Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha mchango wa maandishi kama ifuatavyo; kwanza sekta ya maliasili na utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na utalii; kwa miaka mingi sekta ya utalii imekuwa na mchango wa takribani 25% katika kuingiza fedha za kigeni, hata hivyo baada ya shida ya Covid-19 sekta hii imetetereka kwa hali ya juu sana, katika ajira sekta hii kwa ujumla inaajiri takribani Watanzania milioni nne. Baadhi ya nchi na hata mashirika makubwa ya fedha duniani yamekuwa yakitoa stimulus package ili walau kukabiliana na janga la Covid-19. Sisi Taifa letu bado haliwezi kubeba mzigo wa kuwa na stimulus package na ndio maana hata TANAPA imebidi kuisaidia. Kwa sababu hiyo nashauri tusiongeze tozo katika sekta ya utalii, tuache zilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wanyama pori/TAWA; naunga mkono suala la kugawa vitalu kwa njia ya mnada, hata hivyo ili tupate fedha lazima tuuze kwa bei rafiki kuliko ilivyo sasa ambapo vitalu vingi vinakosa wapangaji na tunakosa sio fedha tu lakini tunaviweka vitalu katika uhatari wa kukosa kuhifadhiwa kwa sababu masharti ya anayepewa kitalu ni pamoja na uhifadhi. Wenzetu Zimbabwe wana maeneo 40 tu lakini kwa mwaka wanapata around USD 130 million, mbali ya kupata fedha kwa kukodisha vitalu kuna faida mbalimbali kama vile ajira kwa rangers, fuel levy kutokana na magari yanayotumika na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwanza Serikali ijiridhishe kuhusu vitalu itabaini kuwa tunakosa fedha kwa sababu ya bei ya kuanzia, hivyo Serikali ipange bei za kuanzia ambazo zitavutia wateja, bei za USD 80,000 hazijaweza kutusaidia, tushuke walau hata nusu, haina maana tuna vitalu lakini hatuvikodishi, ni kama una nyumba unataka kuipangisha kwa shilingi laki moja kwa mwezi, hupati wapangaji kwa miaka mitatu, wakati ungepangisha kwa nusu ya bei, ungeweza kupata mapato lakini pia nyumba ikikaa bila kuishi mtu inachakaa. Nimetoa mfano wa kawaida kabisa wa ki-layman ili walau nieleweke, ninaamini vitalu vya uwindaji vinaweza kutuongezea mapato ya kutosha hata kuvuka bilioni 300.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni misitu/TFS; asilimia 60 ya ardhi ya Mafinga/Mufindi ni misitu, tuna msitu mkubwa wa Sao Hill, ni msitu mkubwa Afrika Mashariki na Kati. Hata hivyo wingi wa tozo umeendelea kupunguza wavunaji katika msitu na hivyo kukosesha Serikali mapato, wavunaji wana opt kwenda kuvuna miti ya wananchi ambayo haitoshelezi, nashauri VAT na LMDA ziondoshwe, duniani kote hakuna anayetoza VAT kwenye mti. Kwa mfano bei ya soko kwa cubic meter moja ni shilingi 320,000 kwa hiyo mvunaji ambaye anauza 320,000 anaingia gharama zifuatazo; ili upate cubic meter moja ya mbao unahitaji miti ya ujazo wa cubic meter tatu ambapo ni 3x64,940=194,820 hii royalty; kuna VAT 18% shilingi 35,068; kuna cess 5%= shilingi 9,741; kuna LMDA 17,000x3= shilingi 51,000 kwa sababu kama nilivyosema ili kupata cubic meter moja ya mbao unahitaji cubic meter tatu za miti na kuna TP yaani transit pass ya miti 7000x3= shilingi 21,000. Kwa hiyo jumla ya tozo ni shilingi 311,629. Ukichukua 320,000 ukatoa 311,629 mvunaji anabakiwa na shilingi 8,371. Hapa sijataja gharama nyingine za uendeshaji kama mafuta, vibarua wa kusogeza magogo na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii tozo tu ni 97% ndio maana wavunaji wanakimbia kuvuna katika msitu wa Serikali tunakosa fedha lakini pia ni double taxation kutoza VAT kwenye mti, halafu tena kwenye mbao, kadhalika cess inatozwa mara mbili, sio tu ni uonevu lakini pia ni kinyume cha sheria lakini pia hotuba inasema Serikali haitaki mapato ya dhuluma, haya pia ni ya dhuluma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tozo kwenye mafuta ya kula; ndugu zangu lazima tuwe honest, hatuwezi kulinda ambacho hakipo, mwaka wa nne sasa hatujaanza kuzalisha mafuta kutokana na mawese, lakini pia jitihada za kulima alizeti na ufuta hazijaimarika ipasavyo, kuongeza tozo ni kumtesa mwananchi, bei ya mafuta ya imekuwa ikiongezeka mwaka hata mwaka kwa zaidi ya 100%. Hivyo nashauri sana tuitazame hii tozo, tusilinde ambacho hakipo, Wizara ya Kilimo iongoze mbio kuhakikisha suala aliloanzisha Mheshimiwa Waziri Mkuu katika michikichi na alizeti ili tujikwamue kwa vitendo suala la mafuta ya kula, tusilinde ambacho hakipo.

