosha vya maji, Bodi hii itaanza lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu, wenzangu wamechangia sana kwenye kilimo, niombe ifike mahali utuongoze, umesema Bunge hili linaenda kuwa la kuimarisha kilimo, kweli tukafikie hapo na tusimame imara kabisa kwa sababu huu ndio ufunguo wa kuinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihame kidogo niombe.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda hauko upande wako. (Kicheko)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)