Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi kuchangia katika mjadala huu muhimu sana wa sheria ndogo na awali ya yote niwapongeze sana Wajumbe wote wa Kamati hii kwa namna ambavyo wamechakata na kuleta mapendekezo yao juu ya nini sasa kifanyike kwa ajili ya kufanya marekebisho ya sheria hizo.

Mheshimiwa Spika, jambo ambalo limenisimamisha hapa leo ni ushirikishwaji wa wadau kwenye kutunga hizi sheria ndogo kwenye mamlaka zetu. Tumeshuhudia maeneo mengi sheria hizi zimetungwa katika mazingira ambayo hazitekelezeki, lakini katika mazingira mengine sheria hizi zinakinzana moja kwa moja na Katiba na sheria mama.

Mheshimiwa Spika, sasa ninaomba sana Bunge lako pamoja na Kamati hii ya Sheria Ndogo kuzichambua zile sheria ndogo ndogo zote ambazo zinakinzana na sheria mama lakini zinatengeneza mtafaruku kwa wananchi katika utekelezaji wake ili kuendelea kuishi katika nchi ambayo ina amani na utawala wa kisheria.

Mheshimiwa Spika, nitakupa mfano wa sheria moja ndogo ya rumbesa. Kuna sheria ambayo inazuia kupakia mzigo kwenye magunia isizidi kilo kati ya 100(+5 na -5). Lakini namna wanavyotekeleza hii sheria, wanapima yale magunia baada ya kupakiliwa kwenye magari badala ya kupima uzito wa gari kwenye mizani.

Mheshimiwa Spika, mimi ninachofahamu, kama unataka kudhibiti rumbesa na kwa sababu rumbesa imewekwa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wasilanguliwe kwenye biashara ya mazao, pale wakati wa ununuzi wa mazao, kama unanunua mahindi kwenye eneo la soko pale ndipo ambapo vipimo vinasimamiwa, mnunuzi anunue kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa katika soko lile.

Mheshimiwa Spika, lakini wakati ameshapakia ule mzigo, kwa sababu unakuta mnunuzi mwingine amenunua mahindi au kabichi au karoti, amekwenda kuzimwaga kwenye chumba kimoja halafu baada ya kununua mazao yake yote anakwenda kuyapaki kwenye magunia na kusafirisha. Wakati anapaki kwa kuwa tayari alikuwa ameshapima wakati wa kununua, wakati wa kupaki anaweza kupaki kienyeji kadri ambavyo anaweza ili kuweza kupunguza gharama pia ya vifungashio.

Mheshimiwa Spika, sasa kinachotokea wenzetu wana-block barabarani, wanaweka vizuizi barabarani na kuanza kupima gunia mojamoja ambalo liko ndani ya gari, kinyume na utaratibu ambao umewekwa kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninaomba sheria hizo zote kwa sababu zimewekwa kwa nia njema na ni sheria nzuri na lengo ni kumlinda Mtanzania aweze kufanya shughuli zake katika mazingira yenye ustawi, ziangaliwe na zitengenezewe kanuni nzuri za utekelezaji ili tusiwaumize hawa pia wanaofanya biashara ya usafirishaji wakati wa kusafirisha mazao haya.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ninapenda kuchangia ni hili la kuandaa sheria hizi kwa mujibu wa sheria mama. Tumeona katika mazingira mengi, na moja amelizungumza Mheshimiwa Naibu Spika kwenye taarifa yake, uki-park gari vibaya Dar es Salaam, gharama ambayo unapigwa inakwenda tofauti na gharama ile ya tozo/faini za magari kwa maana ya makosa barabarani; zinakwenda tofauti.

Mheshimiwa Spika, lakini sheria ambayo tunaifuata ya msingi ni ile ya faini za barabarani. Kwa nini huyu wa jiji akamate tozo kubwa ya faini unapo-park sehemu pengine ambayo siyo rasmi, au unapofanya kosa lolote la matumizi ya magari kwenye maeneo hayo, tofauti na ile tozo mama ambayo imekuwa-defined kwenye sheria.

Mheshimiwa Spika, maeneo hayo yote yakifanyiwa kazi tutaendelea kuishi kwenye mazingira ambayo kila mmoja ataiheshimu sheria na mwisho wa siku tutaendelea kufanya vizuri.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Ester Bulaya.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa tu nampa taarifa kwa sheria ndogo ndogo ambazo zinakera, kulikuwa na mgomo wa waendesha bajaji wa Musoma Mjini, Manispaa ile Halmashauri ni ya Chama cha Mapinduzi. Bajaji akimpeleka mteja haruhusiwi kumpakiza mtu, arudi kwenye kituo chake bila abiria, akipakiza faini shilingi 3000. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Husna, unapokea Taarifa hiyo?

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, ubaya wa hizi sheria ndogo nyingi zimetungwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo halmashauri zetu nyingi zilikuwa na mchanganyiko wa vyama vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee mchango wangu kwenye eneo la elimu, tuna sheria nzuri sana nchini, lakini wananchi hawazifahamu sheria kwa sababu hakuna utolewaji …

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe tu taarifa Mheshimiwa Husna kwamba tukiangalia michango yote ni kwamba kweli hizi sheria ndogo ndogo zinakera, lakini ukitaka kuweka mizania ya vyama mchanganyiko na nini kwa zaidi ya asilimia 80 Halmashauri zilikuwa chini ya Chama cha Mapinduzi na sheria nyingi ambazo zinakera nyingi nyingi Tanzania zimetungwa na hao wa Chama cha Mapinduzi.

Kwa hiyo tuondoe mambo ya uvyama tuangalie nini solution kubwa kwa kuondoa hizi kero ndogo ndogo tukianza kuchagiza CHADEMA, CCM mtajikuta mnajimaliza, maana yake zaidi ya asilimia 80 ilikuwa chini ya Chama cha Mapinduzi, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Taarifa hiyo Mheshimiwa Husna unaipokea?

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, siipokei hiyo taarifa kwa sababu Mheshimiwa Esther Matiko alikuwa ana nafasi ya kuomba kuchangia, nimuombe tu aheshimu nafasi yangu ya kuchangia ili niweze kumaliza mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa la utekelezaji wa sheria nchini ni watu kukosa elimu juuu ya sheria na unafahamu kabisa kwamba kutokujua sheria siyo utetezi mbele ya sheria. Ningeomba sana Kamati ya Sheria Ndogo hii ya Bunge kuelekeza mamlaka zetu kutoa elimu kwa wananchi kabla ya utekelezaji wa sheria iliyotengenezwa kwenda kutekelezwa, hii itatusaidia sana kupunguza migogoro, kupunguza manung’uniko na mwisho wa siku kutekeleza sheria hizi katika hali ambayo ni salama kwa ajili ya malengo ya sheria zilizotengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunipa ruhusa ya kuzungumza, ahsante sana. (Makofi)