Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoa mchango wangu, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan ambaye majuzi alifanya ziara yake akapita kwenye Jimbo langu la Hai na kwa kweli ametuachia ahadi kubwa sana na kukidhi matarajio ya Wananchi wa Jimbo la Hai. Namshukuru sana na Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Azimio hili naona limechelewa na limechelewa kwa nini? Kwa sababu tunalihitaji sana na sisi tuingie kwenye Soko la Dunia. Sasa ningependa nishauri mambo yafuatayo; Azimio hili litakuwa na faida kwetu kama tutafanya mambo yafuatayo;

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Ibara ile ya 5 inazungumza habari ya usalama wa nyama, mimea na chakula. Sasa kwenye eneo hili, sisi tumejiandaaje kuingia kwenye soko baada ya kusaini Mkataba huu? Nitaanza na eneo la Wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende tukaimarishe Sera zetu hapa; tumekuwa tukiletewa wanyama kutoka nje ya nchi kuingia kwetu lakini pia tumekuwa tukipeleka wanayama wetu nje ya nchi baada ya muda wanarudi. Sisi tuna sheria gani ya kuweza kukinga na kuhakikisha hatupati specie mpya zinazoingizwa kwenye nchi yetu pengine zinaweza kuja kuharibu aina ya wanyama tulionao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kupitia Itifaki hii tunayoenda kusaini lazima na sisi tujiandae tuweke standard, tuweke maabara za kisasa ndani ya nchi yetu kupima vinasaba vya wanyama wanaotoka ndani ya nchi na wanaoingia ili tujiridhishe kwamba kama ni Simba wa Tanzania ana vinasaba vya aina hii asije Simba mwingine akaja kuleta kitu cha tofauti. Kwa hiyo, tuwe na Sera ambazo zitaweza kutufungia. Kwenye eneo la mimea hali kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisimame hapa kwenye chakula. Hivi tulivyo tupo hivi kwa sababu ya chakula tunachokula. Sasa tuna usalama/sheria gani ambayo inalinda aina ya chakula tunachokula? Chakula sio tu kikiwa mezani; lazima tuangalie kuanzia namna ya kupanda, kuvuna na kukisafirisha. Hivi ukienda kwenye masoko yetu, tunayo miundombinu inayoweza kutufanya tukala chakula salama? Tunapojenga masoko yetu tunazingatia usalama wa chakula? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri ili twende vizuri na tuweze kunufaika na Itifaki hii, basi tuhakikishe suala la usalama linakaa kisheria na kwenye miundombinu linazingatiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze, ili tuweze kufanikiwa, hebu tukimbie haraka sana kwenda kurekebisha Sera yetu ya Kilimo. Sera hii ya Kilimo ifanane na uhalisia wa sasa hivi na ili tuweze kufanikiwa tuziimarishe pia zile taasisi zetu. Hii ni kwa sababu ili tuweze kuingia kwenye Soko la Dunia, wenzetu wanatazama sana usalama wa chakula ambao unatengenezwa kuanzia hatua ya awali. Tuimarishe Taasisi yetu ya Mlingano iliyopo Tanga ili iweze kufanya utafiti wa udongo; ni eneo ambalo tumelisahau. Tufanye utafiti tujue kwenye udongo huu tunaweza kupanda kitu gani ili tulime kwa tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutazame sasa kuongeza thamani ya mazao yetu. Hapa tulipo ili tuweze kufaidi hii hakuna namna unaweza kuingia kwenye Soko la Dunia kama huwezi kuongeza thamani ya mazao yetu. Ndio maana utaona sasa hivi wenzetu wa nchi za Jirani wanakuja hapa wanachukua mazao yetu, wanaenda kwenye viwanda vyao vidogo wanaita sorting industry, hizo sorting industry ukitazama; bahati nzuri nimefanikiwa kufuatilia mazao yanayotoka pale kwetu Hai yanaenda nchi Jirani nikaenda mpaka huko kwao wanachokifanya wana vibanda tu wanaita sorting industry. Wanachokifanya kama ni karoti imeletwa pale wanapima karoti ukubwa huu inaitwa ni grade one, ukubwa huu grade two; hii itaenda nchi fulani, hii itabaki hapa watakula Watanzania, hili jambo tunaweza kulifanya kwetu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana wakati tunasaini Mkataba huu, tukimbie haraka kuimarisha sheria na taasisi zetu ili na sisi tuweze kufaidi kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ningeshauri, ili tuweze kunufaika pia hebu Serikali itazame namna ya kuwa na kiwanja kimoja cha ndege ambacho kitawavutia watu kuja kununua mazao kwetu kupitia usafiri wa anga. Na kiwanja chenyewe tukitumie kile cha Kilimanjaro Airport, tuondoe kodi ndege zinapotua pale iwe ni free, kodi iwe ni bure pale ili tuwavutie kwa sababu changamoto iliyopo sasa hivi, mizigo kutoka huku Tanzania kwenda nje ya nchi ipo ya kutosha lakini mizigo ya kutoka nje ya nchi kuja huku haitoshi. Sasa ili kuwavutia watu waweze kuja kununua mazao yetu, tuweke Kiwanja cha KIA kile kiwe cha mkakati tuwaambie leteni ndege zenu msilipe kodi. Tukiamua hivi, itatusaidia sana kuhakikisha tunafaidi kwenye Itifaki hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho; niombe hebu tutazame sasa hivi. Tumeshazungumza muda mrefu Serikali yenyewe pamoja na kwamba tunafanya kwa ubia, hebu tengenezeni kiwanda kimoja cha mfano cha kuongeza thamani ya mazao yetu. Wananchi, tunaweza tukafanya kwa mfumo wa ushirika kama tunavyofanya kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwa ukanda wa kaskazini pale Hai mnajenga kiwanda cha kufungasha mazao, wanaotoka Tanga wanakuja wanafungashia pale yanaingia kwenye cold room ya KIA iliyopo pale yanaenda nje ya nchi, ili uwekezaji wa aina huu utatusaidia sana lakini kama tutasaini Mkataba huu na hatutaangalia taasisi zetu, hatujajiandaa kuingia kwenye Soko la Dunia ambalo na lenyewe lina standard ya bidhaa zinazotakiwa kuingia huko, tutakuwa hatujafaidi Mkataba huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nashauri sana tuzingatie mambo haya, tuimarishe Sera yetu ya Kilimo, tuwafundishe wakulima wetu kulima kisasa, tulete sheria hizi tatu kwa maana ya wanyama, mimea na chakula tuzitengeneze hapa na tuhakikishe miundombinu yetu inakuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)