Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na wachangiaji wenzangu kwanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu; Waziri Mkuu; Makamu wa Rais; Mawaziri na Waziri mwenye dhamana hii ya afya, pamoja na Naibu na Watendaji wake wote, kwa namna ambavyo wameonesha vizuri mwelekeo wa bajeti hii kwa mwaka wa 2016/2017. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwe wakweli. Unajua wakati fulani vijembe hivi! Hivi kweli pale Muhimbili hakuna mabadiliko! Muhimbili ukienda sasa hivi pana mabadiliko makubwa kabisa. Duka la MSD Mheshimiwa Rais alisema litakuwa pale, Waziri mwenye dhamana amesimamia liko pale. Vitu vingine, kuna mabadiliko makubwa! Kwa kweli tuwatie moyo kwa kazi nzuri mnayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi kuna mchangiaji mmoja alizungumzia lugha fulani iliyokuwa inagusa akinamama. Akinamama wametuzaa; kalipuka! Ni mama zetu hawa, wametuzaa, lakini mmoja vile vile siku ya nyuma yake pia naye alidhalilisha akinamama hawa hawa! Alitamka kwamba alipokwenda huko wakapigwa, wakakatiwa shanga zao. Hivi ndiyo vya kuzungumza hapa vitu nyeti kama hivyo? Eeh! Sasa niseme, kama Mwenyekiti wa CCM mwenzangu kwa yule kijana ambaye Mbunge alizungumzia lugha ambayo CCM hatukumtuma, mimi namwombea radhi kama Mwenyekiti. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tuliopo hapa, kila mmoja ana akili; na wakati fulani tuliopo hapa wote ni vichaa, lakini vichaa vinatofautiana. Ukienda upande wa elimu na ndiyo maana sekondari, shule za msingi na kadhalika huwa kunakuwa na shule za watu wenye vipaji maalum. Maana yake hawa wana akili kuwazidi wenzao. Sasa baadhi ya Wabunge hapa walizungumzia habari ya viti kumi ambavyo Mheshimiwa Rais anawateua kwa kazi maalum, kwa vipaji maalum. Ndiyo maana alimteua Mheshimiwa Tulia, Naibu Spika kwa kazi maalum. Kwa hiyo, tusimwingilie Mheshimiwa Rais, kazi ambazo anawateua watu, zile nafasi kumi amemteua Waziri wa Fedha, ameteua na wengine, tusimwingilie nafasi zile kumi. Hata Mheshimiwa Mbatia amewahi kuteuliwa kupitia Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie habari ya Jimbo la Makambako. Nilimwandikia Mheshimiwa Waziri ile ahadi ya Mheshimiwa Rais. Ndugu zangu, naishukuru Serikali, miaka miwili, mitatu iliyopita mmepandisha hadhi Kituo cha Makambako kuwa hospitali na mmetuletea Madaktari wa kutosha, tunao. Tatizo kubwa nimekuwa nikisema hapa na niliseme tena kwa Mheshimiwa Waziri, tuna jengo la upasuaji, tulichokikosa ni vifaa vya upasuaji. Gari letu la wagonjwa limekuwa likipeleka watu Njombe kila siku, mara saba, mara tano mpaka mara nane. Ni gharama kubwa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha na nilimltea, akaniambia Daktari anipe orodha ni vitu gani vidogo vidogo ambavyo vimekosekana. Nilimpa! Atakapohitimisha aniambie wamejipangaje kuona sasa tunapeleka vifaa vya upasuaji pale Makambako ili kuwaokoa akinamama na watoto, gari lisiwe linakimbia kwenda Njombe na Ilembula. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati huo huo hospitali yetu ya Makambako tuna wodi ya akinamama na watoto. Wodi nzuri iliyojengwa zaidi ya miaka miwili, vimebakia vitu fulani fulani havijakwisha; miaka miwili tume-invest pale hela ya Serikali. Nawaomba Wizara waone uwezekano wa kuona tunamalizia jengo hili ili liweze kufanya kazi iliyokusudiwa. Chonde chonde, ili kuokoa hela ya Serikali ambayo imeendelea kukaa kwenye majengo hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kufungua maduka ya MSD katika hospitali zetu za mikoa na wilaya, naomba sana, Mkoa wetu wa Njombe ni mpya. Mkoa huu ndiyo Mkoa ambao sasa una kitega uchumi kikubwa ambacho kitaanzishwa, Liganga na Mchuchuma. Kwa hiyo, naomba sana tuhakikishe tunapeleka Duka la MSD la Madawa pale Mkoani Njombe ili kuwasaidia wananchi wetu wa Wilaya na Mkoa wa Njombe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Halmashauri ya Mji wa Makambako tumejenga zahanati tisa katika vijiji tisa; na karibu zahanati saba tumeshazipaua. Naomba Serikali ione upo umuhimu sasa wa kutenga bajeti ya kumalizia kuwaongezea nguvu wananchi hawa wa Mji wa Makambako. Hili linawezekana na ni kwa nchi nzima. Yako majengo ambayo yamejengwa hayajamalizika, tunaomba Serikali itenge fedha kwa ajili ya kumalizia haya majengo ambayo yalishajengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tuna Kituo cha Afya ambacho kilijengwa katika Kata ya Lyamkena. Kituo hiki cha Afya kina zaidi ya miaka miwili. Kilishapauliwa na kadhalika, bado hakijamaliziwa, kimeendelea kukaa pale. Jengo hili la kituo cha afya, inawezekana kabisa na majimbo mengine vituo vya afya kama cha Makambako, vipo! Tutenge fedha kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ili kazi iliyokusudiwa iweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana kwa kasi anayokwenda nayo ambapo yuko nyuma ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imani yangu na imani ya Wabunge hawa, atatufikisha salama. Nampongeza sana kwa dhati pamoja na Watendaji wake. Kwa hiyo, ni imani yangu kwamba haya ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema, atakapokuwa anahitimisha, basi ni vizuri atueleze kwa ujumla wake ili tuweze kuwa kitu kimoja na CCM ahadi ambazo iliahidi, tunamtegemea yeye kupitia Wizara hii ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo haya, nisiwachukulie muda wenzangu, niseme tu naunga mkono hoja ya Waziri wa Afya kwa asilimia mia moja. Nawashukuru sana.