Kuhusu uchukuzi/bandari/TAZARA; nashauri, kwa kuwa bandari ni chanzo cha mapato, yapo maeneo tuyaimarishe ili kupunguza muda wa kusafirisha mizigo; TAZARA iimarishwe ili ifikishe mizigo mpaka Makambako na Mbeya ambapo nchi jirani watakuja kuchukua cargo zao Makambako au Mbeya, tuta-fast track uchukuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale Tunduma malori yanatumia mpaka wiki kuvuka, suala hili linapunguza ufanisi, ndio maana Bandari kama Beira zinakuwa washindani wetu wakati hawastahili, hivyo maeneo yanayotupa mapato tuyalee, tuweke mageti hata Mbozi, suala kwamba transit cargo itarudi nchini, sio sawa labda kama hatuna nia njema kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fuel levy/vinasaba; kwa muda wa miezi karibu miwili TBS wanaifanya kazi hii, jambo hili ni jambo jema kuvijengea uwezo vyombo vyetu, hata hivyo katika wakati wa mpito yaani transition period naomba tuwe makini, EWURA wawezeshwe katika kufanya kaguzi kwa kupewa vifaa vya kukagulia ili tusipoteze fuel levy, as it is tunapoteza mamilioni kwa sababu mafuta ambayo ni transit yanabakizwa nchini, tunapoteza mapato, ushauri wangu Serikali ichukue hatua za haraka na kuthibitisha hilo Serikali ifanye mahesabu ya fuel levy ya mwezi Mei.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulinda viwanda vya ndani/ Kiwanda cha Pareto Mafinga; hiki ni kiwanda cha pili duniani na Tanzania ni ya pili kwa kuzalisha pareto baada ya Tasmania-Australia na kwa taarifa tu, pareto ni zaidi ya data ya kuulia wadudu kama inavyojulikana, bali ni final product ni component muhimu katika masuala ya military. Sasa Kiwanda cha Pareto Mafinga kimekuwa kikitoa mbegu na huduma za ughani kwa wakulima wa zao la pareto, lakini sasa ikifika wakati wa mavuno, wanatokea walanguzi wanaongeza bei kidogo wananunua maua ya pareto, kiwanda kinakosa malighafi, ajira zinakuwa hatarini kupotea, Serikali itakosa kodi na kadhalika. Ninaomba sana maelekezo yaliyotolewa na Serikali yawe kwa vitendo ili sio tu kulinda kiwanda hiki lakini pia kusimamia vitu kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mabenki ya Serikali TADB, TIB, TPB; ninaandika kama layman wa Banking Industry lakini kama mfuatiliaji wa masuala ya kitaifa, je, benki hizi zinapata faida? Kama hazipati faida ni kwa nini?

Nafahamu jitihada za kuunganisha benki ambazo zimeshaanza na tayari TIB Corporate na TPB, hata hivyo ninashauri benki hizi zote ziwe benki moja tu ambayo itajihusisha na kilimo/mifugo/uvuvi na uwekezaji, lakini lazima tukubali kuwa banking industry sio huduma, ni biashara, kama tunataka tupige hatua basi benki hizi zizae faida ili ikopeshe wengine, kwa nini zije benki kutoka nje zipate faida halafu sisi benki zetu Serikali zisipate faida, labda tuamue kuwa ni vyombo vya kutoa ruzuku.

Mwisho, je Benki ya Kilimo toka imeanza imekuwa na tija kwa kiasi gani? Vinginevyo tutalalamika mtaji mdogo, je, hata huo mtaji mdogo umeleta tija gani hata kama ni kidogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, tutazame mwenendo mzima wa hii benki, vinginevyo itakuwa political bank of agriculture, tuwe makini, huu ni uchumi though kila kitu ni siasa lakini uchumi usizidiwe na siasa. Naomba kuwasilisha.