Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia hii nafasi.

Vilevile namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema, ambaye ametujalia kuwa na afya njema na kupata faraja, tunafurahi kama wenzetu wanavyozungumza humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wangu wote, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama mpambanaji ambaye ameamua kutupeleka mbele katika mapambano ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawashukuru watendaji wote akiwemo Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika na Waziri wangu ambaye ni Mjumbe katika Kamati yetu ya Bajeti, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba. Huyu mimi namwita mpambanaji. Ninaamini kwa haya anayoyasikia humu ndani atayafanyia kazi ili utekelezaji wake uwe mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba ni Balozi wa Watu Wenye Ulemavu; anawapenda walemavu na ninapenda kumpelekea salamu zake kama walemavu wanasema wanakupenda, tena karibu sana, uwe nao karibu. Nao wana imani kuwa katika Mpango wako hautawaacha nyuma walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia upande wa kilimo. Kilimo kinachangia uchumi wa shilingi trilioni 44, sawa na asilimia 26.9 ya pato kubwa la Taifa ambalo ni shilingi trilioni 163, lakini ukuaji wake ni 3%. Tujitafakari na tulitathmini, kwa kundi kubwa la asimilia 66 ya Watanzania, wanapata ajira na mapato yao kupitia kilimo. Katika ukuaji huu wa 3% mpaka 4% bado tuna changamoto kubwa katika eneo hili. Maeneo mengine ni ya watu wachache, lakini unapozungumza kilimo, unamzungumzia mkulima aliye kijijini, ambaye anategemea Bunge hili limkomboe na limtoe katika umasikini kumpeleka mbele. Kama uchumi tuna asilimia tatu, tunahitaji nguvu ya ziada katika eneo la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wote humu ni mashahidi, tunakwenda kukutana na changamoto za wanavijiji wakiwa katika hali ngumu na wanahitaji msaada wa kukombolewa. Niliongea katika Kamati ya Bajeti, tumepata pesa za Covid, lakini mkulima hayumo. Kama mkulima hayumo, ina maana siyo priority; lakini kwa vile ni mpango tunataka kuutekeleza hela nyingine zote zilizobakia tuzifanyie mpango tuone tunafanya nini ili kuingiza pesa katika bajeti ya kilimo ili iweze kumkomboa mwananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaizungumzia leo Novemba na Novemba tayari tunategemea mvua za vuli zinaingia na hatuna mbolea. Mbegu hakuna. Tusimame kwa Pamoja, hakuna haja ya kumwambia yule amekosea, amekosea, hapana. Watanzania twende kwa umoja wetu, tujue changamoto hii ya mbolea, ya pembejeo na mbegu tunalifanyia kazi. Tutume haraka kabisa, maana yake tukisema tunangojea muda fulani, suala hili linatakiwa maamuzi yake yawe ya haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika Mkutano Mkubwa wa Mabadiliko ya Tabia ya Nchi Duniani, mnaiyona kama ni rahisi sana. Tunazungumzia uchumi wa dunia unaozungumzwa katika nchi za Umoja wa Mataifa. Nimeangalia katika baadhi ya magazeti, nimeyasoma na ma-bulletin zimetolewa grant nyingi sana za kilimo. Kilimo wamekitangaza, small grant kwa ajili ya wakulima. Je, sisi Watanzania tuliokaa humu ndani, hatuna ripoti yeyote tunazopata kwa wenzetu wanapokwenda katika mikutao mikubwa kama hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni matumaini yangu kutoka sasa hivi, wale wanaokwenda kutuwakilisha katika mkutano mkubwa wa Climate Change waje watupe mabadiliko ya tabia ya nchi na nini inabidi tufanye kwa Tanzania katika masuala ya kilimo, masuala ya afya na masuala mengineyo ambayo yanahitaji kubadilisha uchumi wetu kutoka hasi kwenda katika maeneo chanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata nafasi ya kutembelea bandari. Nilikuja na hoja ya Bandari ya Mtwara na Bandari ya Tanga. Tuipe kipaumbele. Nikupe taarifa, ninaona njia nyeupe ya kuleta mabadiliko ya bandari hizo mbili na pengine na bandari nyinginezo. Bandari ya Mtwara ni bandari ambayo ina uchumi mkubwa kama itasimamiwa wa nchi za jirani ikiwemo Zambia, Malawi na Congo na ndiyo maana ilianzishwa Mtwara Corrido kwa ajili ya kuhakikisha mazao yote katika Mtwara Corridor yanapelekwa Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza, Bandari ya Mtwara haina makasha. Hivyo watu wanatamani mizigo yao waipeleke Mtwara, makasha yako wapi? Hakuna. Nilitamani katika pesa ambazo zitaandaliwa, iwemo bajeti ya kupata makasha ili Bandari ya Mtwara ianze kufanya kazi. Tumekubaliana na Waziri Mkuu alitoa azimio kuwa korosho zote za Mtwara, Ruvuma (maana yake sasa hivi korosho mpaka Njombe kote wanalima, mpaka Mbeya wanalima) zipelekwe Mtwara. Imeshindikana, Mtwara hakuna makasha. Bado tunampa mkulima mzigo wa kuondoa mzigo wa Korosho kutoka Lindi au Mtwara kuupeleka Dar es Salaam.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za kwanza ni kwamba, badala ya ile tozo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Lulida kengele imeshagonga.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Aaah! Naunga mkono hoja na ninakushukuru sana.