Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mariam Madalu Nyoka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambazo ameendelea kuzifanya, naipongeza Wizara ya Fedha kwa bajeti nzuri na bila kusahau Kamati ya Bajeti ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mheshimiwa Daniel Sillo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti yetu ni bajeti ambayo itaondoa changamoto nyingi za wananchi wetu. Hakuna Serikali inayotekeleza miradi yake bila ya kulipa kodi, hivyo niwaombe wananchi wenzangu tulipe kodi kwa maendeleo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu ni kwenye eneo la miradi ya kimkakati; miradi hii ya kimkakati ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba kila Halmashauri inajitegemea yenyewe kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali wakati wa upembuzi yakinifu wa miradi hiyo ni vyema tukawashirikisha wananchi pamoja na wadau wa maendeleo kwenye maeneo hayo badala ya ilivyo hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoa mfano Mkoa wa Ruvuma, Wilaya ya Songea Mjini kuna mradi mkubwa wa mabasi kule umejengwa wenye umbali wa takribani kilometa 21, kama wananchi wale pamoja na wadau wake wangeshirikishwa mradi ule ungejengwa lakini sio kwa umbali ule. Hivyo niiombe Serikali kufanya ushirikishwaji jamii wakati wa utekelezaji na hiyo ndio dhana ya utawala bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi viporo; ninaipongeza Serikali kwa kufanya mabadiliko ya Kanuni ya 21 ya Sheria ya Bajeti, Sura Namba 439 ya kuondoa urejeshwaji wa fedha za miradi kila ifikapo tarehe 30 Juni kila mwaka, na hivyo kusababisha fedha zile zitekeleze miradi yake kama ilivyokusudiwa. Niiombe Serikali kuhakikisha kwamba miradi ile iliyopangwa itekelezwe kama ilivyopangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishauri Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, kuimarisha Kitengo chake cha Monitoring and Evaluation (Tathmini na Ufuatiliaji) kwa kuunda timu ya kikanda na ya kitaifa katika kufanya ufuatiliaji na tathmini ya miradi ya maendeleo, kila robo mwaka ikiwashirikisha Madiwani pamoja na Wabunge wa maeneo husika kwa kila sekta. Kwa kufanya hivyo tutajua tumetoka wapi, tupo wapi na tunaelekea wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa mwisho ni kwenye eneo la ajira; ajira ni changamoto, asilimia 80 ya Wabunge katika kipindi hiki tumeshuhudia wananchi wetu wakitupigia simu za kuomba tuwasaidie kupata ajira. Ninaiomba Serikali yetu iweke uwiano katika utoaji wa ajira kwa kila Mkoa lakini kwa kuzingatia sifa za waombaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba nchi yetu hii ni kubwa sana na hivyo wananchi wake wapo vijijini na Mikoa ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.