Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2022/2023, ikiwa ni maandalizi ya bajeti ijayo. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima kukutana jioni ya leo. Pili, nichukue nafasi hii kumpongeza sana na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa anayoifanya ya kujenga nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi ameendelea kuunganisha nchi yetu na dunia kuhakikisha kwamba, anashirikiana na nchi nyingine katika kuiunganisha nchi yetu kidiplomasia. Sisi tumekuwa tukipata faida kubwa sana ya kimaendeleo na fursa lukuki za kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya Watanzania na ukiangalia ni juzi tu tumetoka kupata fedha ambazo zinaenda kupunguza matatizo makubwa ambayo tunayo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na huduma nyingine za kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze moja kwa moja kwenye Mpango ambao umewasilishwa na Waziri wa Fedha. Nichukue nafasi hii kumpongeza yeye pamoja na wasaidizi wake kwa Mpango waliotuletea ambao unatupa fursa sisi kuanza kuuchambua na kutoa maoni yetu; nikianza na dhima ya Mpango wenyewe ambao unaeleza kwamba, ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipita kwenye eneo hilo wengi wetu tumeeleza hapa, asilimia zaidi ya 65 ya Watanzania wanafanya shughuli za kilimo. Wote tusipoongelea kilimo maana yake tutakuwa hatujagusa Watanzania wengi ambao tunafanya nao kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili kama ulivyosema mwenyewe kwenye mpango haijaelezwa kinagaubaga, ni namna gani Serikali imejipanga kuwekeza fedha za kutosha kuhakikisha kwamba, tunabadilisha kilimo ambacho kinaajiri watu wengi. Kwenye eneo hili tusipoongea kwa kina na kujadiliana kama Taifa hatuwezi kuvuka. Eneo ambalo unapata fedha kwa maana ya unaingiza pato zaidi ya asilimia 26 huwezi kuacha bila kuwa na mpango mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo, ukiangalia eneo hili ni kwamba, tunapiga kelele sasa hivi, leo tunaenda kwenye msimu wa kilimo hatuna mbolea na mbolea iko juu sana, lakini juzi tumetoka kuazimia hapa kama Bunge tukaielekeza Serikali itafute fedha za kununua mazao ya wakulima. Kwa hiyo, kuna mambo mawili yanagongana hapo, tunahamasisha wakulima walime, lakini mwisho wa siku hakuna masoko ya kutosha ambayo yalipaswa yafanywe na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, leo tunataka kwenda kwenye kilimo chenyewe pamoja na athari za UVIKO-19 Serikali ina wajibu wa kuwasaidia wakulima hawa ili tusiendelee kulalamika. Kwa hiyo, nadhani kuna mahali ambapo hatutimizi wajibu wetu kama Taifa. Naomba na nilishasema hapa kwenye Bunge lako siku za nyuma, sehemu ambayo ina wasomi wengi ukiangalia Maprofesa, Madokta na baadhi ya watu ambao wamesoma vizuri nenda ukaangalie ni sekta ya kilimo, wako pale Wizarani pamoja na maeneo mengine. Wamefanya researches za kutosha, wametoa ushauri wa kutosha, lakini tatizo lililopo tuna tatizo la kutenga fedha za kukisaidia kilimo cha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunaongelea habari ya bajeti ya bilioni 80, wakati tunasema sisi tunataka kufikia malengo ya kuongeza kilimo cha umwagiliaji ambacho kinahitaji uwekezaji wa kutosha. Hatuko serious kama Taifa kama hatujaingia kwenye eneo hili.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mtaturu nikuhakikishie wale Maprofesa na Madokta walioko Wizara ya Kilimo hawana hata robo eka wao wenyewe. Kama wewe unayajua mashamba yao nipeleke siku moja nikaone. Ahsante, endelea kuchangia. (Kicheko)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunikumbusha hilo. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba, tupo kwenye theory zaidi, hatupo kwenye practical. Kwa hiyo, ombi langu kwa Serikali, kama kweli tunasema tunataka kuwekeza, wengi wetu toka jana na juzi wamesema, tuhakikishe tunapata angalau trilioni moja iwekezwe ndani ya sekta ya kilimo ili tuweze kupata Maafisa Ugani wa kutosha, tuweze kuwa na mbolea ya uhakika, lakini zaidi tuwe na uhakika wa Maafisa Ugani ambao ni wataalam wa kilimo kwenye vijiji vyetu. Tusipofanya hivyo, hatuwezi kuvuka na hatuwezi kukibadilisha kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea habari ya kilimo cha kutegemea mvua, leo hii wenzetu wa hali ya hewa wametuambia kwamba, tutakuwa na mvua chini ya wastani msimu unaokuja. Je, mkakati uko vipi katika eneo hili kupitia Mpango huu ambao tunaenda kuuweka? Tunayo taarifa nzuri tunaletewa na Serikali, hali ya hewa wametuambia hatutakuwa na mvua ya kutosha, sisi kama Taifa tumejiandaaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, tunasubiri baadaye tuje tuseme kulikuwa na changamoto ya mvua chache wakati tulijua kabla. Kwa hiyo, nadhani kwenye eneo la uwekezaji tumesema hapa kuhusu mabwawa, tumesema hapa namna ya kilimo cha umwagiliaji, lakini tumejiandaaje kweli kuwasaidia wakulima wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda kila halmashauri hapa inaongelea habari ya upungufu wa Maafisa Ugani, ambao ni wataalam. Leo wakulima wengi wanalima kilimo cha kurithi, kilimo kilekile cha mazoea ambacho mtu anapata debe mbili, tatu kwenye eka moja, kitu ambacho anapoteza muda tu. Kwa hiyo, ombi langu kwenye eneo hili, Mpango uweze kubainisha bayana namba gani tutaweza kutoka kumsaidia mkulima ambaye yuko pale kijijini ambaye kwa hakika anaweza kuendelea kusaidia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu namna ambavyo amejitahidi kupita kila mahali anahamasisha kilimo hiki. Anahamasisha kilimo mbalimbali…

