Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza, nimshukuru Mwenyezi Mungu anisaidie kwa haya nitakayochangia kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kumpongeza Waziri wa Kilimo, Prof. Mkenda, Naibu wake Mheshimiwa Bashe, Katibu Mkuu na wataalamu wote wa Wizara ya Kilimo kwa jinsi mlivyotupitisha kwenye Itifaki hii na tukaweza kuelewa. Hata ambao hatukuwa wanasheria mliweza kutubeba vizuri sana na tukaelewa. Nimpongeze pia Mwenyekiti wangu wa Kamati na niungane naye moja kwa moja kuunga mkono maoni yote ya Kamati yaliyowasilishwa mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie kiti chako kuwaomba Wabunge Wabunge lako Tukufu tukubali kuingia kwenye Itifaki hii ya Afya ya Mimea, Wanyama na Mifugo kwa usalama wake. Sababu zinazonifanya niwaombe tukubali ni kwa mustakabali wa Taifa kwa mazao yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia jiografia ya Tanzania tuko katikati ya nchi zote kimpaka lakini Mungu katubariki kwa ardhi yetu yenye rutuba, ardhi ambayo inaweza ikaotesha kila zao. Ukiangalia kwa Afrika Mashariki sisi ni wakulima wakubwa wa mahindi, mpunga na hili zao la parachichi ambalo limeongezeka ambalo ni dhahabu ya kijani. Sasa bila kuwa na Itifaki ya kulinda mazao yetu tutakuwa tunaibiwa kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano leo hii maparachichi yetu yananunuliwa Njombe yanapelekwa Kenya yanawekewa label yanapelekwa kama ya Wakenya, lakini kama tutakuwa tumejiunga kwenye hii Itifaki tuna uwezo wa kuwaambia na ku-harmonize nao kwamba hapana mkinunua kule lazima yaende na label ya Tanzania, kwa hiyo Itifaki itakuwa imetusaidia kwa aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna kilimo cha mbogamboga ambapo mikoa yetu yote iliyo mipakani inaweza ikalima mazao hayo mfano, Kigoma, Kagera, Arusha na Kilimanjaro tunaweza tukaotesha mazao ya mbogamboga na kuweza kuyauza kwa nchi za Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mazao ya maua vilevile ambayo yanaoteshwa Kilimanjaro na Arusha, ni Mikoa ambayo ipo mpakani ambayo Itifaki hii itatusaidia maua yetu yasiwe yanapelekwa nchi nyingine yanakwenda nchi za Ulaya na Asia yakionekana yametoka kwa nchi hizo kumbe yametoka Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hasara ambazo tunaweza kupata bila kuingia kwenye hii Itifaki ni kwa sababu ya kuwa sisi tutakuwa tunatembea peke yetu, lakini hata kwenye kitabu cha Mungu kwenye Amosi 3:3 imesema; watu wawili msipotembea pamoja hamuwezi kupatana. Kwa hiyo hii Itifaki itupeleke basi tukapatane na Afrika Mashariki nzima, tuweze kwenda kwa pamoja, tuweze kutetea mazao yetu, mifugo yetu na uvuvi wetu wa samaki, kwa sababu tumebarikiwa hata sisi ndio tuna Maziwa, Mito na Bahari kwa asilimia kubwa sisi ndio tuna maji mengi hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunavyokuwa hatuko kwenye Itifaki, kwa mfano ukienda Mkoa wa Kagera boti nyingi za Uganda zinakuja kuvua Kagera na kupeleka samaki wetu, lakini kama tungekuwa tumeshajiunga na tuna Itifaki hii tuna uwezo wa kukaa nao mezani na kuongea nao kwamba wasifanye hicho wanachokifanya basi, wavuvi wa kwetu ndio wavue tuuze ndani ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niwaombe Wabunge wenzangu kwa hizo sababu nilizozitaja tukubaliane kwa pamoja kwenda kwenye Itifaki hii, hata sisi tulikuwa tuna wasiwasi kwa nini imechukua muda mrefu lakini tumeelezwa ni kwamba nchi ilikuwa kwenye kujiridhisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa majira na wakati huwa yana wakati wake, umefika wakati ambapo Taifa limejiridhisha sasa kwamba tunaweza tukaenda kwenye Itifaki tukiwa tumejiandaa kwa mfano kwenye mimea tayari wamekuja na sheria tatu zitakazotulinda kwenye Itifaki hiyo. Lakini hata kwenye mifugo na uvuvi tumeielekeza Wizara ya Uvuvi na Mifugo, nao waandae sheria sasa zitakazotulinda kwenye Itifaki hii nao wameahidi watazileta haraka sana kwako, ili Bunge lako lizipitie, basi twende kwenye Itifaki hii tukiwa salama kwa kulinda Watanzania na mali zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)