Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu. Jambo la kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anaendelea kuiongoza nchi hii na jinsi anavyoiweka kwenye ramani ya dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia hotuba aliyoitoa katika Umoja wa Mataifa, lakini tumeshuhudia pia hotuba aliyoitoa juzi; zote zimeleta matunda mazuri sana katika nchi yetu. Kwa kweli tunampongeza sana sana. Pia tunampongeza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na pia Rais wa Zanzibar kwa namna wanavyoshirikiana katika kuziongoza nchi zetu hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kuleta Mwongozo huu wa Mpango na Bajeti wa mwaka 2022/2023. Kwa kweli ni mwongozo mzuri na ambao kwakweli nadhani tukiujazilizia jazilizia, basi unaweza ukaleta matunda mazuri sana. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niipongeze Kamati ya Bajeti kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuchambua Mpango huu, Mkakati huu na Frame Work hii na mpaka hapa walipofikia.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya msingi ambayo kwa kweli yamezungumzwa katika Mpango huu na nimefurahi sana kuona dhima iliyoandikwa katika Mpango huu ambayo imeandikwa kwamba Kujenga Uchumi Shindani na wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Dhima imekaa vizuri sana, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri, isipokuwa Dira bado sijaiona kwenye hii labda Mheshimiwa Waziri angeiweka na Dira, nayo ikakaa vizuri, short and clear itatuweka vizuri sana mahali pazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yapo mambo ya msingi ambao Mpango wowote, Mwongozo wowote tunaoutoa na Mpango tutakaokwenda kuutekeleza, yapo mambo muhimu ambayo lazima Mpango wowote utakaokuja uende kuyajibu. Tutapenda Waziri atakapokuja na Mpango huo basi majibu halisi yapatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, jambo la kwanza ni umaskini uliokithiri katika maeneo mengi, Tanzania sasa hivi kuna umaskini mwingi. Sasa framework hii ituelekeze namna tutakavyoenda kukabiliana na umaskini wa nchi hii, umaskini wa watu walio wengi tutakavyoondokana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni suala la ajira. Ajira kwa vijana wetu, ajira katika nchi hii ambayo imekuwa ni tatizo kubwa. Sasa lazima framework hii ituelekeze namna tutakavyoweza kutatua tatizo la ajira katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, ni ukuaji mdogo wa uchumi. Uchumi wetu hauendani na rasilimali tulizonazo, ukuaji wake bado upo chini sana. Sasa ni namna gani tunaenda kujipanga, tunakuja na mipango gani, tunatekeleza vipaumbele vipi na kwa namna gani ili uchumi ukue kwa kasi kubwa inayolingana na rasilimali tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hayo ni mambo muhimu ambayo tutapenda yawepo katika mpango ambao tunategemea uje. Kuna teknolojia duni ambayo imekuwepo katika nchi yetu, huduma duni katika maeneo mengi, lakini uongozi usiokuwa na maono katika baadhi ya maeneo. Sasa hivi Rais wetu na viongozi wa juu wana maono mazuri sana, mawaziri wana maono, lakini tuna tatizo la uongozi kutoka kwenye ngazi ya kati na kushuka chini. Sasa hili lazima tuliangalie vizuri, namna tutakavyoliweka vizuri ili sasa mambo yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo pia tatizo la mapato kidogo ya Serikali. Ukiangalia mapato yetu ya Serikali sasa hivi makusanyo kwenye upande wa kodi ni asilimia 13 ya GDP na Mpango sasa hivi unaelekeza kwamba framework hii tutaenda kukusanya asilimia 16 ya Pato la Taifa. Sasa nadhani bado tupo chini ukilinganisha na nchi zingine zilizoendelea na nchi za wenzetu zinazoendelea kwa speed kali sana. Kwa hiyo ni muhimu tukayaangalia haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimeangalia uwiano wa ukuaji wa mchango wa Sekta mbalimbali katika uchumi wa Taifa letu. Nimeangalia kwa mfano ujenzi, ilikuwa kwa asilimia 9.1 na imetoa mchango kwenye pato la Taifa kwa asilimia 14.4; lakini ukichukua Uchukuzi imekuwa kwa asilimia 8.4 na imechangia kwa asilimia 7.5 kwenye pato la Taifa; Madini ilikuwa kwa asilimia 6.7 na imechangia kwa asilimia 6.7.