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge makofi kwa Waziri Mkuu jamani. (Makofi)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumpigie makofi mengi Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

MWENYEKITI: Kweli kabisa. katika eneo la kilimo amehangaika sana, kushoto, kulia na kasi. Endelea Mheshimiwa Mtaturu. (Makofi)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndio maana nimembatiza Mheshimiwa Waziri Mkuu, yeye ndio Afisa Ugani Mkuu katika nchi yetu. Anafanya kazi nzuri ya kuhamasisha kilimo, pasipowezekana panawezekana kwa namna ambavyo anakaa na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ninao alikuja Singida amekaa na sisi siku nzima bila kutoka kwenye kiti. Tukaweka mkakati wa namna ambavyo zao la alizeti litaenda kusaidia nchi hii katika mafuta ya kula. Kwa hiyo, kwenye hili Mheshimiwa Waziri Mkuu tunampongeza na sisi kama Wabunge tuiombe Serikali iongeze fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, maeneo hayo tunakwenda vizuri. (Makofi)

MWENYEKITI: Nikupe Taarifa uende nayo Mheshimiwa Mtaturu, Singida safari hii kwenye alizeti mtakuwa wa pili baada ya Dodoma. (Makofi)

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwa sababu, wewe mwenyewe umesema ndani ya Hansard imeandikwa, tunaendelea tutakukumbusha. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka niongelee eneo la miundombinu. Ili uweze kuleta uchumi, uchumi uimarike lazima uwe na miundombinu mizuri ya kutoa mazao kwenye maeneo ya wakulima. Eneo hili nitakumbusha barabara ambazo zimetajwa miaka yote; mfano, Barabara ya Mkiwa – Itigi kwenda Makongolosi. Barabara ile ilitengewa fedha, ikasemwa tutaanza kwenye Mpango uliopita tutajenga kilometa 50, lakini juzi wamesema kilometa 20 na mpaka sasa tunavyoongea bado haijatangazwa hata kutangazwa. Hili nalo ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Barabara ya Singida – Kwamtoro kwenda Kiberashi mpaka Tanga; nayo barabara ile ilitengewa kilometa 20, mpaka leo haijaanza. Tunategemea nini kama Mpango huu hauwezi kwenda kutekelezwa na kuwa na mpango.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili, Mheshimiwa Mtaturu.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno haya, naomba nirudie tena kusema Serikali ijipange vizuri kuleta mpango mzuri ambao utakuja kutusogeza mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)