Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Agnesta Lambert Kaiza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami kwa uchache niweze kuchangia katika Mpango huu. Ili Mpango wowote wa maendeleo uweze kutekelezeka kunahitaji nguvukazi yenye afya bora. Chombo pekee kinachoshughulika na masuala mazima ya kununua na kusambaza dawa na vifaatiba ni bohari kuu ya dawa yaani MSD. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya PAC ya tarehe 18 Agosti, 2021 imeweka bayana jinsi ambavyo deni la Serikali kwa MSD imekuwa ni changamoto kubwa sana inayopelekea MSD ishindwe kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi. Deni la Serikali mnamo tarehe 18 Agosti kama nilivyosema, ilikuwa imefikia shilingi bilioni 269. Baada ya PAC kuikaripia Serikali kwamba sasa inazorotesha ufanisi wa MSD, mnamo mwezi Septemba Serikali ililipa shilingi bilioni 39 tu kutoka katika deni la shilingi bilioni 269. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe mnamo mwaka 2018 na 2019 deni la Serikali kwa MSD ilikuwa ni shilingi bilioni 53.63 na kwa kipindi kile kwa mujibu wa CAG, alisema MSD ilikuwa na hali mbaya, mbaya, mbaya sana. Sasa linganisha deni lile la shilingi bilioni 53.63 na deni la sasa la shilingi bilioni 269; unaweza kuona namna gani MSD wana hali mbaya. Kama MSD ina hali mbaya, basi Watanzania tuna hali mbaya sana. Nimesema Serikali imelipa shilingi bilioni 39 tu mpaka sasa na kufanya balance ya deni liwe ni shilingi bilioni 230 mpaka wakati huu ninapokuwa naongea mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunatambua, bila ya kuwa na nguvu kazi yenye afya bora, Mipango yote tunayoipanga hapa kamwe haiwezi kutekelezeka kwa ufanisi. Tumesikia au niseme nimesikia na nimesoma taarifa ya Kamati ya Bajeti na niseme naipongeza sana Kamati hii kwa sababu imefanya kazi nzuri sana, kwa msemo wa sasa wanasema Kamati hii imeupiga mwingi sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Kamati ya Bajeti inasema, MSD ina hali mbaya na hivyo basi, inahitaji shilingi bilioni 363.39 ili iweze kufanya majukumu yake kwa ufanisi. Yaani hapo MSD wanahitaji mtaji. Kwa lugha nyingine MSD hivi tunavyoongea haina mtaji kabisa na tupo hapa tunapanga mipango ya maendeleo ambayo wanaokwenda kuitekeleza hawana uhakika wa afya bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya bajeti inasema, bajeti inaelekeza kwamba Serikali itenge shilingi bilioni 150 ipeleke MSD. Hiyo ni sehemu ndogo angalau ya bajeti halisi ya shilingi milioni 363.93. Ni wazi kabisa, kwa changamoto ya MSD jinsi ilivyo, hata leo hii tukisema tupeleke shilingi bilioni 150, chombo ambacho hakina mtaji kabisa, shilingi bilioni 150 haiwezi kutosha kabisa, kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mawazo yangu, shilingi bilioni 150 haiwezi kutatua changamoto zilizopo MSD. Ni kwa nini nasema hivi? Tumesema MSD inahitaji mtaji wa shilingi bilioni 363.93 lakini inaidai Serikali shilingi bilioni 269 na kwa sasa imebaki shilingi bilioni 230 kama balance ya deni. Kwa hiyo, leo hii ukipeleke shilingi bilioni 150 MSD, kwanza unawaongezea stress tupu, kwa sababu hazitoshi kuagiza dawa, hazitoshi kulipa madeni na mwisho wa siku sasa wanabaki wanajiuliza, hizi fedha tuzifanyie jambo gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri wa Fedha inayohusu Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2022/2023 kwa maana ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, ameeleza katika ukurasa wa 14 mpaka ukurasa wa 15, naomba nimnukuu, anasema: “Upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya umefikia asilimia 94.”

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge katika Majimbo yetu tujiulize, ni kweli tumefikiwa kwa asilimia 94? Kama haitoshi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha akaenda mbali akasema, “shilingi bilioni 234 zilitolewa kwa ajili ya kununua dawa na shilingi bilioni 26.3 kwa ajili ya vifaa tiba.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo realistic. Nayasema haya kwa sababu kuu mbili; kwanza, PAC imesema, Kamati ya Bajeti imesema na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa mnamo tarehe 10/10/2021 aliongea na Waandishi wa Habari akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Naibu Waziri wa Afya, akawaelekeza na akasema baada ya kutoka kwenye ziara aliyokuwa anaifanya, alikuta kule chini kwenye Mikoa, kwenye kanda kwenye Wilaya, kote kabisa hali ni mbaya. Hali ilikuwa ni mbaya kweli kweli, na Mheshimiwa Waziri aliwaelekeza na kuwapa wiki moja wawe wametekeleza jukumu la kushusha dawa. Sasa hii asilimia 94 inatokea wapi? (Makofi/Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inatokea wapi? Je, tuamini Mpango, tumwamini Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuiamini PAC au Kamati ya Bajeti? Where? Wapi? Ni nani tuweze kumwamini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa…(Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Nusu dakika.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, nafahamu hivi karibuni tumepokea mkopo wa shilingi trilioni 1.3. Ili kuondokana na aibu hii iliyopo ya MSD nashauri mambo makuu mawili. Kwanza itengwe shilingi bilioni 600 zipelekwe MSD kwa sababu ya mambo makuu mawili; mosi, ikamalize balance ya deni la Serikali ya shilingi bilioni 230. Iikisha-clear hiyo shilingi bilioni 230, ina maana kwenye hiyo shilingi bilioni 600 tutakuwa tumebaki na shilingi bilioni 363.93 ambayo ndiyo mtaji halisi wa MSD wanaouhitaji waweze kufanikisha majukumu yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Agnesta. Najua muda hautoshi. Ahsante sana, muda haupo upande wako.

MHE. AGNESTA L. KAIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba wakati nakaa, Waziri anapokuja ku-wind up atuondolee mkanganyiko huu wa taarifa tatu; atuambie tuuamini Mpango, tumwamini Mheshimiwa Waziri Mkuu, tuiamini PAC au tuiamini Kamati ya Bajeti?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)