Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Upendo Furaha Peneza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba tu niseme kwamba, kama Taifa na kama Wabunge, tunahitaji, vita ambayo tunakuwa tumeipigana na ambao wengine wameipigana kabla wengine hatujaingia Bungeni, inapaswa iendelee; lile suala la misamaha ya kodi na watu wanaosamehewa kodi kuweza kulipa. Kwa sababu tumechambua hata katika Sekta ya Afya, pesa nyingi haijapelekwa katika Sekta ya Afya, kwa hiyo, tunahitaji kuangalia kila pesa iliko ili tuweze kuhudumia watu wetu wasiweze kufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Sekta hii ya Afya tuna Madaktari ambao wanatibu katika maeneo yetu, ambao wengi wamepata elimu kwa ngazi ya Diploma na hawa Madaktari wamekuwa wakisambazwa katika Vituo vya Afya lakini pia vile vile hata katika Hospitali za Wilaya katika maeneo mengi na wamekuwa wakifanya kazi na watu wasio na elimu ya Udaktari kama mimi, siyo rahisi sana kutambua kama ana degree ya Udaktari au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo moja kwamba hawa watu pamoja na kutuhudumia vizuri na elimu ambayo wameipata kwa miaka mitatu, wakihitajika kwenda kusoma na kupata degree, inawalazimu tena kwenda kusoma kwa miaka mitano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie hili. Mimi sio mtaalamu wa Udaktari, lakini waweze kuangalia ni namna gani wanaweza wakafupisha hii miaka ili angalau, kwa sababu kuna masomo wameshasoma katika kipindi cha Diploma basi wanavyosoma degree miaka iweze kupungua. Mfano ni katika elimu ya engineering hapa hapa Tanzania, wanafunzi waliomaliza Diploma katika vyuo vya Technical Schools kama Arusha Technical, wanapokwenda kusoma degree za engineering wanaanzia mwaka wa pili. Kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kuliangalia hilo kama angalau tunaweza kuwasaidia hao Madakatari wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hawa wanaosoma Diploma kwa jinsia ya kike, inawalazimu wanapomaliza elimu ya Diploma kwenda kufanya kazi kwa miaka mitatu ndipo waruhusiwe kwenda kusoma Degree kwa miaka mitano. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya alisema ndani ya Bunge hili Tukufu kwamba menopause inaanzia miaka 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukipiga mahesabu, kama binti atamaliza Diploma kwa miaka mitatu, akafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu ndipo akasome hiyo degree ya miaka mitano, kwanza ndani ya hiyo miaka mitatu ya kufanya kazi kuna changamoto. Anaweza akaolewa na mambo mengine hapo katikati yakabadilika. Vile vile anaweza kufikia menopause hata hiyo elimu yenyewe ya Udaktari kwa maana ya MD hajaweza kuifikia. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iliangalie hilo na iweze kurekebisha ili watoto wetu wa kike angalau wapunguziwe muda wa kufanya kazi hapo katikati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile natambua juhudi za kuhakikisha kwamba tunaweka usawa wa kijinsia ndani ya Taifa letu. Kumekuwa na juhudi mbalimbali na harakati za wanawake mbalimbali na leo katika hotuba yake Mheshimiwa Waziri Ummy aliweza kusema na kumshukuru mume wake kipenzi kwa maneno yake, kwa kumsaidia katika utekelezaji wa kazi. Pia nimemsikia Mheshimiwa Mama Mary Nagu, naye anamshukuru anasema mimi Nagu kanisaidia sana! Pia wanawake hapa ndani ya CHADEMA Mheshimiwa Mama Grace Tendega na mama zangu akina Mheshimiwa Susan Lyimo na wenyewe wanawashukuru waume zao kwa kuwasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sasa Wizara iangalie umuhimu wa kuwashirikisha wanaume kuweza kuelewa uwezo wa wanawake katika kuwasaidia kuleta usawa wa kijinsia. Hatuwezi tukaifanya hii vita peke yetu, lakini tunahitaji kuwashirikisha wanaume. Kwa hiyo, naiomba Wizara iweze kutoa kama trainings kutoka kwa mashirika mbalimbali ili wanaume pia wapatiwe hii elimu wapate kuona nafasi ya mtoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo, naomba pia nimshukuru baba yangu mzazi ambaye kwa kupitia kwake, kwa kuona umuhimu wangu kwake, ana watoto watano, wa kiume mmoja na wa kike wanne na aliapa kwamba lazima atengeneze wanawake wanaoweza kujitegemea katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa