Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niwe miongoni mwa Wajumbe wanaochangia Mapendekezo ya Mpango ambao unaenda kuandaliwa na Serikali. Naomba nianze kipekee kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kunijaalia afya njema ili na mimi niwe miongoni mwa hao ambao wamejaaliwa kuchangia leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na wajumbe waliotangulia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri sana ambayo anafanya katika kuleta maendeleo kwa ajili ya Watanzania. Nami ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti, nimepata fursa ya kuchangia na kwa kiasi kikubwa sana naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake mengi ambayo tulichangia wameyapokea na katika kuja na mpango hakika hata yale ambayo yalikuwa yamesahaulika naamini wataenda kuyaingiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nitachangia katika maeneo machache. Eneo la kwanza litakuwa Bandari, Reli ya TAZARA, Reli ya Kati na SGR kwa ujumla wake na muunganiko wa kiuchumi. Kamati yetu tulipata fursa ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam maboresho makubwa sana yamefanyika, imefanyika kazi kubwa sana ya uwekezaji ambao baada ya muda mfupi tunatarajia kama Taifa tutaanza kupata matunda yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mahojiano ambayo tulifanya na Wachumi wakasema Tanzania kama tunataka kujihakikishia uchumi wa uhakika na biashara ya bandari iweze kufanya kazi ya uhakika ni mizigo ambayo inasafirishwa kwenda Kongo ya DRC na wala siyo Zambia na wala siyo Uganda, effort ambazo zinatumia kutafuta mzigo wa kwenda Uganda nusu yake inatosha kuweza ku-explore na kupata mzigo mkubwa wa kwenda Kongo DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kazi kubwa nzuri sana ambayo inafanywa katika ujenzi wa reli Standard Gauge kwa maana ya SGR. Ni matumaini yetu sisi Watanzania kwamba reli hii hatujengi kwa ajili ya kusafirisha abiria, siamini hilo. Ili reli hii iwe na manufaa makubwa ni pale ambapo tutasafirisha shehena kubwa ya mzigo na mzigo ambao tunatarajia kupata kwenda bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilimsikia Mheshimiwa Naibu Waziri akiongelea habari ya Reli ya TAZARA na ubovu wake na manufaa ambayo tunategemea kupata kama nchi. Naomba niieleze Serikali na hili waliandike, kama tunatarajia kwamba mkataba huu utarekebishwa eti na Wazambia wana interest juu ya ufanyaji kazi bora wa TAZARA tunapoteza wakati na hili wanalifanya kwa makusudi. Naomba niikumbushe Serikali, hivi karibuni kuna malori karibu 300 ya Watanzania ambayo yalizuiliwa Zambia takribani mwezi mmoja mpaka miezi mitatu, hii wanafanya kwa makusudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niikumbushe Serikali ili katika mipango yao waweze kuweka mambo haya; mwaka juzi tulipata soko kama nchi wakati tulizalisha mahindi mengi sana kupeleka Kongo, lakini tulishindwa kupeleka kwa sababu ya kodi ambazo ziliwekwa na Wazambia, ikaonekana kwamba huwezi ukatoa gunia la mahindi Rukwa ukalifikisha Kongo likakulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najenga hoja hiyo, naomba niwaambie Serikali, ukitaka kufanya biashara ya uhakika kama Taifa na kuna matunda ambayo yako, hatuhitaji hata kutumia juhudi kubwa ya low-hanging fruits twende tukayachume haya matunda. Ukienda border ya Tunduma ambayo ndiyo border iliyo busy kuliko zote, mzigo ambao unatoka bandarini hauendi Kongo ya Moba wala Mlilo, unaenda Kongo ya Lubumbashi huko ndiko mizigo inakoenda. Kwa hiyo naomba katika mipango Serikali izingatie yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna border nne za kuweza kwenda Kongo; kuna Kongo kwa kupitia Kasesha border ambayo iko Jimboni kwangu, unapita Zambia kilometa 871 ndiyo unafika Kongo la Lubumbashi. Ukitaka kupita Kigoma, unaenda Moba kwenda mpaka Lubumbashi ni kilometa 750. Ukipita Tunduma ambayo ndiyo route ambayo inatumika zaidi ni kilometa 1,088.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa njia iliyokuwa fupi kuliko zote na naomba niipongeze Serikali imefanya uwekezaji mkubwa sana katika kuboresha bandari ikiwa ni pamoja na Bandari ya Kasanga na kwa bahati nzuri sana, tunavyoongea leo hii lami imefika mpaka Bandari ya Kasanga na katika bandari ya ambazo ni natural port ni pamoja na Kasanga ndiyo maana Wajerumani waliitaka Bandari ya Kasanga iweze kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini ambacho kinatakiwa kifanyike? Unajua katika kazi kubwa ambayo tunafanya ya kujenga reli ambayo itaanza kubeba mizigo, si suala la muda mfupi, itachukua muda mrefu kwa sababu heavy investment inatakiwa. Niiombe Serikali ukivuka kutoka Kasanga kwenda upande wa pili ni kilometa 480 tu ushafika Lubumbashi. Kwa hiyo kwa wale ambao walisoma hesabu kwa critical path analysis ndiyo shortest route, niiombe Serikali upande wa kule barabara ipo ambayo inatoka Moba kwenda Lubumbashi, kuna vipande vichache sana ambavyo vinahitaji kumaliziwa ili tutumie njia hii, tutakuwa tunapeleka mzigo Kongo bila kupita Zambia bila kukutana na vipingamizi ambavyo tumekuwa tukivipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, tuna mahusiano mazuri sana na Serikali ya Kongo, hiki kipande kifupi kwa sababu siyo kwamba kilometa 480 zote hazina barabara, barabara ipo ni maeneo machache sana haiwezi kuzidi kilometa 100. Tuanze kuvuna matunda haya ambayo hatuhitaji kutumia jitihada kubwa. Naamini kwa sababu Mheshimiwa Waziri anasikia, katika mpango ambao utakuja na bajeti ianze, kwanza ni bajeti ya maongezi tu, kinachotakiwa ni sisi tuwe na kivuko kutoka Kasanga kwenda upande wa pili ambacho kitaruhusu malori yapakiwe ndani. Ukifika kule ni barabara ya vumbi na kama kuna sehemu ambayo tutaweza kuwa na barabara ambayo PPP itafanya kazi ni kwa kipande hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuhitaji pesa nyingi, ni pesa ambayo ipo, hizi barrier zote ambazo tumekuwa tukikutana nazo za kiuchumi itakuwa ndiyo mwisho wake, tukitarajia kwamba eti tuna mahusiano mazuri na wenzetu wa Zambia wataturuhusu, tutachelewa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo na nimemwona Mheshimiwa Waziri akitikisa kichwa, naamini katika mpango ambao utakuja tutaliona hili likionekana vividly ili tuanze kuchukua hayo matunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)