Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa na mimi nafasi hii niweze kuchangia. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kunipa kibali cha kuweza kusimama hapa leo nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu wake kwa hotuba nzuri sana ya mwelekeo wa mwongozo wa mpango wa mwaka 2022/2023. Lakini pia nikupongeze wewe na Naibu Spika kwa kazi nzuri ambazo mnaendelea kuzisimamia katika Bunge hili ambalo kwa kweli unaliendesha kwa kiwango cha hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuungana na Wabunge wenzangu kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu, Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri ambazo anaendelea kulitumikia Taifa letu bila kujali tofauti zetu za kisiasa, udini, kanda, ukabila, na wote tunashuhudia; mama kazi iendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ameweza kushusha fedha nyingi sana katika miradi ya maendeleo kwa nchi yetu, miradi ya afya, elimu, maji n.k. lakini pia kwa Wilaya yangu ya Nyang’hwale kwa kweli Mheshimiwa Rais ameweza kutumwagia fedha nyingi kwa kipindi kifupi, zaidi ya bilioni nane kwenye miradi mbalimbali ya afya, elimu, maji, miundombinu hadi TASAF. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni mfupi sana kwa leo, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, nizungumzie upande wa sekta ya madini; sekta hii hivi sasa na yenyewe inachangia sana pato la Taifa. Lakini pamoja na uchangiaji wa pato kubwa la Taifa kutokana na madini hizo fedha ambazo zinapatikana kwa wachimbaji wadogo ni fedha ambazo tunaona ni nyingi sana, lakini nasema ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba sana katika mpango huu tuweke mkakati wa kuweza kuwawezesha wachimbaji wetu wadogo ili waweze kuweza kujipatia kipato na kuongeza kipato cha Taifa. Leo hii tunasema sekta ya madini imechangia zaidi ya bilioni 500, ni wachimbaji wanaotumia sululu, je tukiwawezesha wachimbaji hao tutakusanya mabilioni na tutapata mabilioni mengi kutokana na hawa wachimbaji wetu wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapohapo kwenye upande wa sekta ya madini, Mheshimiwa Waziri ninaomba sana sasa hivi kumekuwa na utoroshwaji mkubwa sana wa dhahabu inayotokana na uchenjuaji wa kutumia mercury. Kwa hiyo ninaomba sana tuweke mikakati madhubuti ya kuweza kuitambua ile mialo na kuwatambua hawa wachennjuaji wanaotumia mercury ili tuweze kuidhibiti dhahabu hiyo ambayo sasa hivi inatoroshwa kwa wingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo bilioni 500 ambazo tumezipata zinatokana na wale ambao wana elution machine na wale ambao wana VAT leaching. Lakini kwa hawa wachenjuaji wadogo kwa kweli dhahabu zao hazukusanywi ipasavyo, kwa hiyo Taifa linapoteza mapato sana. kwa hiyo kwenye mpango wetu huu wa 2022/2023 tuweke mkakati ulio mzuri zaidi tuweze kuwatambua hao wenye mialo ili tuweze kuzikusanya hizo dhahabu tuweze kuongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naomba pia nizungumzie kuhusu TRA; ushauri wangu, kwa kweli naiomba Serikali kupitia TRA waweze kuongezewa kibali cha kuajiri watumishi ili waweze kuwa wengi, waweze kudhibiti huu mtindo uliopo sasa hivi ambao wafanyabiashara wanakwepa sana kutoa risiti kwa sababu watumishi wa sekta hiyo ya TRA wanakuwa ni wachache, hawapiti maeneo mbalimbali kufanya ukaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nalisema ushahidi wake ninao. Kwa sababu unapoingia dukani mpaka sasa hivi bado kuna mtindo wa wafanyabiashara anakuuliza nikupe bei ya risiti ya mkono ama ya EFD machine. Kwa nini wanasema hivyo; ni kwa sababu usimamizi haupo wa kutosha. Kwa hiyo, ninaomba sana TRA wajaribu kuangalia upande huo. Bado Serikali inapoteza mapato makubwa sana kwa wafanyabiashara wetu kwa sababu bado wanakwepa kutoa risiti za EFD machine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe ushauri mwingine kuhusu suala hilo la TRA. TRA izidi kabisa kuendelea kutoa elimu ya mlipakodi, lakini pia kwa waanyabiashara wetu pamoja na wanunuzi. Elimu hii bado inahitajika sana, kwa sababu leo unakuta mtu anaulizwa nikupe risiti ambayo ni ya mkono au ya EFD machine, anapewa bei mbili tofauti kwa sababu elimu hiyo haijawafikia vizuri sana Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natoa ushauri kwamba tuweke mikakati ya kutosha kuhusu hawa wao wafanyabiashara wanaokwepa, ama kuwaongezea adhabu. Lakini pia wanunuzi wanaonunua bila kuomba risiti atakapokamatwa na kifaa ama bidhaa ambayo haina risiti inabidi naye adhibitiwe na afikishwe sehemu husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Sisi Wabunge tuliomo humu, kwa ushahidi ninao kabisa, tunakutana maeneo mbalimbali iwe kwenye maduka ama kwenye huduma mbalimbali, huwezi ukamkuta Mbunge anaomba risiti, wakati ni kiongozi. Kwa hiyo, na sisi Wabunge hebu tuwe sasa mstari wa mbele kuanza kuomba risiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili uthibitisho ninao. Nikiwauliza hapa Waheshimiwa Wabunge tunaoingia kwenye migahawa wangapi tunatoka na risiti? Tunaoingia kunyoa vipara ama kutengeneza saluni ya akinamama, akina mama wangapi Waheshimiwa Wabunge wanatoka na risiti za saluni, wangapi? Kwa hiyo, nasema hayo kwa sababu nina ushahidi na tunakutana maeneo hayo mbalimbali, na sisi pia kama viongozi tuwe mfano wa kuweza kukusanya kodi kwa ajili ya pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. (Makofi)