Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ali Hassan Omar King

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Jang'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Awali ya yote, nami namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kupata uhai na uzima wa kuhudhuria Bunge lako hili Tukufu, leo tunajadili Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2022/2023 ambao utakwenda kuwa bajeti huko mbele kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kitu kimoja; chanda chema huvishwa pete. Chanda chema huvishwa pete. Nakusudia kwamba anayefanya mazuri, basi ni lazima asifiwe kwa mazuri na ndiyo maana ya chanda chema huvishwa pete. Maana yake pete huwa kama ni tunza. Sasa kwa nini tunasitasita kuyasema yale mazuri ambayo yamefanywa na hii Serikali ya Awamu ya Sita? Kwa nini tunasita? Pete ambayo tutamvisha mama, tunasema mama mitano tena 2025 – 2030. Hiyo ni pete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa haya mazuri ambayo ameyafanya. Nafikiri kwa Majimbo ya Tanzania Bara katika masuala ya TARURA, walipata kila Jimbo shilingi bilioni 1.5, katika shilingi trilioni 1.3 zimekwenda kwenye madarasa. Wengine wana madarasa 270 na wengine wana madarasa 300. Sasa haya ni maendeleo ambayo ndiyo tunayotarajia. Ndiyo maana tukasema, chanda chema huvishwa pete. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati, sisi Watanzania tuna kawaida ya kuwa na mawazo mgando. Mtu mwenye mawazo mgando kule kwetu sisi huwa tunamwita tozobi. Kwa hiyo, wapo matozobi ambao hawatambui lile jema ambalo linafanywa hata kama analiona. Sasa kwa kuwa akili yake imeganda, mtu kama huyu huwa anaitwa tozobi. Huyo hata awe na jina kubwa vipi, lakini huyo ni tozobi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuepukane na kuwafuata matozobi. Nasi wengine tukawa matozobi kwani huoni kinachofanyika? Huna macho? Au ndiyo bwegenazi? Macho matatu, lakini hakuna jicho hata moja linaloona!

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, amewasilisha vizuri sana. Waheshimiwa Wabunge. ripoti ya Kamati ya Bajeti ni ripoti ya Wabunge wote. Kama utakuwa unazo ziada zako, nawe unaweka pale inputs zako. Ripoti ya Kamati ya Bajeti ni ripoti ya Wabunge. Wewe kama ni Mbunge, ina maana hii ni ripoti yako, unaipingaje? Unaipingaje? Kama una yako, weka, lakini hii imefanyiwa kazi kitafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwaambieni Waheshimiwa Wabunge, hii ni ripoti yetu sote. Nina usemi mmoja, wanasema kwamba bubu hutaka kusema mambo yanapomzidia. Nami leo mambo yamenizidi, nataka niseme. Nataka kusema kwenye kilimo. Sijawahi kusemea kilimo, lakini leo naona nisemee kilimo. Nasema kwenye kilimo, namuunga mkono Mheshimiwa Spika Job Ndugai, alisema Bunge hili la Kumi na Mbili liwe ni Bunge la Kilimo. Kwa hiyo, naunga mkono mawazo yote ambayo yametolewa na Wajumbe au Wabunge wa Bunge hili kuhusiana na kilimo, yote waliyoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naongeza kusema usemi ule ule unaosema kwamba mtemewa mate na wengi, hulowa. Mheshimiwa Waziri, uwekezaji katika Kilimo bado haujatosheleza. Kamati ya Bajeti imeshauri tutenge shilingi bilioni 450 kwa sababu kilimo kinachangia kwenye pato la Taifa kwa asilimia 26.6, lakini hiki kilimo kimeajiri Watanzania asilimia 67. Ina maana kwamba kama tuta-invest zaidi kwenye kilimo, impact ya kukua kwa uchumi itaongezeka zaidi kwa Watanzania wengi na kila mahali tutapagusa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tukiwekeza kwenye kilimo, tukija tuki-set inflation, rate ambayo tunaitaka tutaipata kwa sababu tayari mazao ya kilimo yatapanda bei kubwa. Ina maana kwamba inflation itazidi kwa maana kwamba tuki-control tukiwa tume base kwenye kilimo, tutakuwa tuko vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ukuaji wa uchumi, kwa kuwa inachangia asilimia 26.6, tuki-invest