Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nami kupata fursa hii na kuchangia katika hoja hii ya Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
(Agreement Establishing the African Continental Free Trade Area).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika siku ya leo ni siku ya kihistoria ambayo, kama dada yangu Mheshimiwa Pindi Chana alivyosema, ni siku ambayo ndiyo chanzo cha ndoto za Baba wa Taifa mwanzilishi wetu kufika sehemu ya kuwa na Afrika moja. Siku zote nchi kuungana zinatakiwa ziwe na chachu na chachu kuu ya muunganiko ulimwengu mzima ni biashara na uchumi. Kuanza kufanya biashara kwa pamoja mkawa na soko moja ndiyo chachu kuu ya kuunganisha nchi au mabara kote ulimwenguni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndoto ya Baba wa Taifa ilikuwa Afrika iwe moja, na ndoto yakeni tofauti na Kwame Nkrumah, fikra zake ilikuwa Afrika iwe moja kwa kupitia building blocks. Kwame Nkrumah yeye alisema tuwe wamoja kuanzia siku ya kwanza, kama Muammar Gaddafi alivyokuwa anafikiria.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Baba wa Taifa alisema through building blocks ya Afrika Mashariki, ya SADC, COMESA na Building blocks nyingine. Na huu mkataba chanzo chake ndiyo hivyo, mazungumzo ya mkataba huu yalikuwa mazungumzo ya viongozi wa Secretary General wa East African Community, kipindi kile alikuwa Balozi Mwapachu, SADC na ECOWAS ndio chanzo, inakwenda sambamba na ile ndoto ya Baba wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wasiwasi mwingi mkumbwa niliousikia leo ni kama Tanzania tupo tayari au la; na kama tumejipanga na kama tuna kasoro zozote. Kasoro hazikosekani kila nchi ina mapungufu yake. Lakini Tanzania na mfumo huu wa soko tayari sisi tumeshajifunza na tupo daraja la juu kabisa kulinganisha na nchi nyingi hizi za ndani ya Afrika, tofauti na tunavyojifikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jumuiya ya Afrika Mashariki ni jumuiya ya mambo mazito kabisa. Kwanza, Umoja wa Forodha, pili, Soko Huria ndani ya nchi hizi tano, tatu, Umoja wa Kifedha. Kwa sehemu kubwa Umoja wa Forodha tayari umeshakamilika, na kwa kipindi ambacho sisi tupo toka mwaka 1999 mpaka leo; wakati tunaanza hofu kubwa ya Tanzania ilikuwa kuwa soko la Kenya kwa sababu kulikuwa kuna dhana ya kwamba Kenya ina uchumi mkubwa, ambao ni sahihi, na sisi kwa sababu uchumi wetu ni mdogo tutakuwa tu na watu wengi, tutakuwa tu soko la Kenya; lakini ukweli uliothabitika ni tofauti na hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita mpaka saba leo Tanzania ina positive balance of trade. Maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba inauza zaidi katika masoko ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kushinda tunachokinunua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona kuna kimya hivi kana kwamba hamuamini, angalieni takwimu. Tanzania inauza bidhaa yenye thamani kubwa Kenya kushinda inachonunua kutoka Kenya kuja Tanzania kwa zaidi ya miaka sita. Hali kadhalika Tanzania tunauza vitu vingi Uganda kushinda tunachonunua. The same Rwanda, na Burundi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ki ukweli kama Mheshimiwa hapa mmoja aliyezungumza hatuna tatizo lolote na wajasiliamali na wafanyabiashara wetu. Tatizo muda hadi muda tunawafunga minyororo wanashindwa kufanya kazi vizuri zaidi, lakini juu ya hivyo tuna mifano ya kampuni za kitanzania ambao wanafanya biashara nchi zaidi ya kumi na mbili na nyingine kumi na nane na zina-compete vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakupa mfano; Azam ipo ndani ya Afrika inafanya biashara nchi 15, MeTL nchi 18, export trading nchi 12, MM Steel Intergrated nchi 13, wamekwenda huko wanaendesha viwanda vikubwa na wanaweza ku-compete. Sasa huu umoja umuhimu wake ni soko, soko ni watu. Ukiangalia nchi ambazo zimeendelea kwa haraka sana kama vile China, India, Brazil, Marekani, nchi zote hizi zina kitu kimoja, zina watu wengi. Jumuiya Afrika Mashariki ina watu zaidi ya milioni 200, hili eneo lote hili litakuwa na watu zaidi ya bilioni moja, hii ni fursa adhimu sana kwa Tanzania kujipambanua na kuuza nje ya soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini tunachokiuza kikubwa Kenya na ndani ya Jumuiya Afrika Mashariki ni mazao, Tanzania inalisha Afrika Mashariki katika kuzalisha, na tunalisha mpunga, vitunguu, machungwa na mananasi. Kimsingi tunaweza ku-compete.

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita, nikimalizia, nilikuwa naangalia You Tube kupitia Internet kuangalia katika sekta ya muziki, kwa sababu nimekaa na kaka yangu hapa naona niigusie, sekta ya muziki. Nikaangalia katika You Tube, ni miziki gani inasikilizwa Nairobi kwenye ile top ten ya You Tube. Katika top ten wana muziki saba wa Tanzania wakiongozwa na Diamond Platinums.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nazungumzia hilo, vijana wetu hawana hofu ya kupambana wakati sisi tunafunguka Music Industry Nairobi ilikuwa imefika daraja kubwa kushinda sisi, lakini wale vijana hawakuwa na hofu. Leo hii Afrika Mashariki yote vijana wetu wana dominate. Hii ni message positive kwamba Tanzania mapungufu tunayo, tunajua matatizo yetu yapo wapi, lakini tunauwezo mkubwa sana wa kupambana na kushindana na kupata manufaa makubwa katika hili eneo huria la biashara. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)