Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kwamba, naomba nichangie mpango wa bajeti yetu ya 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Kamati ya Bajeti kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuandaa jambo hili, lakini pia namshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake, lakini kuna vitu ambavyo tunaomba sisi kidogo kama Waheshimiwa Wabunge tujaribu kushauri katika jambo hili. Ni kwamba, mpango wowote utakaokuwa umeandaliwa halafu mpango ule ukawa unakinzana na ilani yetu ya uchaguzi, sisi Wabunge tunaanza kupata hofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba, tulizungumza hapa katika suala la sheria zetu za nishati na madini kule tuliruhusu maduka ya kuuza dhahabu. Leo maduka haya ya kuuza dhahabu yamekwenda kuzingirwa tena kwa ajili ya kuanza kudaiwa kodi kubwa ambazo hazikuweko katika sheria. Sasa leo utoroshaji wa dhahabu umeanza upya mara 20 zaidi ya ulivyokuwa mwanzo hapo. Sasa tunajiuliza nchi gani hii leo inakuwa hivi kesho inageuka hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunakuomba sana Mheshimiwa Waziri na Kamati ya Bajeti hebu nendeni kwenye haya masoko uya dhahabu mkaangalie matatizo waliyonayo. Mambo mengi yamebadilika sasa huku kwenye madini tunataka kuleta tabu nyingine ambayo ilikuwa haipo; hawa wanunuaji wa dhahabu kule kwa wachimbaji hawa wengi ni ma-middle man japo wana leseni wenye pesa zao wako kule ghuba, wako Dubai, wako Madina, wako wapi, wale ndio wenye hizi pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu analetewa bilioni tatu watu wanataka labda kilo 20, kule ndani katika kilo 20 ana faida ya shilingi laki tatu-tatu tu, kilo 20 anapata milioni sita yake na anaweza akakaa miezi mitatu hajapata ile kilo 20 anakuja kudaiwa kodi ambazo haziwezekaniki kulipika. Kwa hiyo, badala ya kupitisha pesa katika mifumo yetu ya kibenki sasa pesa zinaanza kuletwa kwenye magunia kwenye magari. Hii Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana uangalie katika mpango huu namna gani mtakavyoweza kuweka jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna suala la biashara ya mafuta na gesi. Katika mpango wako hatujaona hiki kitu kwa sababu, lazima tukaziangalie hizi sheria, juzi tumetoa tozo, tumefanyaje, sasa huku tukaangalie. Tuangalie sera zetu za mafuta na sheria ambazo zinaonekana kwamba, kwenye gesi tunachelewa namna gani, kuna mpango wa bomba la gesi kutoka kwa wenzetu kule Mtwara na Lindi, hii biashara sasa hivi inaonekana kama sio biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye suala la mafuta tunashukuru mpaka sasa hivi ni kwamba, Wizara ya nishati imechukua nafasi ya kutafuta mpango mpya kwa ajili ya kushusha hizi bei za mafuta. Lakini biashara ya mafuta ile iweze kuchangia katika uchumi wetu. Hili Mheshimiwa Waziri katika mpango liingizwe tuone namna gani ambavyo tunaweza tukaenda katika mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jingine suala ambalo tunaliona sisi kwamba ni matatizo ni kilimo cha pamba. Kwenye kilimo cha pamba kwenye ilani yetu tumesema tunataka kuzalisha tani milioni 10, leo mwaka unaisha tunakuja katika mpango mwingine tena wa 2022/2023 hatuoni jitihada za pamba tupate tani milioni 10. Tulikuwa tumezungumza kwenye mpango wa 2021/2025 katika ilani na katika mpango huu juzi tumeujadili, huku na kwenyewe Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ni kwamba, tunakuomba uangalie katika pamba. Tulisema mbegu zitazalishwa Igunga, kwenye mpango wako hapa hatujaona kiwanda kinachotengenezwa Igunga kwa ajili ya kuzalisha mbegu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mbegu hakuna kwa wakulima. Mbegu zinauzwa mpaka 1,500; 1,200. Juzi