Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Nikupongeze kwa namna ambayo unaendesha Bunge hili kwa weledi. Pia nijiunge na wenzangu kutoa pongezi na shukurani nyingi, kwa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa jinsi ambavyo anaendeleza kazi hii kwa kasi na kusema kweli anatekeleza kwa mafanikio. Sio mafanikio tu, lakini huku akizingatia kile ambacho watu wengi wanakisahau; Katiba, Sheria, Sera na Kanuni. Jambo hili limeanza kuvutia sana wawekezaji kutoka nje na hapa ndani na watu kujisikia wako nyumbani. Naamini hiki kitachangia sana katika ukuaji wa pato letu katika miaka inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yake yote kwa yote ambayo walifanya. Wameleta mapendekezo ya Mpango ambayo yanakubalika. Nimpongeze pia Mheshimiwa Daniel Silo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, kwa namna ambavyo aliwasilisha ushauri na maelekezo fulani fulani ambayo, yametoka kwenye Kamati yake kuhusiana na mapendekezo haya ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajikita kwenye lile ambalo nataka nizungumzie zaidi ambalo ni la mambo ya sera ya fedha, niseme kwamba licha ya mipango mingi na mikakati mingi ambayo inatekelezwa kwa sasa hivi, ikiwepo ile ambayo inaendana na mpango wa kupambana na athari za COVID-19. Utaona kwamba bado Mpango huu umekuja na maoteo ya ongezeko la pato la Taifa ambalo nafikiri ni chini sana asilimia 5.2. Ni ongezeko kidogo sana ukizingatia kwamba mambo mengi yanatokea na yanatokea kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hivyo, naamini kwamba, sisi hatutoki kwenye uchumi ambao ulikuwa kwa hasi, uchumi wetu umekuwa chanya, kwa hiyo tuna kila sababu ya kutegemea kwamba, kile kinachotokea kwenye ground na ukweli ni kwamba maoteo ya ukuaji wa chumi zilizoendelea ni asilimia sita kwa mwaka 2020/2021 na mwaka unaokuja unaotea wakue kwa asilimia 4.9, yote hii itachochea ukuaji wa uchumi wetu. Kwa hiyo, ni lazima pengine tuangalie vizuri kwamba tusiwe-conservative sana bali, tujaribu kuangalia ni namna gani tutachukua hatua na nafikiri kwamba, hatua zitakazochukuliwa zilete matokeo ni hizi ambazo nazungumza sasa hivi ndio hizo zitaweza na ndio kitu kimekuwa kikwazo kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaona kwamba ukuaji wa pato la Taifa unatokana zaidi na sekta zile ambazo zinanufaika na uwekezaji wa Serikali. Miundombinu, ujenzi ndio utaona hizo sekta ndio zinanufaika na zinakua kwa kasi mpaka asilimia 13 mpaka 14, lakini sekta nyingine hizi za watu binafsi binafsi za kilimo na kadhalika, zinakua kwa kiwango ambacho naamini bado kiko chini. Ukuaji huu mdogo kwenye sekta hizi naamini unatokana zaidi na kile ambacho hakijafikiwa licha ya kwamba tuna uchumi ambao tunasema ni uchumi tulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi tulivu maana yake ni uchumi ambao una-low inflation (mfumuko mdogo wa bei). Hata hivyo, utakuta kwamba, mahitaji kwa uchumi kukua kwa kasi sio tu kwamba uwe na mfumuko mdogo wa bei, wanasema necessary but not sufficient conditions ziko tatu. Moja ni hiyo mfumuko wa bei mdogo; lakini huu mfumuko wa bei mdogo lazima uweze kutupelekea kupata riba zilizo chini. Cha kwanza, riba ziwe chini na tulivu na maana ya riba kuwa chini na tulivu ni riba ziwe chini kwa maana ya kwenye tarakimu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni kwamba, thamani ya sarafu yetu iwe nayo tulivu; exchange rate stability. Kwa hiyo, the three ni necessary but not sufficient conditions za rating growth. Sasa niseme hivi, tutaona kwamba uchumi wetu kwa miaka mingi umekuwa na inflation ambayo ni chini ya asilimia 10. Imekua kwenye zaidi ya miaka 10 iliyopita, tuna inflation ambayo iko kati ya tatu sasa na sita au saba, lakini utakuta kwamba bahati mbaya licha ya kuwa na hiyo, bado kuna matatizo ya sera ya fedha haijaweza kutuletea riba ambazo ziko chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, issue ni kwamba tujiulize ni kwa nini sera hizo haziji chini? Benki Kuu imefanya mambo mazuri, imeweza