Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia draft hii ya Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza nianze kwa kuelekeza shukrani zangu kwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi ambayo anaendelea kuyafanya na kuhakikisha kwamba wananchi wetu wanaendelea kunufaika. Nitoe shukrani za pekee baada ya wananchi kutoa kilio cha bei za mahindi na kupelekwa kwake alitoa shilingi bilioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa mahindi na fedha hizo kwa kweli zilifanya kazi kubwa tu ya kuhakikisha kwamba mahindi yananunuliwa na niliona mwenyewe kwa sababu hata Jimboni kwangu fedha hizo zilifika. Tunatoa shukrani nyingi sana kwa niaba ya wananchi wote ambao walinufaika na angalau bei ikaweza kuwa stable kidogo kutoka pale ilipokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze kwenye mambo machache ambayo nimeona ni vizuri nikitoa ushauri kwa Serikali wakati wa kuandaa mpango ambao tutakuja kuupitia utakapokuwa umekamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba niweke nyongeza kidogo kwenye ukurasa wa 68 wa Mpango unaohusu zao la chai, naomba niikumbushe Serikali kwamba wametaja Njombe, wametaja Lushoto, lakini Kilolo imesahaulika pale nafikiri ni makosa ya kiuchapishaji, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili basi akafanya marekebisho kwamba pia nako kule kuna mashamba makubwa yana zaidi ya miaka 30 na nimeshasema hapa kwa muda mrefu hilo ninafikiri litakuwa ni kosa la kiuchapishaji kwa sababu Kilolo isingeweza kusahaulika kwa sababu hata Waziri wa Kilimo ameshatembelea tayari.

Kwa hiyo, nafahamu analijua, kwa hiyo utakaporudi mpango nitaiona kwa sababu ni kitu ambacho kinafahamika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa kilimo hasa kwenye mahitaji ya mbolea, nchi yetu inahitaji mbolea kiasi cha kama tani laki saba na hivi tunavyozungumza ukisoma mpango hata kwenye utekelezaji pale haukusema mbolea iliyokwisha ingia ni mbolea kiasi gani. Mpango pia hauoneshi mipango ya kuingiza hii mbolea kiasi gani zaidi ya kusema kuna kiwanda hapa Dodoma, kuna mwekezaji kutoka Burundi atajenga, kwa hiyo tunatarajia kitakapokamilika na hatujui hicho kiwanda kitakamilika lini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeambiwa na watabiri wa hali ya hewa kwamba mwaka huu tutapata mvua za wastani au chini ya wastani, maana yake ni kwamba mikoa michache sana itakayopata mvua na hiyo ndiyo inayotegemea ilishe nchi yetu. Kwa hiyo upo uwezekano mkubwa wa kutokuwepo na chakula cha kutosha au kuwa na mabaa mawili baa la kwanza linalotokana na asili ambalo ni baa la kukosa mvua, lakini baa la pili ni baa ambalo tunalitengeneza wenyewe la kuto kutoa ruzuku kwenye mbolea na kusababisha mbolea hiyo iwe bei kubwa na kuwafanya wakulima wasinunue. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo wale wakulima wanasubiri mvua kidogo inayonyesha, kwa mfano baadhi ya Mikoa mvua zimeanza hawajapa hilo punguzo la hiyo mbolea wala ruzuku na wala Serikali mpaka sasa haijasema chochote kwa sababu ameshatoa maelekezo tunaamini kabla ya Bunge hili kuisha basi tutasikia. Pia kwenye mpango ili hii iwe endelevu ningependa kushauri kwenye mpango utakapokuja basi tujue ni mpango gani wa muda mrefu utakaofanya wakulima waweze kupata nafuu ya mbolea kama ilivyo kwenye nchi za jirani ambazo baadhi yake wengine wamezitaja walipokuwa wakitoa michango yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo ningependa kutoa ushauri ni kuhusu mikopo kwa vijana, akina mama na wenye ulemavu na hasa mifumo inayotumika. Ningependekeza kwenye mpango unapokuja sasa mwanzoni ilikuwa vikundi viwe vikubwa baadaye ikawa watu watano pendekezo langu ni kuwa, lengo la mikopo ile ni kuongeza ajira, mawazo ya kutengeneza mradi ili uweze kuleta ajira si lazima iwe watu watano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu mmoja anaweza akatengeneza mpango wa kukopesha watu na akaajiri zaidi ya watu ishirini wakati kikundi kinaweza kikawa cha watu watano na kikawa na mradi wa kufanya wao watano peke yao. Maana yake ni kwamba mpango uje na vigezo vinavyofanya hata kijana mmoja, hata mwanamke mmoja, hata mlemavu mmoja kukopa ili mradi anazalisha ajira nyingi kwa vijana, wanawake na watu wengine na hiyo itasaidia sana kwa sababu inaonekana wasiwasi ni uwezekano wa kulipa, kwa hiyo kuna dhamana zinazoweza kutengenezwa na nyingine zilishawahi kupendekezwa hata humu ndani, watu wapeleke vyeti ziwe dhamana wamemaliza degree zao au vitu vingine vyovyote vinavyoweza kuwa dhamana, au basi vijiji na maeneo watu wanaofahamiana vidhamini, lakini hii mikopo lengo ni kuzalisha ajira mtu mmoja apewe kusiwe na hii kusema wangapi ili mradi anazalisha ajira kwa watu wengi zaidi kwa sababu lengo ni kukuza uchumi ni kuweka mzunguko wa kutosha. Kwa hiyo, kigezo cha vikundi kinaelekea kupitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite pia kwenye kitu kingine cha miundombinu hasa vijijini kuhusu suala la barabara. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ametoa fedha…

