Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kutoa mchango wangu kuhusiana na bajeti hii ya mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, aidha nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa mwongozo wake aliotupatia tukaweze kuwasilisha bajeti hii ya aina yake, bajeti ambayo imegusa wananchi na bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge wameiunga mkono kwa kiwango cha hali juu kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nichukue fursa hii vilevile kuipongeza sana Kamati ya Bajeti ya Bunge lako Tukufu chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Daniel Sillo na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Kigua na Wajumbe wote wa Kamati hii, pamoja na Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa michango yao mizuri sana ambayo imesaidia sana katika kufanya tuweze kuwa na bajeti ambayo tutaikamilisha leo Mheshimiwa Waziri atawasilisha majumuisho yake ya ufanisi wa hali ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nianze kwenda moja kwa moja kwenye baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezichangia; hoja ya kwanza ambayo nilitaka kuizungumzia leo ni ufafanuzi wa hoja ambayo Waheshimiwa Wabunge wameizungumzia baadhi yao kuhusu miamala ya simu kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, wapo Wabunge ambao walitaka kuona kwamba fedha hii ambayo inakusanywa kwa malengo mema kabisa, je, fedha hii ambayo inatozwa kodi kwa wananchi wote wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini mipango ya matumizi yake haijagusa miradi ya maendeleo ya kijamii kwa upande wa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kutoa ufafanuzi huo naomba niseme neno moja kwa ufupi sana, Muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni muungano wa damu na ni muungano wa kindugu, si muungano wa vitu au maslahi hata waasisi wa Taifa hili kilichowashawishi na kuwafanya waweze kuunganisha nchi hizi mbili ni historia ya udugu wa damu baina ya pande hizi mbili tokea wakati kabla ya ukombozi wa nchi hii mpaka hivi sasa na haikuwa kwa sababu ya maslahi kwamba nani atapata nini na nani atafaidika na nini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini wakati kila miaka ikielekea mbele na vizazi vinavyoendelea kuzaliwa na sisi wazee ndiyo tunamalizika malizika, basi utaona kwamba hii dhana inaanza kupotea uelewa wake na ndiyo maana wazee hawa waliamua kwa makusudi kabisa kuweka kwenye Katiba kuanzisha Mfuko wa Pamoja wa Fedha. Dhamira yake ni hiyo hiyo kuweza kubaini mapato na matumizi ya Muungano ili yaweze kutumika kwa mujibu wa Katiba.

Mheshimiwa Spika, lakini wakati mchakato huo unaendelea kama ambavyo tumeahidi wakati tunawasilisha bajeti ya Wizara siku chache zilizopita, hivi sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuna baadhi ya mapato yake ambayo inaruhusiwa kukusanya yenyewe na hivi majuzi tu mliona Mheshimwia Waziri alivyozungumzia kwenye bajeti yake kuhusiana na mapato yanayohusu uhamiaji, kwa maana hiyo basi hatuoni tatizo lolote kwenda sambamba na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge na hivyo tumewapa wataalam kazi ya kuchambua matumizi haya ili pale zitakapokusanywa, zile fedha ambao zitakusanywa kwa Zanzibar ziweze kupelekwa Zanzibar, zitumike kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa kwamba tukifanya hivyo tutaweza kupanua ile dhana nzima ambayo tumekuja nayo ya kuhakikisha kwamba kila mtu analipa kodi na anafurahia hayo maendeleo ya kodi yake kwa sababu madhumuni ya kodi hii ni kugusa huduma za jamii, kodi hii ama tozo hizi zinagusa maisha ya watu watu moja kwa moja katika sekta zote za kijamii muhimu ikiwemo afya, elimu na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo limezungumzwa vile vile ni ile hoja ya kwamba taarifa ya ambazo zinatoka BOT kwenda masharika ya kimataifa hazina taarifa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, BOT ni chombo cha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taarifa za kifedha zote ikiwemo sera ya fedha pamoja na taarifa zingine zote zinahusisha ama zinazingatia upekee wa Zanzibar kwa uchumi wa Zanzibar. Lakini hoja ya taarifa zinazotoka World Bank na yenyewe tunaona ni ya msingi. Hivyo basi kwa kuanzia tumeamua kwamba tutawashawishi Benki ya Dunia wafungue ofisi yao Zanzibar ili kuweka karibu na kuweza kutatua tatizo hili kwa siku zijazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo mambo mengi ambayo yamefanyika kurekebisha zinazoitwa changamoto za Muungano na tumeweza kwenda nazo vizuri tu, hata hili ambalo Wabunge wengi wamelalamikia kuhusiana na changamoto ya magari ambayo yanakuwa registered Zanzibar kutokufanya kazi upande huu naamini kabisa muda si mrefu, Mheshimiwa wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa wakati ambao ataona unafaa na kama utaratibu zitakazokua zimekamilika za Kiserikali hataleta mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ambayo yataondoa moja kwa moja tatizo hili na kulipatia ufumbuzi wa kudumu. Kwa hiyo, kwa hayo makubwa tumemaliza hatuwezi kushindwa na hili dogo.