zinazowakabili watoto wetu wa kike. Mheshimiwa Ummy katika Hotuba yake ameweza kutaja kwamba kuna vifo vya wanawake, bado vipo na hii hali inatisha, lakini tunaweza tukatambua kwamba baadhi ya watoto au watu wanaokufa kutokana na hivi vifo ni watu wanaobeba mimba kabla ya kufikia umri halisi wa kuweza kupata mimba. Kuna changamoto za kielimu pia ambazo zinawakabili watoto wetu, ndiyo maana wanashindwa kwenda shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binti anaingia katika kipindi cha hedhi ambapo kama hana vifaa vya kujisitiri (Sanitary towels) anashindwa kwenda darasani sawasawa na mtoto wa kiume. Katika adult level msichana anaweza kwenda katika kipindi cha hedhi kwa siku nne, at maximum siku saba. Sasa binti akikosa darasani siku nne, somo kama ndiyo limeanza leo, baada ya siku nne maana yake hilo somo limekwisha. Kama ni siku saba, hivyo hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tutambue kwamba Serikali imeweka msamaha wa kodi kwenye sanitary towels, lakini bado sanitary towels zinapatikana kwa bei ya juu. Sanitary towels kwa bei ya chini kabisa Dar es Salaam ni sh. 1,500/=, lakini nyingine ni sh. 2,500/= mpaka bei ya juu zaidi. Sasa hapa suala linalokuja ni kwamba, Serikali itengeneze chombo maalum ambacho. Humu ndani tunapitisha misamaha ya kodi ili iwanufaishe wananchi, lakini mwisho wa siku inakuwa ni manufaa kwa wafanyabiashara na siyo wananchi tuliowalenga hapo mwanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali itengeneze chombo maalum cha kuangalia kila bidhaa tuliyoiwekea msamaha wa kodi kinasimamia na kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana kwa bei iliyolengwa kwenye soko. Suala hilo pia linagusa mpaka maeneo ya dawa, kwamba dawa zimewekewa misamaha ya kodi, lakini ukienda madukani kwenye private pharmacies bei ni kubwa. Kwa hiyo, Serikali iliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala hilo hilo, tunasema kwamba Wizara hii ya jinsia iweke kipaumbele na kuhakikisha kwamba, sekta nyingine zote zinaangalia jinsia katika utekelezaji wa mambo yake. Katika kilimo, watu wote wanaofanya kilimo 80% ni wanawake. Usipowaangalia wanawake katika kilimo, maana yake ni kwamba kilimo lazima kife. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika elimu, ni vizuri sasa Wizara ya Afya kushirikiana na Wizara ya Elimu, ikatenga pesa, kama ni sh. 10,000/= kwa ajili ya Shule za Msingi kila mwanafunzi, basi kwa mtoto wa kike iwe ni sh. 12,000/= ama sh. 13,000/= ili ile sh. 3,000/= iweze kugharimia kwenda kulipia sanitary towels. Vile vile katika Vyuo Vikuu mkopo wa Chuo Kikuu uweze pia kugusa kuhakikisha kwamba wa msichana uwe juu zaidi ili kumsaidia asikose darasani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi sasa katika masuala yangu ya Mkoa wa Geita. Mkoa wa Geita tuna changamoto nyingi na tuna vijiji vingi ambavyo havina umeme. Naiomba Wizara ya Afya ishirikiane na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba, zahanati na vituo vya afya vinapatiwa umeme wa solar ama umeme kabisa kutoka gridi ya Taifa. Kwa sababu, mtu anaweza akajifungua usiku! Sasa mtu anazaaje gizani kwa kweli? Ni kitu kidogo ambacho kinakuwa kigumu! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasi tuna tatizo hilo hilo la CHF ambapo wananchi hawapati dawa. Vile vile CHF mtu akitoka Geita akienda Chato hapatiwi huduma; akitoka Geita akaenda sehemu nyingine, hapatiwi huduma. Hili nalo muweze kuliangalia ili tuweze kuona ni namna gani tunaweza tukawasaidia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kuiomba Serikali kwamba, ikumbuke Hospitali ya Mkoa wa Geita ambayo mmeifanya sasa imekuwa ni Hospitali ya Rufaa, lakini haifanani hasa na kuwa na sifa hiyo ili iweze kuwahudumia wananchi wa Mkoa wa Geita. Pamoja na hilo, liangaliwe suala la kutafuta fast ferry kwa sababu, kutoka Geita kwenda Mwanza tuna maji pale katikati. Ukitegemea hizi ferry za kawaida, mgonjwa anaweza kufia ndani ya ferry. Kwa hiyo, ferry badala ya kwenda na mgonjwa inarudi na maiti. Kwa hiyo, tunaomba sasa tuweze kupatiwa pia fast ferry kwenye hilo ziwa kuhakikisha kwamba wagonjwa wanafikishwa on time katika hospitali zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.