Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii lakini nakuomba kidogo Mwenyezi Mungu akikujaalia basi uniongezee muda kidogo kwa sababu nina suala la kuisaidia Serikali yetu katika suala la mapato nakuomba sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa kuunga mkono hoja. Nazungumzia suala la uagizaji wa mafuta kwa pamoja. Hili suala la uagizaji wa mafuta kwa pamoja lilianza mwaka 2014 kwa ajili ya kupata zabuni ya kuagiza mafuta, kupata mzabuni atakayetuletea mafuta kwa pamoja. Shughuli hii imekwenda imefanyika kwa vizuri zaidi mpaka leo hii takribani mwaka wa saba, lakini yapo maeneo ambayo katika uagizaji huu wa mafuta tunakosa fursa ya kupata mapato katika eneo hili. Kwa nini nasema hivi, Mheshimiwa Waziri wa Fedha ni kwamba, katika eneo hili kuna suala la kupata nafuu ya bei katika uagizaji wa mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo nchi marafiki. Tuna nchi kama Saudi Arabia, Iran, Kuwait, Abu Dhabi, Bahrain, Dubai pamoja na Oman. Nchi hizi zote zina Mabalozi katika nchi hii. Kwa nini tusitumie uagizaji sasa wa tender yetu iwe ya nchi kwa nchi badala ya mtu wa kati? Huyu mtu wa kati anaweka faida yake hapa ndani, hili liangaliwe sana katika mfumo huu wa uagizaji. Tunaiomba sana Wizara ya Fedha pamoja na Wizara ya Nishati, wakae Makatibu Wakuu waanze kuangalia upya tathmini ya uagizaji wa pamoja je, nchi inapoteza kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi ni kwamba, fedha hizi za uagizaji ni kwamba, bei zao za watu wa OPEC wanatoa discount ya asilimia 30 katika uagizaji. Kwa nini tunapoteza kiasi hiki cha asilimia 30 wakati sisi ni maskini lakini wakati huo huo tuna shida na fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha katusikia Wabunge na Kamati ya Bajeti wametusikia Wabunge kwa kuweka shilingi mia moja. Hii shilingi mia moja iliyowekwa katika bei za mafuta, bei hizi za mafuta zinapanda na kushuka. Leo hii wananchi wanalalamikia jambo hili kwa sababu bei iko juu, lakini mwaka jana mwezi wa Nane bei ilikuwa chini shilingi 1,500 mpaka shilingi 1,600 kwa lita. Hii gap isingeonekana sasa hivi inaonekana hapa kwa sababu hiyo, lakini fedha hii shilingi 100 ina faida kubwa sana katika nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, haijawahi kutokea nchi hii toka imepata uhuru tumekuja kuweka jambo kubwa sana hili la kutengeneza barabara zetu katika Halmashauri zetu na vijiji. Kwa nini nasema, ni kwamba fedha za toll road ambazo zilikuwa zinakusanywa zinakwenda kwenye Mfuko wa barabara, ilikuwa ni shilingi 263. Katika shilingi 263 TARURA ilikuwa inapewa asilimia 30 na asilimia 30 ilikuwa ni shilingi
78.90. Sasa leo hii shilingi 78.90 ukiongezea shilingi 100 tunapata shilingi 178.90. Ni sawa sawa na makusanyo kwa siku bilioni 2,148,000 pigeni makofi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa aliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Samia Suluhu kwa jambo hili tunakuambia Mheshimiwa Rais, tunakwenda kutengeneza barabara zetu kwa kiwango kikubwa haijawahi kutokea tokea uhuru. Hongereni sana, hengereni sana kwa bajeti nzuri na wananchi wanakwenda kuiona faida yake. Nini ambacho kinapungua TARURA, kinachokwenda kupungua TARURA ni kwamba tunawapelekea fedha nyingi zaidi ya bilioni 770 tunakuja kupata kwa ajili ya kazi ya barabara za TARURA. Sasa, ninachoomba ni kutengeneza ring fence ya hizi fedha. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hizi fedha tunatakiwa tuzitengenezee ring fence zisitoke. Waheshimiwa Wabunge sijui mnanielewa ndani ya hili Bunge! Ni kwamba hizi fedha jamani lazima tutengeneze sheria kabla ya kuondoka hapa kuzi-fence hizi fedha zikawe na manufaa kwetu, zitakwenda kutumika katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukuambia hii fedha tunazokwenda kuzitengeneza kule shilingi bilioni 78 ni fedha nyingi sana. Tunakwenda kupata bilioni 770 za TARURA lakini pamoja na hali hii ni kwamba hapa kuna fedha zingine ambazo zinapotea. Hizi fedha za EPS hawa wanaweka stamp katika vinywaji, wanaweka stamp katika sigara, hawa wanachukua shilingi bilioni 94 wakati tunalo Shirika la Posta. Hili Shirika la Posta ndilo kazi hii ikafanye kama walivyoenda kufanya TBS. Posta ndiyo wenye kazi ya stamp katika nchi hii iweje aachiwe mtu binafsi akaweke stamp hizi, wakati Shirika la Posta linakwenda kufilisika na kufa? Tuliokoeni Shirika letu la Posta na hizi fedha bilioni 94 zikienda kule Posta, Posta itatoa gawio kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani ninachotaka kuwaambia hapa kuna fedha nyingine zinatumika Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Fedha zinazokwenda MaxMalipo tuna kitengo chetu sisi cha fedha za Serikali GPE. Kama GPE ni watu wa mfumo wa malipo kwa nini tunatumia MaxMalipo wanaondoka na mabilioni ya shilingi kila mwezi? Haiwezekani fedha Mheshimiwa Mwigulu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa Tabasam.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja nimalize jambo la muhimu sana hapa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Hapo nilishakupa mbili tayari umeongeza sekunde 30 malizia sentensi yako.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni hawa watu wa mfumo wa malipo ya Serikali. Tunao watoto tumesomesha wamesoma katika hivi vyuo, tunavyo vyuo vyetu sasa hivi tulivyonavyo katika nchi hii, kwa nini tusiwatumie tunakwenda kutumia MaxMalipo anaondoka na fedha nyingi? Haya, kule Posta kuna wafanyakazi ambao hawana kazi sasa hivi na stamp hizo zinatengenezwa na hawa watu wa Posta ndiyo wanatoa kibali kumpa EPS, tunaruhusu jambo hili liende EPS wakati kuna Posta inakwenda kufilisika isifanye kazi hii?