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ninalota kulizungumza ni changamoto ya upatikanaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi; mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha tunatumia rasilimali zetu vizuri ili tuweze kujitegemea, huo ndiyo mwelekeo wa msingi kabisa na ndiyo maana ukiangalia katika bajeti hii ni bajeti ambayo katika kipindi cha miaka kumi imeweza kuja na utegemezi mdogo wa asilimia 8.1 kutoka kwa wahisani, lakini ni lazima tukope ili tuendelee kama ambavyo walioendelea wanaendelea kukopa. Lakini cha msingi mikopo hii ambayo tunakopa tunataka tuhakikishe kwamba inaendelea kulengwa katika miradi ya maendeleo ambayo inachochea uchumi wa nchi hii. Lakini tuhakikishe mikopo hii inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuepuka mazingira yote ya ubadhilifu na wizi wa fedha hizi.

Mheshimiwa Spika, sasa katika kufanya hivyo Serikali yetu hii ya Awamu ya Sita imeendelea kuhakikisha kwamba inaimarisha mahusiano na Jumuiya ya Kimataifa na ninyi mashahidi kwa kipindi kifupi toka Mama Samia ameingia madarakani ameweza kuimarisha mahusiano ya kimataifa na tumeweza kupata mikopo yenye masharti nafuu ya zaidi ya dola 1500 kwa kipindi kifupi na mikopo hii ya masharti nafuu ni muhimu sana ili kwanza kuhakikisha tunalinda maadili na heshima na uhuru wetu, lakini vilevile tunapata mikopo haiwi mizigo kwa wananchi wa nchi hii yenye riba nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mikopo hiyo zaidi tunalenga kama ambavyo Kamati na Waheshimiwa Wabunge mmeshauri ni mikopo ile ya concessional loans na semi concessional loans ambao vilevile ina element ya grant ndani yake na masharti yake yanaridhisha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na hoja deni tunaendelea kukopa haliyakuwa tukiji-proud kwamba deni letu ni himilivu, kwa sababu ukiangalia takwimu mpaka Desemba, 2020 uwiano wa deni la mapato ya ndani ni asilimia 13.7 wakati ukomo ni asilimia 23; kwa hiyo tuko vizuri, ziko nchi majirani zetu wanakaribia kufika kwenye ukomo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini maoni yenu kuhusiana na mchakato wa sovereign credit rating tumechukua na tunafanya kazi kama ambavyo tume ya Mheshimiwa Waziri imeelezwa na vilevile tutaendelea ku-maintain ukopaji wa ndani wa chini wa kiwango cha asilimia moja ya pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo imezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusiana na projection ya asilimia 5.6 ya ukuwaji wa uchumi kwamba ni ndogo sana. Projection hii imezingatia nadharia nzima ya hali ya ulimwengu wetu na mazingira yaliyonayo sasa hasa katika kipindi ambacho ulimwengu umekumbwa na janga la UVIKO 19. Hali hiyo imesababishwa hata uchumi wa dunia na wenyewe ukuaji wake projection yake iwe kwa asilimia sita kwa mwaka unaokuja, ingawa inatarajiwa vilevile mwaka 2022 kurudi katika kiwango cha asilimia 4.4 almost kiwango cha kawaida.

