Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Abdulaziz Mohamed Abood

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia bajeti ya mwaka 2021/2022. Natumia nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya. Nawapongeza Mawaziri wote, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu, kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Waziri wa Fedha na Naibu wake kwa bajeti nzuri sana. Naunga mkono bajeti kwa asilimia 101. Ila hii moja naitoa kwa sababu katika kusoma bajeti yake, hakuitaja Simba, kaitaja Yanga peke yake. Kwa hiyo naibakisha asilimia 100.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite kwenye Sera ya Viwanda. Tanzania tupo kwenye Sera ya Viwanda. Ili tuwe na viwanda vingi ambavyo vinamilikiwa na wazawa wenyewe, lazima tuwe na investment banks. Tanzania hatuna investment banks, tunayo moja tu ambayo ina mtaji mdogo. Lazima tuwe na investment banks zenye mitaji mikubwa ambazo zinaweza zikakopesha na wananchi wakaweza kufungua viwanda vikubwa vitakavyotoa ajira nyingi kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukichukulia kwa mfano TIB, tuna benki moja tu Tanzania na mtaji wake ni mdogo. Ukichukua majirani zetu Wakenya, wana investment banks karibu kumi na riba yao iko chini, 4%. Sisi hapa Tanzania riba yetu ni kuanzia asilimia 12 mpaka 18. Kwa hiyo ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba tujitahidi; na hasa hizi pension funds zote tungezifanya pia investment banks ili ziweze kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wawekezaji wazawa wa Tanzania na mikopo mikubwa ili kuwekeza katika viwanda na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye viwanda vya kilimo bado tuko nyuma sana, tunahitaji lazima tuwekeze kwenye viwanda hivi. Viwanda hivi vinategemea sana wakulima. Sasa jinsi ya kuwakopesha wakulima nayo vilevile Serikali iangalie. Kwa sababu ukitazama wakulima wa nchi mbalimbali duniani, huwa wanakopeshwa kwa riba ndogo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukichukua Malaysia ambao ni wakulima wakubwa wa mawese; minimum mkulima anakopeshwa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kilimo cha mawese kwa miaka kumi. Hapa Tanzania agro-processing inahitaji tuwe na sera ya muda mrefu, siyo ya mwaka kwa mwaka, ili wakulima wajitayarishe; na wenye viwanda wanaokopa wawe na sera ya muda mrefu ya kuweza kuzalisha mazao haya, kama ni mafuta ya kula, kama ni nini, ili kama anakopa anaweza akarudisha mkopo wake kwa muda wa miaka kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala lilishawahi kutokea mwaka 2004. Wakulima walilima sana alizeti, baada ya kodi ya mafuta kupanda. Baada ya mwaka mmoja kodi ikaondolewa, wakulima wakazima. Kwa hiyo, mimi naomba sera iwe ya muda mrefu, siyo ya mwaka kwa mwaka ili viwanda hivi vya agro-processing viweze kujipanga kwenye kilimo kwa muda mrefu na wakikopa wajue kabisa kwa miaka kumi, sera haitabadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, linguine ni kuhusu pesa za wahisani zinazokwenda kwenye miradi mikubwa. Pesa hizi naishauri Wizara ya Fedha kwa kumtumia Msajili wa Hazina, wafuatilie. Kwa mfano, Morogoro, tumepata Euro milioni 70 kwa ajili ya mradi wa maji, ambayo ni sawasawa na shilingi bilioni 180, lakini Wizara ya Maji mpaka leo hatujui kama hizo pesa zimefika na Morogoro mradi hakuna. Sasa tunataka tujue, hizo pesa ziko wapi ili mradi wa maji uanze? Sasa Hazina nayo itusaidie kutupa majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri amekuja kule, ametumbua tumbua, hatujui pesa ziko wapi? Kwa hiyo, naishauri Serikali kwa kumtumia Msajili wa Hazina, miradi mikubwa kama hii ingekuwa inafuatiliwa ili tuwe tunapata majibu ya haraka kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme tu,…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, naona muda wangu umekwisha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa Abdul-Aziz Abood.

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. (Makofi)