Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Elibariki Emmanuel Kingu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuweza kushiriki kutoa mchango wangu katika mapendekezo ya mpango, lakini pia kwa mpango ambao tunaendelea nao kuutekeleza wa mwaka 2020/2021. Mimi ninakwenda kuzungumza maeneo mawili tu kwa kifupi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu la Tanzania idadi ya ajira ambayo ni active employment katika sekta ya kilimo ni zaidi ya Watanzania inakadiriwa kwa mujibu wa ripoti ya SAGCOT, inakadiriwa kwamba Taifa la Tanzania watu waliojiajiri katika kilimo ambao ni adult wanacheza kati ya watu Milioni Saba mpaka Milioni Nane na wakati mwingine ripoti zingine zinaonyesha kwamba watu walioajiriwa katika sekta ya kilimo wanafika milioni 9.6 mpaka milioni 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mara nyingi sana huwa nakufuatilia unapokuwa umekaa kwenye kiti chako unapokuwa unatoa dondoo za kuchomekea kwa upande wa Serikali. Huwa najifunza mambo mengi sana na huwa nayachukulia hayo madondoo unayoyasema huwa nayachukulia in a very serious way. Wiki iliyopita ulitoa dondoo ambayo ilikuwa inatoa msisitizo wa kuikumbusha Serikali katika suala zima la kuangalia nini Serikali inaweza ikakifanya, katika suala zima la kuwasaidia wakulima wetu kutokana na hali ilipo sasa ya masuala mazima ya mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme neno moja. Pamoja na kwamba Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan, imefanya vizuri sana katika mambo ya revenue collection kwa kweli hilo tunawapongeza sana, hatukutegemea kama revenue collection zingeweza kwa utulivu lakini mapato yakaongezeka katika kukusanya. Tunampongeza sana mama na Serikali yake sana sana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme neno moja, nilipokuwa Mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 2015 wakati ninakaa kiti cha pale nyuma mchango wangu wa kwanza kwenye Bunge lako hili Tukufu, niliishauri Serikali ya Chama changu kama kweli tumedhamiria kumkomboa mkulima wa Taifa hili, mkulima wa nchi hii atakombolewa peke yake kwa Taifa kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga mabwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilienda mbali nikatoa mfano nilipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Igunga, tuna Mito inaitwa Mito ya Manonga inayounganisha Mikoa ya Tabora, Simiyu na Shinyanga, nikatoa mfano kwenye Bunge hilo Hansard zako zikipekuliwa zitasema. Mimi ninachojiuliza hivi kwa nini wenzetu upande wa Serikalini michango ambayo inaweza mkaichukua ikawapa hata ninyi Mawaziri legacy kwamba, mmeweza kulisaidia Taifa katika eneo fulani kwa nini kila mara tunakuja kama vile tu show? Tunazungumza mambo ya msingi yanayozungumzwa na Waheshimiwa Wabunge hayachukuliwi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonekana kama tu basi fulani kesho Mheshimiwa Nape naye pia atachangia aonekane ametimiza jukumu lake la kuzungumza Bungeni, kwa nini constructive ideas zinazotolewa na Wabunge Serikali hawazichukui na kutekeleza? Mimi hapo napata wakati mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kujenga mabwawa nimetoa mfano kwa Wilaya ya Igunga bwawa pekeyake la Mwanzugi, lenye ujazo wa maji mililita milioni 20 lina uwezo wa kuzalisha mpunga unaozalishwa na lile bwawa moja lililojengwa toka enzi za Hayati Mwalimu Nyerere lina uwezo wa kulisha nchi karibia za Afrika Mashariki katika mchele ninaweza nikasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wewe ulikuja kuzindua kampeni kwangu hili huwa siachi kulisema. Ulikwenda kwenye Kata za Iyumbu na Mgungira sisi kule tuna mabonde, tukijenga bwawa moja tunaweza kutoa ajira ya watu wasiopungua zaidi ya 25,000 ajira za moja kwa moja, lakini mchele unaweza ukasafirishwa kwa Mataifa zaidi ya matano. Serikalini jamani kwa nini hamtaki kuweka hizi legacy? Mheshimiwa Nape amezungumza hapa kwa uchungu sana, mimi nasema na Bunge hili niseme wazi mbele ya Wabunge hawa, tukimaliza vikao vya Bunge kama hatujazungumza ultimatum ya kuwasaidia wakulima juu ya disaster iliyoko mtaani ya mbolea tutahukumiwa na Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Bunge hili tutamaliza kukaa vikao vyetu vyote hatujaiagiza Serikali yetu iliyoko madarakani kwenda kuwasaidia wakulima, kuhakikisha ya kwamba kuna subsidies zinawekwa kupunguza ukali wa bei za mbolea pamoja na mbegu tutakuwa hatujalitendea haki hili Taifa. Nataka niseme kama tunaweza kuwaangalia wamachinga tukasema wamachinga tukapeleka Shilingi Bilioni Tano sijui ngapi, hapa leo tunazungumza voters of this country. Lakini mimi mwenyewe huku cha ajabu nimeshangaa nimesoma huu mpango kwa kweli lazima tukosoane ili tuweze kwenda mbele lazima tukosoane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika sekta ya kilimo na toka juzi nilikuwa namsumbua Naibu Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe nimemsumbua sana kwenye simu, nilipoona yuko busy Kaka yangu alinijibu tu kwa haraka haraka nimemtafuta Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo nikamwambia hebu naomba unipe takwimu masuala mazima ya mbolea na mambo kama hayo.