Mheshimiwa Spika, ukuwaji wa uchumi wa nchi zilizopo chini ya Jangwa la Sahara wenyewe unakadiriwa kuwa kwa asilimia 3.4. Kwa hiyo, sisi makadirio yetu asilimia
5.6 yamezingatia mazingira mazima ya hali ya uchumi wa dunia ingawa maoteo yetu kwa miaka mitano inayokuja kama ambavyo mpango unaeleza ni kufikia kiwango cha asilimia nane.

Mheshimiwa Spika, tumeweka mazingira mazuri na misingi mizuri katika bajeti hii ili malengo ya asilimia nane yaweze kufikiwa na mambo haya ambayo tumefanya miongoni mwao kwanza ni kuhamasisha matumizi ya malighafi zetu za ndani ili kuongeza mnyororo wa thamani, lakini pia kuimarisha miundombinu wezeshi hususani sekta ya usafirishaji kwa maana ya barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari halikadhali nishati na umemelakini kuhakikisha tunaimarisha uwekezaji na biashara wa sekta binafsi tunaamini kabisa mambo haya ndiyo msingi ya bajeti yetu tukiyasema vizuri ongezeko la ukuaji wa uchumi kwa asilimia nane kwa miaka mitano inayokuja tutaufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine la kuzingatia na lamsingi kabisa ni kwamba katika bajeti hii tumetenga asilimia 37 ya bajeti kwenye maendeleo ambayo yanachochea ukuaji wa uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa mengine ambayo nilitaka niyazungumze kwa haraka haraka kuna hoja kadhaa ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezungumza ikiwemo hoja hii ETS, lakini vilevile kulikuwa na hoja ya gypsum pamoja na hoja ongezeko la kodi kwa matrela haya.

Mheshimiwa Spika, nimebahatika kuongoza kikao kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri ambacho kilihusisha baadhi ya malalamiko mengi ambayo yalijitokeza kuhusiana na hii suala ya ETS, kwa hiyo, hatua ambayo tulichukua tuliona kuna umuhimu wa kuzikutanisha pande zote ili tuweze kujua, kusikiliza hoja za pande zote mbili na kutoa maamuzi sahihi. Katika kikao hicho ambacho mimi ndiye nilikuwa Mwenyekiti wake tulikubaliana yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza; tumekubaliana kwamba hoja ya Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na ukubwa wa gharama wa ETS ni sahihi, lakini tumekubaliana kwamba matumizi ya teknolojia hii ni muhimu sana katika kuhakikikisha kwamba tunadhibiti mapato ya Serikari. (Makofi)

Kwa hiyo maelekezo ambayo tumetoa ni kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweza kukutana na wadau hawa ili kufanya majadiliano ikiwemo pamoja na mambo mengine kuangalia uwezekano wa kuweza kushusha gharama hizi ambazo zinalalamikiwa ambao ni mzigo kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wakati hilo linaendelea hali kadhalika tumewaelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania kujipanga ili siku zijazo zoezi hili waweze kulifanya wenyewe. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kana kwamba hiyo haitoshi kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hili tumekubaliana kwamba kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu unaojitegemea ili kubaini kwa undani kabisa masuala yote yanayohusu utekelezaji wa mradi huu na jambo hilo litasaidia kuweza kutupa mwongozo wa baadaye wa kuweza kutoa maamuzi sahihi ikiwemo wakati wa majadiliano ya kibiashara pamoja na wawekezaji wanaohusiana na biashara ama hata ikifika mahali tumeweza wenyewe kufanya basi tuwe tunaweza kufanya tukiwa tuna taarifa ambazo za kitalaam na zimethibitishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna mambo ambayo mengine yamezungumzwa niseme tu kwa ufupi ni kwamba tumeyapokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge na yale ambayo pengine kutokana na muda hatuwezi kuyaeleza najua Mheshimiwa Waziri ataeleza mambo mengi, lakini kwa sababu mambo ambayo yamezungumzwa ni mengi na hatutaweza kuyamaliza yote kwa leo.

Mheshimiwa Spika, tuhakikishie kwamba tumeyachukuwa na tutazingatia maoni ya Waheshimiwa Wabunge ikiwemo mambo haya mawili ambayo sikupata muda wa kuyazungumzia ya ile hoja ya gypsum pamoja na ongezeko la kodi ya ushuru wa forodha kwenye matrela, lakini tutayachukulia hatua kwa mujibu wa maelekezo na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana; naunga mkono hoja. (Makofi)