tumemuuliza sisi Waziri, Naibu Waziri wa Kilimo, suala la kuuza mbegu limetoka wapi? Leo mbegu imekwenda kuanza kuuzwa wakati mbegu ilikuwa inagawiwa kwa wakulima halafu badaye wanakuja kukatwa? Hii mnaanza kutengeneza vita kati ya sisi Wabunge tunaotoka kwenye zao la pamba; tutapataje hiyo ajira milioni 10 kwa sababu wakulima wa pamba ni wengi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, na huko kwenye pamba tunapata pamba kwa ajili ya nguo, tunapata mbegu kwa ajili ya mafuta, tunapata mashudu kwa ajili ya mifugo yetu, hatukuona kwenye mpango wako. Sasa hili halikubaliki Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine Mheshimiwa Waziri katika hili suala lako la mpango ni suala la, tulikuwa tuna shirika letu sisi hapa la mbolea TFC, leo watu wanaanza kuzungumza tena ruzuku? Nani wa kupewa ruzuku kama sio Shirika la Mbolea? Tunatakiwa TFC tunayo, jambo lolote ambalo lilianzishwa na Mheshimiwa Hayati Baba yetu wa Taifa Mwalimu Nyerere, jamani, leo tunaanza kutoa ruzuku tena kwa mabepari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, aah! Hii inauma sana kwa wastani. TFC, tunaiacha TFC leo tunakuja kununua mbolea, mbolea inaanza kulalamikiwa wakati hii mbolea tumeishauri sisi kwenye mpango kwamba, mbolea inunuliwe wakati ambao sio wa season. Sasa leo mnakuja kuagiza mbolea kwenye high season, inakubalika wapi? Wakati mngeiimarisha TFC mkapeleka kule mtaji mkubwa katika TFC, kwanza mkisema ruzuku kule ndio mahali penyewe sasa; Mheshimiwa Waziri hili suala la mbolea liangaliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mwisho ambalo nataka kuzungumza ni hili suala ambalo limekuja katika nchi yetu. Sijui tumeenda kulipata wapi, suala la ujenzi wa Force Account, nchi inakoelekea Mungu ndiye anayejua. Wenzetu Wakenya miaka 10 walikataa Force Account, leo watumishi wa Serikali badala ya kuja kufanya kazi za Serikali tunawaona kwenye mitandao, unamuona mkuu wa wilaya, mkurugenzi, anachimba misingi, eeh! Hii nchi. Mipango gani hii tunayokwendanayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakwenda wataalamu wote wanahama ofisi za Serikali wananchi wanaacha kuhudumiwa kwenye ofisi za Serikali unakwenda kuuliza unaambiwa watu wote wako vijijini. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu wewe ni mchumi, makandarasi wapo, tunao makandarasi zaidi ya elfu 60, wapeni kazi tutengeneze uchumi katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sasa hivi imekuwa ni wizi, tunakwenda kuziimarisha ofisi zetu kule, watu wanakwenda kuiba hizi pesa zinapelekwa hazina ukaguzi. Kwenye mpango wako hatujaona hapa sisi suala la CAG unakwenda kumuimarishaje CAG? Hatujaona kwenye mpango wako na ndiye anayekwenda kukagua hizi pesa hizi trilioni 1.3 subiri balaa lake utakuja kuliona. Pamoja na vitisho mnavyovitoa sasa hivi ambavyo havina meno wataendelea kuiba hizi pesa kwa sababu, walioiba hawajapelekwa kotini mpaka sasa hivi. (Makofi) [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuambie CAG unakwenda kuongeza idadi ya watumishi CAG kwa kiwango gani kwa sababu ofisi hiyo iko kwako? Hawa wakaguzi wetu wa ndani ndio ni sehemu ya wezi wanaoiba kule katika halmashauri, hatujaona kwenye mpango wako unakuja kusemaje kuhusiana na suala la CAG?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hili mimi bado napinga huu mpango. Kauandaeni vizuri muulete. Mtuambie namna gani watakavyopelekwa kortini jhawa wat una Mahakama kule za hawa watu mnaenda kuziongezea fedha kiasi gani ili tuwe tuna uhakika na jambo hili. Lakini suala la kuwaondoa makandarasi katika nchi hii tunabakiza wachina, tunabakiza waturuki, habari yake mtakuja kuiona mbele ya safari. Ahsante sana. (Makofi)