kupunguza ile riba ambayo wanatoza mabenki wanakwenda kukopa kwao. Imepunguza fedha ambayo mabenki wanalazimika kuweka kwenye Benki Kuu ambayo haipati riba. Zote hizi zimejaza mabenki ukwasi wa kutosha. Hata hivyo, bahati mbaya hatua hizi zilizochukuliwa siku za karibuni zimesaidia yale mabenki kutengeneza faida kubwa kwa manufaa ya wana hisa wao tu, hazijaenda kwa walengwa, yaani hizi hatua zimguse yule mzalishaji wa sekta binafsi ambaye ili yeye aweze kuongeza uzalishaji au awekeze kwenye uzalishaji mpya, ni lazima apate mkopo ambao ni acceptable kwa riba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiyo haijatokea. Nafikiria kwamba, siku itakapotokea kwamba riba zishuke ziwe kwenye tarakimu moja, ndio utaanza kuona kwamba mahitaji ya mikopo yataanza kuongezeka. Kwa sababu, unajua kwamba unaenda kuzalisha, lakini huhatarishi ile dhamana yako, hawaji kuiuza kwa sababu utaweza kulipa ule mkopo na u-service. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kwa hizi riba za asilimia 16 mkopo unaji-multiply mara mbili baada ya miaka mitano. Hebu niambie ni kitu gani duniani hapa utawekeza halafu kiji-multiply mara mbili kwa miaka mitano. Hata nyumba yako wewe mwenyewe miaka 20, 30 ndio unarudisha fedha yako. Kwa hiyo, nasema hiyo haitawezekana mpaka wafanye hivyo. Sasa napenda kutoa hoja kwamba, kitu kinachopelekea mabenki wasishushe riba sio kana kwamba hawana ukwasi, ni kwamba kuna riba ambayo ni bench mark, kigezo ambacho wao ndio wanaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika wao wanaangalia kwamba kwenye soko la dhamana za Serikali, je, riba inayopatikana pale ni kiasi gani? Wakishapata pale wanasema ok, hii ni risk free rate kwa hiyo ile ndio kigezo chetu. Hatuwezi kushuka chini na ukweli ni kwamba fedha hizi zilizopatikana zote kwenye huu mlegezo uliotolewa na Benki Kuu, nyingi zimekwenda kwenye dhamana za Serikali, hazikwenda kwenye sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme hivi, ukweli ni kwamba hata deni la Taifa linachochewa zaidi na riba hizi za dhamana za Serikali za muda mrefu ambazo ni asilimia 15, 16. Kwa hiyo, tunaposema deni la Taifa tatizo sio tu kwamba eti wanakopa sana, hapana. Rate service burden inakuwa kubwa kwa sababu riba hizo ziko hivyo. Ukiangalia miaka ya nyuma riba kwa dhamana za Serikali hazikuwa hivi. Kwa hiyo, nasema ule mfumo wa ku-auction dhamana za Taifa, una-auction kwa kutaja bei, kwamba, nauza dhamana za bilioni 400 kwa asilimia 16 nani atashusha bei? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni soko au una-dictate? Nakuapia hazitakaa zishuke hizo riba ilimradi namna ya kuendesha hiyo minada ni hiyo hiyo. Kuna mwanaume anaitwa Dutch Auction natumai wajaribu kuangalia namna gani ya kufanya au waanze kushusha waseme tuta-auction kwa asilimia 10, tuone kama hawatanunua. Mabenki yatakimbilia hata mimi nitanunua kwa sababu asilimia 10 it is a big real interest rate. Real kwa sababu ukitoa hii asilimia tatu, nne ya inflation bado nina real benefit ya six, seven percent. Kwa hiyo, kuna kila haja tumwombe Waziri atekeleze kwa sababu, hiyo itasaidia kwenye kupunguza burden kwa kila mtu na kuanza kuona tena hali inarudi kikawaida, watu kuchukua mikopo, biashara kukua na sisi wote tukafaidi na utakuta hata kwenye kilimo watu watapata mikopo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba, nafikiria hilo ni la msingi na tuseme kwamba pamoja na kwamba mfumuko wa bei umetufaidisha kuhakikisha kwamba exchange rate bado imekuwa stable, lakini bado haujatufikisha pale ambapo, that is the most critical issue ni riba na niseme hivi nazungumza riba kwa sababu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya fedha sio kitu kingine isipokuwa riba, basi ukienda nje huko duniani kwenye masoko yaliyoendelea, nenda US, nenda wapi kitu cha maana wanaangalia bank rate, that is all, mambo mengine yanaji- set yenyewe kwenye soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naambiwa muda umeisha. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)