Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Raisi kwa kazi nzuri anayoifanya, na mim ni mmojawapo wa watu ambao kwa kipindi chake tumeshanufaika na mabilioni ya Mheshimiwa Rais Samia. Nimepata madarasa siyo chini ya sabini, lakini kwenye barabara nina zaidi ya Billioni Nne ni kazi kubwa sana, tunampongeza sana na tunamuombea aendelee kufanya kazi na kusaka pesa Watanzania waweze kufaidi Urais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba katika mpango unaoandaa hebu angalia ukamilishaji wa miradi. Tunakuwa na miradi mingi ambayo haifiki mwisho, ukiangalia kuna baadhi ya Halmashauri mpya zilipewa Billioni Moja za kujenga majengo na ramani ikaletwa ya ghorofa, leo tunamaliza mwaka hamna hela wala sioni kama kuna dalili ya kupewa tena hela ya kumalizia kwa kipindi kifupi, watu wameshamaliza majengo utakuta wengine wameweka na kenchi mbao zinaoza mirunda imeoza, ikija tena Bilioni Moja mnakuwa tena kama mnaaza kukarabati majengo upya. Kwa hiyo ninaomba katika mpango wako upange kukamilisha ile miradi ambayo Serikali ilikuwa imeianzisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vivyo hivyo Mheshimiwa Waziri hata kwenye hivi vituo vya afya ulivyotoa pesa milioni 250 tutajenga majengo mengine yatafika renta na ramani mmeleta, mengine yatakamilika tutabakiza ukamilishaji, tena tunasubiri miaka miwili mitatu ndiyo unafikiria kutuletea, kwa hiyo ni vizuri ukatoa kama ni hizi chache mlizotoa zikamilishwe ziishe ili mwakani muanzishe nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza hapa kuna watu wengine humu ndani wana Hospitali za Wilaya bado hazijakamilika mpaka leo, kuna wengine pesa zao zilichukuliwa na mfumo wa Serikali ule wa mwezi wa sita mpaka leo Halmashauri yangu inadai milioni 290 mpaka leo, sasa tunaenda kuanzisha zingine. Kwa hiyo, ni vizuri mpango mzuri ni ule unaokamilisha na watu wanaanza kukitumia, tunaanzisha vitu tunasema vizuri majukwaani halafu kitu kinakuwa ni jengo halina huduma, haliwasaidi Watanzania na sidhani kama wanafaidika sana na hiyo mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linguine tunazungumza kukuza Shirika latu la Ndege, nimeona kwenye mpango unataka tukushauri unajenga viwanja, Mheshimiwa Waziri, ninashauri tu naona hapa Dodoma hatujakaa vizuri, uwanja wa Dodoma unatumika mwisho saa 12. Ninyi wenyewe ni mashahidi ukiwa na kazi Dar es Salaam umeitwa Dodoma tunakimbizana kweli kuvizia ndege kila siku imejaa. Uwanja ule uliwekwa taa za kutua usiku lakini feki, kwanini msiweke taa ndege ikatua mpaka Saa Mbili, Saa Tatu, Saa Nne tukawa na route za usiku, tumefungiwa taa mpya mpaka leo zinamaliza mwaka hazifanyi kazi, bora kama tulipigwa famba na Mheshimiwa Waziri agiza taa tumalize uwanja huu uwanja wa kiuchumi, watu wanataka kuja kufanya kazi Dodoma wamalize mikutano Saa Mbili wakalale Dar es Salaam, haya ndiyo maisha Mheshimiwa Rais anasema nchi imefunguka kwa hiyo tufunguke vitu vyote siyo kufungua vitu nusu nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumza kwa upole sana suala la wamachinga maana nikizungumza kwa ukali nitasemwa mimi siyo Mtanzania, lakini nilivyolisema mwanzo nadhani watu hamkunielewa. Nikishukuru sana Chama cha Mapinduzi kupitia Mwenezi wake alinisaidia, niposema niliambiwa mimi ni Mrundi siyo Mtanzania lakini Mheshimiwa Mwenezi wangu kwa sababu yeye ni mweupe nilitegemea alivyosema wangesema yeye ni Mwarabu, sasa kwa vile imekuwa ngoma draw nitalizungumza kwa upole sana.(Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka vijijini nami ni mkulima wa mpunga, tunavyozungumza leo gunia la mpunga ndani ya mwezi mmoja limeshafika Shilingi 90,000, mimi nimeuza jana shilingi 90,000 na wiki mbili tatu tulikuwa tunauza shilingi 40,000 hadi shilingi 50,000 nikawa najiuliza huu mpunga tunauza nchi gani ambako kumefumka njaa, hakuna! yaani mchele umepanda hapa hapa ndani kwetu nikajiuliza swali ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya research kulingana na akili yangu kidogo tu, kwamba walaji wa mchele sasa hivi wameongezeka, ukienda huko Njombe, Lushoto na sehemu zingine wauza viazi vya chipsi wanalia vinaoza hamna walaji! Kwangu nauza mananasi tulikuwa tumezoea ukipeleka mananasi Mjini wananunua machinga hawa wanakatakata wanawauzia watu Shilingi Mia Mbili, Mia Mbili, Mia Moja linanunulika, hakuna Watanzania wengi wanaoweza kununua nanasi la Shilingi Elfu Tatu au tikiti maji ambalo lilikuwa linauzwa kwenye kapu shilingi 500 sasa hivi hayanunuliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge niwaambie ukiondoa kama hatuna maisha ya Kibunge hata mimi naamini humu ndani Wabunge wenzangu kwamba kama Wasukuma wenzangu tunazaa watoto 10 - 15 bado Shangazi na nani wamekuja kukusalimia, unaweza kweli ukakaanga chipsi mkala mlo wa usiku, utaweza hiyo gharama za kuandaa chipsi? kwa hiyo watu wote wamerudi kwenye wali, tunakula tunabakiza na kiporo cha chai! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanasomesha wana watoto labda 15, wana Watoto watatu hata Dar es Salaam, mtoto anatoka Mbagala anasoma shule ya Uhuru, ulikuwa unampa elfu moja, maisha ni magumu elfu moja anakula chipsi kavu kwenye nailoni, sasa hivi machinga wote wamefurumshwa mnataka watu wakale kwenye restaurant. Kwa hiyo, ni vizuri mimi nilielewa kabisa Mheshimiwa Rais alivyosema tukawaandalie mazingira mazuri, mazingira mazuri ni yapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo yameandikwa public interest labda mimi kwa sababu sijui kizungu yana kazi gani? Kwa mfano Mnazi Mmoja ile ipo wazi, public interest sasa hivi wamebaki kukaa mateja tu wavuta unga kwanini msiwaweke pale wamachinga, unamtoa mtu unampeleka Mbagala kwa hiyo ni vizuri Mheshimiwa Waziri tuchunguze vizuri kwamba tunawatoa watu tunawapeleka kule tunapobaki hapa tunaanzisha vita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mimi nina duka Kariakoo nijitolee mfano nina siku ya Saba sijauza kila siku ninatuma nauli hapa, hebu jifikirie mfanyakazi wangu ambaye nilikuwa nampa elfu tatu posho ya chakula leo anatakiwa akale restaurant chai Shilingi Elfu Mbili, mchana Shilingi Elfu Tano inakuwa Shilingi Elfu Nane nitaitoa wapi? Kama mnabisha Waheshimiwa Wabunge wewe nenda tu pale Kariakoo sasa hivi pale Congo, utaona kila anaefungua duka ana mfuko una hotpot, watu wanakuja na makande, watu wanakuja na wali wa kiporo, haiwezekani kuhudumia kwa sababu hatuuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nakushauri sana Mheshimiwa Mwigulu, jaribu kuliangalia na bahati nzuri umenitaja nakushukuru maana wewe ni Waziri wa Fedha inawezekana una takwimu vizuri kwamba mimi ni tajiri, mimi ni zao la machinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, machinga wapo wa aina tofauti, kuna machinga mwingine anashinda tu mlangoni kupiga debe anakaribisha watu anapata elfu mbili, usifikiri watu wote wana mitaji na hao wenye mitaji ndiyo wanaowawezesha machinga huwezi kuwatenganisha, ukiwatoa machinga mtaa wa Congo biashara imekufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaofanya research ni machinga, unataka unitoe Mwenge nikanunue Congo halafu nije nimepanda daladala, machinga akinunua Congo anakuja kwa miguu anauza barabarani, kwa hiyo ni vizuri hili zoezi tulichukue kwa uzuri. Hata ukiangalia nilikuwa napata takwimu za Mkoa wangu wa Geita, vijijini tunataka kwenda kupiga watu Katoro kuwatoa machinga, hatuna mtaro wa maji, hatuna waenda kwa miguu, hatua yaani ‘bagosha’. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufike mahala kwa kweli kwenye mpango najiuliza vizuri, mlitengeneza maandiko mazuri sana mkajenga stendi mkajenga masoko, chukua mfano soko la Kisutu, soko la kuku bahati nzuri kuku zinatoka kwa Waziri wa Fedha kwa Mwigulu, kuku ya Singida huko Kinampanda unaipeleka kwenye soko ya kioo na kigae, ikidonoa hivi inaumia mdomo, ikiangalia juu kuna taa hee! Zimeshindikana, ndiyo maana Rais anawaambia jamani haya masoko mengine tuyageuza yawe ukumbi wa starehe hamumuelewi! Kwa nini msifanye hizi gharama za kuandaa stendi na masoko ya ajabu ajabu mkawekeza kwa wamachinga kuliko kuwatesa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli najiuliza mpaka kuna masoko mengine ambayo machinga tumeanzisha wenyewe, tunaenda kupigwa. Mfano Mwanza Nyamagana, kuna soko linaitwa Buhongwa kule barabarani watu wameenda wameanzisha miaka na miaka, leo eti unatengeza mazingira bora, unaenda unawatoa barabarani unawapeleka dampo wanapotupa vinyesi….

MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha umenipata vizuri kuhusu kuku.