zaidi ina maana kwamba tutapata ukuaji wa uchumi mkubwa zaidi. Hapo hapo katika mauzo ya nje, kama tutakuwa tumeuza mauzo ya nje mengi katika balance of payment tutakuwa tume-improve. Kwa mauzo ya nje hayo hayo, exchange rate yetu itakuwa stable; katika mauzo hayo hayo ya nje pia kutatusaidia katika masuala mengi. Kwa kuwa GDP itaongezeka, hata kile kipimo cha uhimilivu wa deni la Taifa, kwa sababu itakuwa GDP imeongezeka kuwa kubwa zaidi na deni la Taifa litakuwa halijakua sana, ina maana kwamba tutapata zaidi uhimilivu wa deni la Taifa na itakuwa rahisi kwetu sisi kupata mikopo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, kiwango cha umasikini kitapungua kwa sababu asilimia hiyo ya kilimo itakayokuwa imeongezeka ni kubwa mno na Watanzania wengi watakuwa wamefaidika. Sasa mimi niseme jambo moja katika vihatarishi kwenye Mpango huu. Naomba hili, kwa kuwa haya ni mapendekezo ya Mpango, naomba hili Waziri alichukue. Kihatarishi tulishaambiwa, tutakuwa tuna mvua chini ya wastani. Kwa kuwa tutakuwa tunamvua chini ya wastani na sisi tulisema kwenye Bunge la Kumi na Moja wakati wa Covid-19, Rais alituhamasisha tulime, tukalima tukapata mavuno mengi. Sasa hivi tumelima huko mahindi mpaka yameshuka bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali iongezee mtaji wa NFRA kwa ajili ya kuhifadhi vyakula hivi. Kuhifadhi vyakula hivi, tutanusurika na balaa ambalo linataka kuja, lakini tutapata na mbegu. Ukipita huu muda wa mvua hizi ambazo ziko finyu, ina maana kwamba tutalima tena. Kwa hiyo, ushauri wangu nauweka kwa Serikali kwamba; kwanza, kutoka shilingi bilioni 234.1 tuweke shilingi bilioni 450, Mheshimiwa Waziri tunalisema hilo wazi. Kwa kuziweka hizo, zikafanye kazi gani? Hizi tukapate pembejeo za kutosha, pia muda sahihi na kwa bei nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika hicho kilimo, tukatengeneze mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji. Kingine, zile kodi na tozo kwenye mazao ambazo zinakera, tukiziondoa tutaweza kuweka kama ruzuku, kwa maana hiyo, hayo tutayafikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashauri katika kihatarishi. Kwenye kihatarishi, sisi watu tuliosoma soma vitabu, Mashehe kama sisi, huwa tunajua Nabii Yusuf; Mfalme aliota ndoto akasema kwamba raaitu sababa karatul simani yakul huna sabuna hijaf. Nimeota ng’ombe saba walionona wanawala saba waliokonda. Wasabu sumbulat nhudhuri wa bukharu yabisat. Na mashuke saba mabichi na mengine saba makavu. Kwa hiyo, Mfalme akataka taawil, apewe tafsiri ya ndoto. Nabii Yusuf alimjibu kwamba mtalima miaka saba, itakuwa ya neema, lakini itakuja miaka saba ya njaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hifadhini chakula kwa ajili chakula na kingine kwa ajili ya mbegu kwa miaka ambayo mvua zitaanza kunyesha tena. Kwa hiyo, nami natoa ushauri huu kwamba kwa kuwa tumeshatabiriwa kwamba mvua zitakuwa finyu, tuweke chakula, tuhifadhi. Kuhifadhi ina maana kwamba, hifadhi ya chakula cha Tanzania ipewe mtaji kwa ajili ya kuhifadhi. Utakapokuja muda wa njaa, watu watatutegemea; na sasa hivi watu wanatutegemea, tulilizungumza hili mwaka jana 2020. Tumelima kwenye Covid, tukapata mazao mengi, faida yake tuje tuipate hapa sasa hivi. Tumeshaambiwa mvua hazitakuwa sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda nichangie mchango huu wa kilimo katika nchi yangu hii na hilo ndiyo maana nikasema kwamba bubu hutaka kusema mambo yanapomzidia. Limenizidi mwenzenu, leo nasimama mbele yenu, kauli yangu kwenu kuitoa. Kwa hiyo, nami hii kauli kwangu ilikuwa siyo ya kawaida kuzungumzia kilimo, lakini leo imenipasa nizungumzie kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashukuru sana. Tunaiomba Serikali, kwa kuwa haya ni mapendekezo, hebu ajaribu kutazama, tuki-invest kwenye kilimo, tutavuka. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)