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!

MWENYEKITI: Taarifa nafikiri inatoka Msekwa. Taarifa kutoka Msekwa, Mheshimiwa Jacqueline Msongozi nafikiri.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo. Nataka nimpe taarifa mchangiaji anayechangia sasa Mheshimiwa Nyamoga kwamba kuhusu suala la mikopo kwa vikundi itoshe tu kwamba Serikali inatoa pesa kwa ajili ya vikundi kwa maana ya asilimia 10 (4:4:2), lakini mikopo hii iwe yenye tija. Unakuta kikundi cha watu hamsini wanakopeshwa milioni mbili bado hiyo pesa haitaweza kuleta tija kwa watu hamsini shilingi milioni mbili. Kwa hiyo, ikiwezekana vikundi mbalimbali viwekewe pesa ya kutosha ili waweze kuanzisha hata viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Justin Nyamoga unaipokea taarifa hiyo.

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeipokea. Nijielekeze kwenye mpango wa TARURA, tumefurahi sana tumepewa wengine Bilioni 1.5, wengine Bilioni Moja kwa ajili ya barabara na kwa kweli fedha hizi zimesaidia sana tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu sasa kwa sababu ukiangalia tulivyojadili mwaka jana tulikuwa tunasema kwenye mfuko wa barabara iwekwe sheria zigawanywe ielekee... mpaka sasa TARURA ilianzishwa lakini chanzo chake cha mapato hakijawa kile ambacho ni mfuko kama ilivyo mifuko mingine, mfuko wa maji, mfuko wa barabara na mifuko mingine. Kwa hiyo tunagemea Mheshimiwa Rais akitoa kama hivi na tunamshukuru anaendelea kutoa na mwakani labda itafanyika hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ingekuwa kwenye huu mpango kama hizi fedha zipo na zinaendelea kuwepo basi ianzishwe programu kama ilivyo programu nyingine ambazo zimekuwa zikianzishwa na zinapewa fedha, labda iitwe Rural Road Maintenance Program na iwe na mipango kabisa ili tusiwe tunaenda kwamba leo kuna fedha tujue mpango huu labda ni wa miaka mitatu, miaka minne na tuta-cover barabara ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo TARURA ije wakati wakuja wana mpango, waje na mpango wa ukarabati wa barabara za vijijini unaoeleweka ambao utasababisha sasa fedha zinazopatikana zinapelekwa na zinaenda moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho ningependa kushauri kwenye mpango ikiwepo ni miradi ya kimkakati kwenye Halmashauri na nina uhakika kwa sababu hili suala ni la Wizara ya Fedha Mheshimiwa Waziri analifahamu. Vile vigezo vilivyopo vya kupewa miradi ya kimkakati tumekwisha kuvilalamikia sana kwamba vinatengeneza ubaguzi katika kunufaisha Halmashauri hasa zile zenye vipato vidogo na zile zenye hati chafu na hati zenye mashaka. Kwa hiyo, tulikuwa tumependekeza kwamba vigezo hivyo vipitiwe ili viweze kuwa rafiki kwa Halmashauri zote. Pendekezo langu ni kwamba mpango huo utakapokuja basi uwe unataja kwamba vile vigezo kwa sababu mara nyingine kwenye Kamati tulikuwa tumeambiwa unapitiwa basi tuambiwe kwamba vimepitiwa na vipo kwa namna gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)