Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. BERNADETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri, Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa hotuba ya bajeti iliyoandaliwa vizuri. Nina imani kubwa juu ya kuwezesha utekelezaji mzuri wa bajeti hii, kwani ninatambua uwezo mkubwa, uthubutu, unyenyekevu na uchapa kazi walionao Waziri na Naibu Waziri. Pia naipongeza sana Kamati ya Bajeti kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya. Bajeti hii ni nzuri, imegusa maeneo mengi ya kuleta maendeleo na imelenga kutatua changamoto nyingi za wananchi. Ni bajeti ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha, naomba kupendekeza yafuatayo; ulipwaji madeni ya wazabuni ya mwaka 2011 hadi 2016. Kuna wazabuni waliotoa huduma na vyakula kwenye shule za sekondari kati ya mwaka 2011 hadi kati ya 2016, hawakulipwa. Madeni yalihakikiwa, Hazina ikasema italipa. Wazabuni waliokwenda Hazina baadhi walilipwa. Baadae Serikali ilirudisha madeni haya kwenye Halmashauri. Halmashauri hazikuweza kuyalipa sababu vyanzo vikubwa vya mapato vilihamishiwa TRA. Hawa wazabuni wamesubiri, wengine sasa ni miaka kumi wanaidai Serikali, huduma walitoa, lakini Serikali haijawalipa. Madeni yamelala kwenye Halmashauri mbalimbali nchini. Wazabuni hawa wameumia, wamefilisiwa na benki wamefililisika. Naomba na kuiishauri Serikali kuu ilipe madeni haya. Miaka kumi jamani, waonee huruma. Waziri ukija kuhitimisha naomba jibu ni lini watalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoani Kagera wakulima, wastaafu, wajasiriamali, viikundi vya wanawake na SACCOS mbalimbali walikuwa wameweka fedha zao katika Benki ya Wakulima ya KFCB. Benki hii ilifungwa na Benki Kuu mwaka 2018. Watu waliokuwa wameweka fedha zao humo, hawana makosa lakini wanateseka sababu fedha hizi zilifungiwa humo. Mheshimiwa Waziri ni lini watu hawa watarudishiwa fedha zao?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuomba upendeleo maalum (preferential treatment) wa kisera, kisheria, kikanuni, kiutaratibu, kikodi ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Kagera. Mkoa wa Kagera uko takribani kilometa 1400 hadi 1500 kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Mkoa umezungukwa na nchi nyingi kama Rwanda, Burundi, Uganda, na Sudan Kusini na DRC zinafikika kirahisi kutoka Kagera. Nchi hizi zingeweza kuwa soko zuri sana kwa Mkoa wa Kagera, lakini kwa sababu wao wana sera nzuri zaidi za kuvutia wawekezaji na biashara, basi kwao wanafanya vizuri kuliko sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya bajeti hii inaonesha kuwa Mkoa wa Kagera una wawekezaji kwenye viwanda wachache sana. Gharama kubwa za usafiri zinachangia mkoa kukosa wawekezaji kwenye viwanda na biashara, inapunguza uwezo wa ushindani kwenye masoko. Gharama kubwa za usafirishaji wa wataalam, kufuatilia vibali mbalimbali na usafirishaji wa wataalam na usafirishaji wa bidhaa zilizozalishwa ili zifikie masoko makubwa yaliyo Dar es Salaam, gharama hizi ni kubwa, haziwavutii wawekezaji kwani zinaongeza gharama za uzalishaji. Mfano mfuko mmoja wa simenti unaununua kati ya shilingi 13,000 hadi 14,000 Dar es Salaam, ikifika Kagera mfuko huo huo unauzwa kati ya shilingi 22,000 na 25,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi zilizotuzunguka zina sera na utaratibu mzuri zaidi unaowavutia wawekezaji. Nchi jirani zimetambua gharama za usafirishaji kama Non-Tariff Barrier (NTBs), hivyo wameweka utaratibu wawekezaji wanawekewa viwango vidogo vya kikodi. Matokeo yake sasa tunashuhudia wawekezaji wengine wakihama kutoka Tanzania kuhamia nchi jirani. Hata wafanyabiashara Watanzania, wengine wamevutiwa na kuhamishia mitaji yao nchi za jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mipakani mfano Mtukula, Rusumo na kadhaika, biashara zinachangamka upande wa Uganda na Rwanda, upande wa Tanzania biashara zinadorora. Sera, sheria na kanuni zao zimerahisishwa sana kiasi wafanyabiashara wanashawishika kufungua biashara nyingi kwa kasi Uganda kuliko Tanzania. Hata baadhi ya Watanzania wanapeleka biashara zao nchi jirani mfano pale Mtukula.

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2019, Mkoa wa Kagera uliwasilisha ombi Serikalini wakiomba mkoa upewe Upendeleo maalum, wawekezaji Mkoa wa Kagera wapewe unafuu wa kikodi ili kufidia gharama kubwa za uzalishaji na uendeshaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitolewa upendeleo huu wa kisera, kisheria, kikanuni na kikodi mkoa utashindana sawa na nchi jirani, milango ya uwekezaji na biashara itakuwa imefunguliwa, wawekezaji wataongezeka, uzalishaji kwenye viwanda utaongezeka, biashara za mpakani upande wa Tanzania zitaongezeka, mzunguko wa uchumi katika Mkoa wa Kagera utaongezeka na mapato ya Serikali yataongezeka.

Mheshimiwa Waziri wa Fedha, ombi la kuupatia Mkoa wa Kagera upendeleo maalum (preferential) lililoletwa Serikalini tangu mwaka 2019 ili kuchochea uwekezaji wa viwanda na biashara Mkoani Kagera litatekelezwa lini? Naomba jibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.