Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Pili wa Bunge

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia kwenye taarifa hii ya Kamati ya Sheria Ndogo nanikushukuru sana kwa nafasi ya kuniteua kuwa katika Kamati hii, na nikiri imekuwa ya manufaa sana kwangu hasa ukilinganisha kwamba mimi nilikuwa Diwani miaka 10; kwa hiyo, chini kule niliona sheria hizi zinapoanza, na namna zinakuja kuhitimishwa huku juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitakwenda kwenye ujumla tu; la kwanza ambalo limeongolewa na watu wengi ni lile suala la ushirikishwaji wa wadau. Kuna upungufu mkubwa sana, yapo mambo mengi ambayo Kamati inafanyia kazi lakini wadau wangeshirikishwa tangu awali wala hayo mambo yasingetakiwa yatufikirishe sana kwenye hizi ngazi za juu. Kwa hiyo ninaomba sana sheria ndogo hizi hasa za Halmashauri ushirikishwaji wa wananchi usiangalie tu ile ya kutoa matangazo kwenye mbao za matangazo, lakini viko vikao vya chini kama vikao vya mitaa ambavyo sheria hizi zikipelekwa na wataalam wakitoa elimu kule basi mambo mengi yanaweza yakajaziwa nyama na mengine yakarekebishwa kabla ya kuja ngazi za juu na kuja kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sura nyingine ambayo inaonekana kwa haraka katika kodi nyingi ambazo tumeziona hasa za Halmashauri ni position ya watu wawili ambao wanahusika na utungaji.

Mheshimiwa Spika, wataalam inaonekana wao wanakuwa na pressure ile ya kuongeza mapato kwa hiyo wanakuwa wanazijazia tu mapato unakuta kuna mahali tuliona sheria imeletwa eti kuuza dawa za kienyeji kuwe na tozo kwa siku shilingi 1,000/shilingi 5,000; hizo dawa za kienyeji ukiangalia zingine hata hayo makusanyo ya siku hayafiki hiyo shilingi 5,000. Kwa hiyo, kunakuwa na ile presha tu ya kuhakikisha kwamba watendaji wanataka kukidhi kiu ya kupandisha mapato na inapoenda kwa pressure na kwa viongozi kama Madiwani nayo inapita basi ikija huku uhalisia unaonekana hauwezekani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nadhani inahitajika wakati makundi haya mawili kwa maana ya kwamba watendaji pamoja na wawakilishi waangalie uhalisia wa ukusanyaji wa kodi kwa sababu baadhi ya kodi ilionekana, hata gharama yake ya kukusanya ni kubwa kuliko kile ambacho kinahitajika kuja kuwa kinakusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini lipo suala lingine ambalo limekuwa linaleta matatizo sana kwenye Sheria Ndogo za Halmashauri, baada ya vile vitambulisho vya ujasiriamali wapo watu ambao wanakuwa excluded kabisa kutokana na ile definition kwamba turnover yao haizidi shilingi milioni nne. Lakini unakuta halmashauri nyingine wamewaleta hawa na kuwatungia sheria ambayo inawatambua katika kutozwa tozo mbalimbali. Sasa ukiangalia inakinzana na ile sheria au definition ya vile vitambulisho vya wajasiriamali wadogo. Kwa hiyo unakuta kuna muingiliano wa sheria mbili katika sehemu moja.

Mheshimiwa Spika, niongelee kidogo suala la filamu; tumepata matatizo sana kwenye sheria ile. Pamoja na mambo mengine, inasemekana waigizaji wetu wakitaka kuigiza kwa mfano kama polisi, wakaombe kibali polisi ili kuvaa zile nguo zinazofanana na polisi au jeshi. Lakini hata kutumia maeneo yanayofanana na ya Serikali wanasema inakinzana na usalama.

Mheshimiwa Spika, sasa wenzetu wanatengeneza mpaka maeneo ya bandia, hawa wa kwetu hawana uwezo huo, lakini sheria na kanuni unakuta zimewanyima kuingia huko na kama unavyofahamu, filamu ni jambo la kimataifa, zinakwenda kushindana na filamu nyingine. Sasa unakuta filamu zetu watu wanakuwa ni polisi lakini amevaa kama mwanamichezo, kwa hiyo uhaliasia unakuwa hauwezi kuonekana kwa sababu ya masharti ambayo tunaweka ambayo hayawasaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata kwenye mavazi, wadau walipokuja walituuliza swali ambalo pengine nafikiri hata Wabunge watashangaa; walisema masharti yamekuwa magumu kana kwamba inabidi hata mtu anayekwenda kuogelea kwenye filamu ya Kitanzania aogelee na hijabu. Sasa inaleta shida, ushindani kwenye soko la kimataifa, filamu zetu haziwezi kushindana na zile nyingine kwa sababu ya masharti ambayo tunajiwekea wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa kifupi kabisa huo ndiyo mchango wangu, na ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)