Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Na mimi naunga mkono hoja ya kuridhia Mkataba huu wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania siyo kisiwa na sisi tuko ndani ya Afrika, na mimi pia najivunia kuzaliwa Afrika. Pamoja na maamuzi ambayo Serikali imefanya kupitia Wizara, tunawapongeza sana kwa maamuzi haya, lakini mimi nitakuwa na mambo machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhia ni jambo moja lakini lazima tujipe muda wa kufanya tafiti za kina, faida ambazo tutakwenda kunufaika kama nchi lakini Watanzania ni namna gani tumewaandaa ambapo wanaweza kunufaika na maazimio haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni kwamba kama tunatambua tunaingia kwenye ushindani lazima tujue mshindani wetu ana nini na sisi tuna nini. Lazima kuandaa bidhaa ambazo tunaamini ndiyo hitaji kwenye biashara hiyo. Kwa mazingira hayo hayo tumekuwa na kasumba fulani tukiamini kwamba watu fulani ndio wanastahili kuwa wafanyabiashara. Kupitia hii nafasi lazima tuanze kuwandaa Watanzania ambao wanaweza wakawa ma-supplier kwenda kwenye nchi nyingine za Afrika, hiyo itakuwa ni faida mojawapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia ushindani lazima kuna vitu vinavyoitwa vikwazo. Lazima tutengeneze mazingira rafiki kwa uwekezaji pamoja na wafanyabiashara ambao tunaamini kwetu tutakuwa tumeitumia hiyo fursa kama nchi. Pamoja na kuangalia ni kipi ambacho tunaweza tukatumia kama fursa baada ya kuridhia, lazima pia tujenge uaminifu. Tusipojenga uaminifu pia ni changamoto. Uaminifu wetu utatengeneza mazingira rafiki ya watu waliopo nje kuja kwetu na sisi kujijengea mazingira ambayo hata mtu ambaye alikuwa hajawahi kufikiri kupitia tu ile sifa ya mtu mwingine ambaye aliona uaminifu wetu tunaendelea kutangaza Taifa letu na kunufaika na hayo maazimio. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la teknolojia lazima tuone kama hilo jambo ni kipaumbele. Lazima tuachane na biashara za mazoea tuanze kuwandaa Watanzania kutumia teknolojia kuweza kunufaika kwa kuangalia huu mkataba ambao tunaamini utalisaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri pia tuangalie sera zetu ni rafiki kiasi gani. Mara nyingi tumekuwa na mabadiliko sana ya hizi sera, lazima tuwe na sera ambazo hazitawapa shida hizo nchi wanachama ambazo tumeamua kuingia nazo kwenye Bara la Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuzungumza yote ambayo Wabunge wenzangu wamezungumza hatuwezi kukwepa biashara mtandao, lazima tujijenge kwa kuanza kuwaandaa vijana wetu, kabla ya kufikia hayo malengo ambayo tumejiwekea, lazima tuanze kuwaandaa leo. Wafanyabiashara waliopo ni wajibu wa Serikali kuona namna bora ya kuwatengenezea network lakini kuna wale ambao lazima tuwaandae sisi, tutengeneze mabilionea wengine, tusifikiri walewale ambao walikuwepo kuanzia mwaka 2010, leo tuanze kutengeneza wengine ili na sisi tuweze kunufaika kwenye huu mkataba ambao tumekwenda kuridhia.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mazingira yote ni lazima tujue sisi kwa upande wa kilimo ni mazao gani ambayo yana-pick kwa Bara la Afrika kutoka Tanzania, lazima tuwe tunatumia hiyo nafasi. Tusisubiri baadaye tukiwa tumechelewa, ni nini kinahitajika tunaanza sisi kwanza kuitumia hiyo fursa. Leo tunahangaika na mahindi, kama mahindi hayalipi lazima muwe mmeshaangalia mapema, kama siyo mahindi ni kipi mbadala? Tunakiandaa mapema kwa ajili ya kutumia hiyo nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa leo ni kupongeza na kuendelea kuwasisitiza kwamba lazima tuendelee kufanya tafiti za kina, faida ni zipi, hasara ni zipi. Lakini kuna mengine yanaweza yakawa kama challenge kwetu ikawa kama fursa lazima tuitumie kwa sababu tunaamini itasaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, ahsante sana. (Makofi)