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya kwenye huu Muongozo haijaonyesha kilimo kilikuwa kwa asilimia ngapi? hili halijaonyeshwa, lakini imeonyeshwa mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa ambao ni asilimia 26.9. Sasa kilimo kinatoa mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa, lakini kilikuwa kwa kiwango gani na tuweke mikakati gani ili kilimo kikue kifikie katika kiwango tunachokitaka, hili nafikiri ni muhimu tukaliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia viwanda, biashara vyote hivi vimeonyeshwa mchango wake kwenye pato la Taifa, lakini vimekua kwa kiwango gani ili tutoke hapo sasa, Mpango utuelekeze tunataka tufike asilimia ngapi ya ukuaji ili tufikie malengo yetu, bado Mpango huu haukuweza kueleza. Sasa nafikiri hayo ni mambo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia vile vile uwiano wa ugawaji wa rasilimali ambao tunaenda kuufanya sasa. Sekta zipo kama tatu; kuna Sekta za Uzalishaji ambazo ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi hii. La pili, kuna Sekta za Biashara na Huduma na sehemu ya tatu ni Huduma za Jamii. Sasa katika uzalishaji wote, lazima tuuangalie katika Mpango huo na katika Mpango unaokuja tuone rasilimali zinaenda kuwekeza kwa asilimia ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo swali ambalo tunajiuliza ni kiasi gani rasilimali zitatengwa kwenda kwenye Sekta za Uzalishaji na hasa kilimo ambacho kinaajiri watu wengi ambapo kwenye kilimo hapo ndiyo tunapata chakula chote, fedha za kigeni na wananchi wetu wanapata ajira yao, lakini ndiyo tunapata ajira nyingi kwa sababu ndio tunapata malighafi zote za viwandani, uchumi wetu kwa kiwango kikubwa unategemea kilimo. Sasa ukikichukua kilimo kwa mapana yake ndiyo unaweza ukatatua hata tatizo la umaskini na tatizo la ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namna gani tunaenda kufanya hilo ili kusudi tuone sasa sekta inatengewa kiasi gani, asilimia ngapi inatengwa kwa ajili ya kwenda kwenye sekta za uzalishaji, zikiungana na Sekta ya Uvuvi, Sekta ya Ufugaji, Sekta ya Madini, Viwanda, Utalii na Mazingira na hizo ndiyo sekta za uzalishaji, rasilimali kiasi gani zinaenda kutengwa kwa ajili ya kwenda kuongeza uzalishaji kwenye maeneo hayo. Tukiongeza uzalishaji kwenye maeneo hayo maana yake hata eneo la biashara litakaa vizuri, biashara itakaa vizuri, mambo mbalimbali ya biashara yatakwenda vizuri, lakini ndipo huduma za jamii tutakapokwenda kwenye maji, elimu, afya, ushauri na utafiti yatakaa vizuri. Sasa lazima tuwe na jedwali lile linaloonyesha mgawano wa hizo rasilimali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri tumefika mahali sasa tuweke malengo shabaha. Shabaha za kila sekta, tunataka sekta ya kilimo ikue kwa asilimia ngapi, ichangie kwa asilimia ngapi? Ili tunapofanya kazi tukajipime kwa kiwango hicho. Kama ni ufugaji tufanye hivyohivyo, kama ni biashara tufanye hivyohivyo, kama ni huduma tufanye hivyohivyo. Basi nafikiri hili litatusaidia sana katika kuweza kuimarisha ukuzaji wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naangalia mambo muhimu, nchi ya kwetu ndiyo pekee ina bahari, ina maziwa, bandari pale, hivi tutaimarishaje? Kwenye kilimo, upatikanaji wa mbegu. Sasa hivi hali ni mbaya, mbegu sasa hivi nimesikitika sana, mpaka leo tunapoongea mwezi Novemba Serikali bado haijatangaza hata bei za mbolea, haijatangaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezoea huwa wanatutangazia bei elekezi. Tunaponunua mbolea kwa mfuko wa pamoja huwa kunakuwa na bei elekezi, mpaka leo hazijatangazwa. Tunakwendaje kuzalisha, wakulima wa nchi hii wanakwendaje sasa kuzalisha, ambayo itaathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu. Kwa hiyo, nilidhani kwamba hilo ni muhimu sana Mheshimiwa Waziri angeliangalia waone kitu ambacho kinaweza kufanyika ili kiweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia hali ya uchumi sasa hivi, kwa mfano mazingira yamebadilika, mvua hazijanyesha. Kule Mikoa ya Mbeya, Songwe, tunategemea sana mvua za mwezi Septemba na Oktoba kwa ajili ya zao la kahawa. Sasa hivi hazikunyesha, zimeanza kunyesha mwezi Novemba. Maana yake maua yote ya kahawa yameshaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwaka mzima mwakani hatutaweza kupata kahawa ya kutosha. Sasa mkakati tunauwekaje ili kukabiliana na hii hali. Kwa hiyo, ninadhani ni maeneo muhimu sana ya kuyaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie Reli ya TAZARA, itachangiaje kwenye uchumi. Siyo tu suala la kwamba hii reli inamilikiwa na nchi mbili, suala ni kwamba tunaongezaje mabehewa ya kuweza kusafirisha mizigo mbalimbali ili hii treni isaidie katika kukuza uchumi wa nchi yetu, hata kuishia pale mpakani tu. Tutajengaje pale kituo bandari kavu ili mizigo kutoka Dar es Salaam ifike pale nchi za SADC waje kuchukulia eneo hili. Nafikiri ni kitu ambacho lazima tukiangalie vizuri.

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)