Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

Hon. Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa fursa hii uliyonipa na pia vilevile naomba nichukue fursa hii kuunga mkono hoja na hali kadhalika kuipongeza sana Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia katika Azimio hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwa namna ya kipekee sana nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri mwenzangu na wataalam wetu kwa kazi hii kubwa walioifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tatu; nimefurahi sana juu ya michango mbalimbali iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge iliyotoa msisitizo namna ambavyo tutatakiwa tufanye sisi katika Serikali katika kuhakikisha kwamba Itifaki hii tunaitendea haki na kusogeza mbele maendeleo ya sekta mbalimbali zilizotajwa hapa katika kilimo, mifugo na uvuvi vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa mifugo kwa maana ya afya ya mifugo na uvuvi, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge juu ya Serikali tulivyojipanga. La kwanza, niwatoe hofu kwenye upande wa instrument kwa maana ya sheria upande wa mifugo sheria zipo na tuna competent authority ambayo ni Directorate of Veterinary Service. Hii inatambulika Kimataifa Sheria ya Mifugo Duniani inamtambua yule DVS wetu hapa, anatambulika kabisa kwa mujibu wa taratibu zote za kidunia, Shirika la Afya ya Mifugo Duniani (OIE) linamtambua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria yetu ya Usalama wa Mifugo kwa maana ya wanyama na chakula cha mifugo ipo siku nyingi sana ni Sheria Na. 17 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2007 vilevile tukaiboresha 2019 na tuliiboresha tena mwaka 2020 ili iweze kuendana na hitaji la soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwa na Sheria hii ya Afya ya Wanyama, pia tunazo Sheria za Veterinary ambayo tuna Bodi yake na ipo kwa mujibu wa Sheria Na. 16 ya Mwaka 2003 vilevile na Kanuni zake. Vilevile tunayosheria ya Wakala wa Maabara ya Veterinary na yenyewe yote hii ni katika kuangalia afya ya wanyama. Sheria Sura Na. 245 ni ya siku nyingi na yenyewe pia vilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie kwa upande wa namna tulivyo tupo vizuri kwa maana ya sheria inayolinda afya ya wanyama kwa maana ya mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona namna tulivyokwenda vizuri hapa tazama tuna kitengo kwenye eneo hili la afya ya Wanyama, ndio maana katika miaka mitano iliyopita tumefanikiwa kuanzisha na kuzalisha chanjo ambazo hazikuwepo huko nyuma, yote hii ni katika lile lengo la kuhakikisha mifugo yetu inakuwa na afya njema na kuwalinda walaji wetu. Mwanzo tulianza na chanjo mbili; Chanjo ya Mdondo na Chanjo ya Kimeta, hivi leo tumeshafanikiwa kufika katika chanjo saba; tuna Mdondo, tuna Kimeta, tuna Chambavu, tuna ya kutupa mimba, vilevile tuna chanjo ya mapafu ya ng’ombe, tuna chanjo ya mapafu mbuzi na sasa tunakwenda katika chanjo ya Sotoka ya Mbuzi na chanjo ya Kondoo, tukimaliza hiyo tunatengeneza ya Kichaa cha Mbwa. Hizi zote zinahusiano wa moja kwa moja wa mwanadamu na wanyama. Kwa hiyo, akiumwa mnyama na mwanadamu pia vilevile anadhurika, hiyo ni kwa upande wa mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, nataka niwahakikishie na ndiyo maana hata rate yetu ya kulinda mifugo yetu imeongezeka. Mwaka 2018/2019 tuliweka bajeti ya lita 8,000 ya kuogeshea mifugo tukaanzisha ile programu ambayo haikuwepo kwa miaka mingi sana, mwaka 2019/2020 tukaongeza kutoka 8,000 tukaenda 12,000, mwaka 2021 tumeongeza tena kutoka 12,000 mpaka 15,000 liters na mwaka 2021/2022 sasa tunakwenda katika lita 17,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia yetu hapa ni kuangamiza kabisa ugonjwa unaosababishwa na mbung’o. Kwa hivyo, yale magonjwa yote yanayosababishwa na mbung’o yaondoke na rate yetu ya kupunguza maradhi haya ni kubwa sana. Tumeshakwenda chini ya asilimia 30 hivi sasa tulichobaki nacho. Kwa hivyo, Waheshimiwa Wabunge unaweza ukaona jitihada za makusudi za kushindana kuhakikisha tunalinda afya ya mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi kwa jitihada hizo tulizozifanya pia pamoja na kuchelewa huku kumetupa nafasi ya kujipanga vema, hapa miaka michache iliyopita hatukuwa hata na viwanda vya kuchakata nyama, hatukuwa na viwanda vya kusindika maziwa. Nimemsikia Mheshimiwa Kiswaga hapa akitaja kiwanda cha ASAS ni moja katika mifano mizuri tuliyonayo. ASAS wana sindika maziwa na yanaweza kuuzwa kokote pale duniani, ni vile tu kwamba hizi itifaki ndiyo zimetuchelewesha, lakini niseme kwamba maziwa yao ni mazuri ukiingia leo katika baadhi ya ndege za Kimataifa kama South African Airways unakuta mtindi wa ASAS unaliwa mle.

Kwa hiyo, hii yote ni mipango mizuri tunajipanga katika kujitosheleza wenyewe ndani ya nchi na vilevile kuuza njeya nchi ndiyo maana tuna ASAS tuna Tanga Fresh, tuna Kilimanjaro Diaries na wengineo na viwanda vya kuchakata nyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha tunajitosheleza ndani, lakini tunauza na nje ndiyo maana tumefungua masoko kama yale ya Uarabuni tumemuona Prince Crown wa Saudia alipokuja hapa na wamepita katika machinjio zetu kadhaa. Zile machinjio wameziangalia ubora wake. Nataka niwahakikishie kwamba wameridhika sana, wamekwenda Tan Choice - pale Soga wameona, vilevile wamekwenda na Elia foods kule Namanga wameona kazi ni nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa samaki tunayo maabara kubwa na nzuri ya Nyegezi, ile maabara ya Nyegezi ni maabara ya Kimataifa nataka niwahakikishie inapima vimelea vya kibailojia, lakini inapima na vimelea vya kikemikali. Imekubalika Kimataifa na ndiyo maana Samaki wetu wanaweza kuuzwa Ulaya, wanauzwa Asia, wanauzwa kokote pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge maoni yenu ya namna ya kuweza kuboresha tumeyazingatia na ndiyo maana hata katika bajeti hii mialo kadhaa itatengenezwa, pamoja na kulinda afya za walaji wa ndani na kuendelea kulinda soko letu la nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii nami naendelea kuunga mkono hoja azimio hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)