Ninachoweza kusema ni kwamba kama Serikali yetu itakuwa tunakuja Bungeni hapa Wabunge tunazungumza kutoa michango ya kulisaidia hili Taifa, lakini tunaonekana kwamba tu ni mazoea tu fulani atachangia, fulani atachangia, hatutalisaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kujenga mabwawa kwa ajili ya kuwa na zone za kilimo cha umwagiliaji wakati umefika msaidieni Rais, Mheshimiwa Bashe jengeni mabwawa angalau kila Mkoa pawe na mabwawa matatu makubwa. Kwa Dodoma jengeni bwawa litakalowasaidia wakulima wa zabibu, Singida kajengeni bwawa litakalowasaidia wakulima wanaolima mpunga pamoja na alizeti, pamba kwa upande wa Kanda ya kule kwa Wajomba zangu Wasukuma, Taifa hili litakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa tuliyonayo Watanzania sisi tuna tabia moja ambayo ni nzito sana naomba niiseme kwa ruhusa yako. Sisi ni wazuri sana katika kuzungumza lakini katika kutekeleza mambo yanayoweza kuleta mapinduzi ya maisha ya Watanzania tuna kigugumizi kikubwa sana. (Makofi)

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

SPIKA: Nimekuona Mheshimiwa Olelekaita.

T A A R I F A

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nataka nimpe ndugu yangu taarifa tu hapa, kwa mujibu wa Ilani yetu mfano tu, kwa sekta ya mifugo tulisema tutajenga mabwawa 400 na change nyingi kidogo hivi, lakini kwa mwaka huu uliopita Wizara ya Mifugo peke yake wametengewa fedha ya kujenga mabwawa matano tu na ilitakiwa mabwawa 91. Sasa tukiendelea na trend hiyo kwa miaka mitano ijayo maana yake ni kwamba tutajenga mabwawa kama 20 hivi kati ya 450 na hiyo ni mfano tu. Kwamba tusipobadilisha mwelekeo na mipango ikaweza kujibu Ilani inavyosema maana yake tutakwenda hatutafanya vizuri zaidi. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Taarifa hiyo unaipokea Mheshimiwa Kingu?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii naipokea kwa unyenyekevu mkubwa kwa sababu ninajua Kaka yangu pia anatoka kwenye jamii ya wafugaji. Wafugaji na wakulima ni watu wamoja, ahsante sana kwa taarifa ninaipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nataka kumalizia kusema ni kwamba, chukulia tu mfano tunaposema kilimo kina ajiri adult kwa mujibu wa takwimu za SAGCOT, watu Milioni Nane mpaka Milioni Tisa ndugu zangu tunapozungumzia ajira ya watu Milioni Nane mpaka Milioni Tisa tunazungumzia ajira ya Taifa, yaani kama kuna jambo tunatakiwa tulifanye Bunge hili ni kuilazimisha Serikali yetu kwenda sambamba na matakwa ya wakulima ambao ndiyo voters wetu wengi waliotuleta katika Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaambia Waheshimiwa Wabunge ikiwa tutakuja kwenye Bunge hili tukasahau kuwasemea wakulima, tukasahau kuwasemea wafugaji, tukasahau kuwasemea wafanyakazi na watu wengine, hakika mimi ninakuambieni vizazi vitaandika kumbukumbu na tutakuja kuhukumiwa, kwa sababu tutakuwa tumesahau kundi la watu ambalo ndiyo wanabeba roho ya uchumi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, tunajenga madarasa 3,000. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kama alivyosema Mheshimiwa Nape. Mama ameonesha uwazi wa hali ya juu katika mikopo aliyoipata na namna mikopo ilivyotumika. Kwenye hilo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini madarasa haya 3,000 kuna jambo hapa kwenye Mpango sijaliona…

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Ndiyo, taarifa.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, madarasa ni 15,000 siyo 3,000.

MWENYEKITI: Unapokea taarifa hiyo Mheshimiwa?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba kaka yangu Mheshimiwa Tabasam aende taratibu. Haya ninayosema ni ya shule za awali, shule shikizi na kuna madarasa mengine 12,000 kwa ajili ya sekondari. Kwa hiyo, nilikuwa natoa takwimu katika...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha, wind-up.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapo-windup ni kwamba madarasa 3,000 katika shule shikizi ina maana tunakwenda ku- recruit wanafunzi 120,000; wapi? Tuna madarasa 12,000 ya sekondari, ina maana tunakwenda ku-recruit wanafunzi 480,000; wapi? Kwenye Mpango nilitegemea Serikali ituonyeshe namna gani imejipanga kuziba gap la upatikanaji wa walimu na vifaa vya kufundishia kwa madarasa haya tuliyoyajenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusipofanya hivi, tutajikuta tumejenga madarasa, wanafunzi wamekwenda, na jambo la uhaba wa walimu linazaliwa. Haya ni mambo ya planning na namna ya kuweza kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)