Naiomba sana Serikali, jamani tuweni wazalendo kwenye nchi yetu tumsaidie Mama tuvuke. Ahsanteni sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Tabasamu umeongea jambo la msingi sana hapo, hebu tusaidie hao MaxMalipo ni vijana pia wa Kitanzania au wao siyo Watanzania?

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, hawa MaxMalipo ni kampuni imekuja kutoka nje ikaja hapa, Watanzania wachache sana hapo. Mnabisha nini hayo maneno gani?

NAIBU SPIKA: Aah! ngoja Waheshimiwa Wabunge.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mimi ndiye ninaye muuliza Mheshimiwa Tabasam, vijana tumewasomesha wengi, nauliza hawa wa MaxMalipo ni Watanzania pia au siyo Watanzania?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, hajui.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hata kama watakuwa ni Watanzania ndiyo ninachotaka kuwaambieni.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, basi!

NAIBU SPIKA: Ongea na mimi usiongee na mtu mwingine.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Hata kama watakuwa ni Watanzania lakini si tunalo Shirika la Posta hili Shirika la Posta si liko pale lifanye kazi?

NAIBU SPIKA: Sasa, ngoja nilikuwa nataka kuinyoosha vizuri hoja yako. Kwa sababu, umesema hivi tumesomesha watoto wa Kitanzania, sasa nikafikiri labda MaxMalipo siyo Watanzania. Ahsante sana, Mheshimiwa Tabasamu. (Makofi)