Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipa fursa hii niweze kuchangia hoja ya Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na wataalam wote kwa kuandaa bajeti nzuri ambayo kwa kweli inakwenda kutatua changamoto katika maeneo yetu katika ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata, Halmashauri na Wilaya. Kwa hiyo, katika hatua hii nasema naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri ambao mmetupatia katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuboresha elimu msingi na sekondari, kuboresha huduma za afya ya msingi katika zahanati, vituo vya afya na Hospitali za Halmashauri. Ushauri mzuri mmetupatia kwa ajili ya kuboresha barabara za vijijini na mijini kupitia TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumepokea ushauri wenu Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuimarisha Utawala Bora ikiwemo usimamizi wa rasilimali fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Waheshimiwa Wabunge, tunawashukuru sana na tunawaahidi kwamba tutafanyia kazi ushauri wenu na tutatoa taarifa kupitia kwenu kupitia Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijibu mambo makubwa matatu au manne. Jambo la kwanza, Waheshimiwa Wabunge tumepokea ushauri wenu. Kwanza tunapokea pongezi kwa Serikali kupitia Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ya kuamua kubeba mzigo wa posho za kila mwezi za Madiwani kulipwa na Serikali Kuu. Pia tumepokea maoni yenu kwamba sasa kile ambacho kitaokolewa kiende kikalipe fedha au posho kwa Wenyeviti wa Vitongoji na Vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili linatakiwa kufanya uchambuzi, lakini tumeona mahesabu ya haraka haraka, tunaweza tukapata savings. Mheshimiwa Comrade Mkuchika katika Halmashauri yake ya Mji wa Newala wana Madiwani
22. Kwa hiyo, Madiwani wa Kata ni 16 na wengine ni wa Viti Maalum. Kwa hiyo, kama wangelipa Halmashauri, ni kama shilingi milioni 7.3. Kwa sababu Serikali inabeba huu mzigo; na kwa sababu pia tumeelekeza ile shilingi 100,000 angalau ikalipe posho za watendaji wa Kata, kwa hiyo, ukitoa shilingi milioni 7.3 na shilingi milioni 1.6, Halmashauri itabakiwa au ita-save shilingi milioni 5.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, inawezekana kabisa kuwapa hata hela kidogo; shilingi 20,000 ya kuweza kuwasaidia. Kwa hiyo, hili Waheshimiwa Wabunge tumelipokea na tutalifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili tumepokea maoni ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika Halmashauri zetu hususan masoko yamejengwa au stendi ambayo hayaleti tija au yamekuwa ni kero katika baadhi ya Halmashauri. Tumepata ushauri kutoka kwenye Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Comrade Sillo; tumepata ushauri kutoka Kamati ya TAMISEMI inayoongozwa na Comrade Polepole. Kwa hiyo, tutafanya mapitio ya utekelezaji wa miradi yote ya kimkakati. Waheshimiwa Wabunge mtashiriki kuamua miradi hii katika majimbo yenu iende ikatatue kero gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Watanzania hawataki soko la ghorofa, wanataka simple soko. Kuna roofing, chini kuna floor nzuri, lakini pia ina maeneo mazuri. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, haya tutayashirikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu ni TARURA. Tunawapongeza na kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa kueleza kilio chenu kuhusu ubovu wa miundombinu ya barabara katika majimbo yenu na Halmashauri zenu. Ni kweli, TARURA imeanzishwa chini ya Sheria Na. 13 ya 2007 na TARURA inafanya kazi kwa mujibu wa sheria ndani ya Tanzania Bara. Kwa hiyo, mtandao ambao TARURA unahudumia ni kama zenye urefu wa kilometa 100,008.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna utafiti, barabara za lami ni asilimia 2.1, barabara za changarawe ni asilimia 25 na barabara za udongo ni asilimia 72. Kwa hiyo, kwa kweli kilio cha ubovu wa barabara ni kikubwa. Kulikuwa na mvua, kwa hiyo, pia imefanya barabara zetu nyingi hazipitiki na ukiangalia hali ya barabara ni asilimia 23 tu ya barabara zetu kwa mujibu wa Taarifa ambazo ninazo ndiyo ziko katika hali nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tumesikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge. Namshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Fedha, kwamba sambamba na fedha ambayo tunaipata kupitia Mfuko wa Barabara Mheshimiwa Waziri Chamuriho ameeleza, kuna fedha angalau Hazina walitutengea kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara. Ndiyo maana katika ile dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia ya kuwashirikisha Wabunge, tukasema badala ya kuwaachia wataalam waamue fedha hizi ziende wapi, tukaona kila Mbunge tutende haki na usawa kwa kila jimbo, shilingi milioni 500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze, ninaposema kila jimbo, ni jimbo ndani ya Tanzania Bara kwa sababu TARURA kwa mujibu wa sheria inafanya kazi ndani ya Tanzania Bara. Kwa hiyo, naomba niweke vizuri hili. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge shilingi milioni 500 siyo nyingi lakini tunaamini inaweza kuleta mabadiliko makubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kesho Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ana mambo mazuri zaidi anakuja nayo. Mapendekezo yetu Waheshimiwa Wabunge, kwenye nyongeza hii ambayo tutapata kutoka Hazina, Wabunge wa Dar es Salaam mnisamehe, mtapata DMDP II. Kwa hiyo, hatutawaingiza kwenye fedha itakayoongeza, kwenye hela ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, kuna miji 45 tunategemea itapata fedha kupitia mradi wa TACTICs. Kwa hiyo, tutawoandoa pia kwenye fedha hizi ambao Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atatupa. Kwa hiyo, Wabunge tunaamini badala ya shilingi milioni 500 mnaweza mkajikuta mnaondoka hata na 2B. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa namsafishia njia Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Kwa hiyo, mambo mazuri tutayasikia kesho. Wabunge wa Dar es Salaam DMDP II, mambo mazuri; Wabunge wa Majiji 45, Mheshimiwa Naibu Spika, nawe ni mnufaika. Mambo pia yanakuja vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la nne ni la kuboresha miundombinu ya elimu msingi na sekondari. Waheshimiwa Wabunge tumepokea ushauri wenu lakini kubwa zile shilingi milioni 600 tunawaomba sana, tunataka shule iliyokamilika, yenye madarasa nane, yenye vyumba vya maabara vitatu. Yenye nyumba mbili za walimu; two in one na yenye vyoo. Kwa hiyo, mnaposema tuwagawie kidogo kidogo, Waheshimiwa Wabunge tunaomba sana, hebu tufanye kitu complete kipendeze katika majimbo yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwapa siri nyingine, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kesho anakuja na mambo mazuri zaidi. Tutatoa fedha za kujenga madarasa haya mawili mawili, manne manne katika shule zenu zaidi ya 10 au nne katika majimbo yenu. Kwa hiyo, haya tunawaomba sana, shilingi milioni 600 hii ikatumike kufanya kazi iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dada yangu Mheshimiwa Prof. Ndalichako tunafanya kazi nzuri na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Tuna network, tuachieni, tutawatafutia fedha chini ya Rais Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kujenga miundombinu ya elimu, miundombinu ya afya na pia miundombinu ya afya katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hili nilitolee ufafanuzi. Kwa hiyo, tunaomba shilingi milioni 600 ile msiende kuikata kidogo kidogo. Nami nimeshawaambia watu wangu, kama tunampa Mbunge kwenda kuongeza madarasa, lisiwe chini ya madarasa mawili. Kwa hiyo, kila Mbunge kama atapata, angalau madarasa mawili, matatu au manne kwa ajili ya shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulisisitiza samahani sana Waheshimiwa Wabunge; sambamba na fedha ambazo tutazitoa kutoka Serikali Kuu nataka nikiri katika miezi miwili ambayo nimekuwa Waziri wa TAMISEMI, kuna ubadhirifu au matumizi mabaya ya fedha za Serikali katika Halmashauri zetu. Fedha zinapigwa ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge. Baadhi ya Halmashauri hawajali. Tukiwabana Halmashauri; nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, nasi sote ni Wajumbe wa Kamati za Fedha; wewe uliza, nataka kuona asilimia yangu 40 ambayo itaenda kutatua kero za ndugu yangu pale Jimbo la Tandahimba, kaka yangu. Kwa hiyo, mnatakiwa mkikaa, usikubali tu wakiwaambia ukarabati, sijui kumalizia, ndiyo wanapiga fedha. Mwulize umekarabati kitu gani? Umekarabati msingi? Umepiga rangi? Umeweka bati? Umeweka dari? Au umeweka floor chini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwaambia Waheshimiwa Wabunge bila kupepesa macho, tunazo fedha siyo nyingi, lakini zinaweza kwenda kutatua kero za wananchi wetu katika elimu na afya. Pia kuna Halmashauri zinapata zaidi ya shilingi bilioni 500. Waheshimiwa Wabunge, siyo vibaya kuweka bilioni moja kwenda kupiga kilometa mbili za lami katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kaka yangu Mheshimiwa Tarimba nadhani anafahamu, Kinondoni wanapata shilingi bilioni 33, wanatakiwa kupeleka kwenye maendeleo shilingi bilioni 19 kwa mwaka mmoja. Mheshimiwa Gwajima, ninyi sio masikini, yaani mna uwezo wa kupiga sekondari mbili za ghorofa kila mwaka za shilingi bilioni mbili mbili. Mna uwezo wa kupiga vituo vya afya viwili vya ghorofa kila mwaka, shilingi bilioni mbili mbili; kwa Mheshimiwa Gwajima na Kinondoni. Nawaomba sana tushiriki kuwasimamia Halmashauri zetu. Nasi tutajitahidi kuwapitia Waweka Hazina wa Halmashauri wote. Mama akishamaliza kuteua Wakurugenzi, tunaenda kufanya mapitio ya Waweka Hazina wote, lakini pia tunaenda kufanya mapitio ya Maafisa Mipango wote. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia kengele ya pili. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)