Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ally Anyigulile Jumbe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kyela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ALLY A. J. MLAGHILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 30 machi, nilimuandikia message ndugu yangu Mwigulu Nchemba nikimuombea kwamba ikitokea baada ya kuchukuliwa Mheshimwa Mpango kuwa Makamu Rais basi nikasema naomba Mheshimiwa Rais ikimpendeza uwe Waziri wa Fedha; na bahati nzuri yale maombi yalitokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilifanya hivyo kumuombea kwa sababu nilijua uwezo wake na nilijua uzalendo wake alionao kwa nchi hii ya Tanzania. Sasa tumeshakupata Mwigulu Nchemba na baada ya kukupata tumeshaanza kuona matunda yako pamoja na ya Naibu Waziri wako. Matunda haya hayajajificha, tumeanza kuyapata kwa kuyashika mkononi. Katika hili naomba nimshukuru sana Mama yetu, Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Ingekuwa tupo mtaani ningesema ameupiga mwingi kukupata wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaona matunda ya kupata shilingi milioni 500. Kwa jimbo langu mimi Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa pesa hiyo tunakwenda kujenga kilometa 2.5 za lami mjini. Hii itakuwa ni alama kubwa sana ya kazi kubwa uliyoanza nayo kuifanya. Maana yake ni nini? Kama naweza kujenga kwa milioni 500 kilometa 2.5 kwa kujiongeza ninaomba niiongezee shilingi zingine milioni 500 niende vijijini nikapige kazi ya mara mbili ya hiyo pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninaomba niseme, sifa zangu zitakuwa nyingi sana baada ya kuona matunda mengine yajayo, hasa kwenye eneo la jinsi utakavyogawanya hizi pesa zilizopo kwenye bajeti. Huko nyuma tumekuwa tukiona wakati mwingine sehemu nyingine hazifikiwi ilhali ni sehemu muhimu.

Ninaomba kama ni ma-flyover basi hata Tunduru kule, hata Iringa wayaone, siyo Dar es Salaam tu. Kama ni flyover pale Mbeya napo nani amewaambia hai-fit? Inakaa vizuri, tena inapendeza; ninaomba twende huko. Lakini hebu tupeleke akili sehemu zote za Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza watu ambao wanastahili kupata hata ile reli ya SGR TAZARA inastahili ifike hapo, tusirudi tu huku kwenye mpya, tukitengeza TAZARA, nataka nikuhakikishie, uchumi wetu utapanda zaidi ya ulivyo sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunapotoa hizi rasilimali Mheshimiwa Mwigulu, wakati mwingine inasikitisha. Kyela ni sehemu ambayo inapata magonjwa mengi kwa sababu ya jiografia yake. Hata hivyo tangu mwaka jana hospitali imeungua wodi zimeungua pesa leo ndiyo zinapelekwa milioni 500 tu ilhali tuliomba na kwenye bajeti ilitengwa 1.3 billion, lakini sehemu zingine utakuta pesa zimeenda na wala hawakuunguliwa. Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri, hebu iangalieni Kyela kwa jicho tofauti na sehemu zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ile ndiyo inayopokea masalia yote ya maji yanayotoka milimani, Ileje, Rungwe na Busekelo. Sasa miundombinu yake yote imeharibika kiasi kwamba hata kupeleka wagonjwa hospitalini ni ngumu, watu wanakufa vijijini kwa sababu hawawezi kufika haraka sehemu za kutolea huduma za afya. Kwa hiyo ningeomba hili tuliangalie si kwa Kyela tu lakini kwa Tanzania nzima. Twende tuangalie maeneo ambayo yapo prone namna hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la takwimu. Katika kitu muhimu kuliko vyote kwenye uchumi ni takwimu sahihi. Leo kwenye bajeti tumetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wananchi wa Tanzania, lakini hivi tunahitaji kutenga hizo fedha? Mimi kwa mawazo yangu, nilitaka nishauri kwamba inawezekana hatukuwa na haja hiyo iwapo tungetumia vizuri sana rasilimali watu tulionayo; na nina uhakika wala tusingekuwa tunakisia idadi ya Watanzania, tungekuwa tunasema kwa uhuru tena kwa uhakika; kwamba leo hii tumeamka asubuhi tupo na watu kiasi fulani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusiwatumie hata mabalozi kwamba watoe taarifa za kila siku watu wapo wangapi hapo kwake Inawezekana ikaenda kwa mwenyekiti wa kitongoji tukatengeneza system nzuri ya mtandao. Tunaweza tukawa na computer zikaa pale kila siku au hata kwa wiki zikawa zinatolewa taarifa za idadi ya watu waliopo hapo. Mimi nafikiri kiasi hiki kisingefikiwa tungefanyia kazi nyingine. Ninaomba sana hebu twende tuangalie takwimu zetu za kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za Ulaya zimefanikiwa sana. Hakuna mtu anayelala nchini au kwenye nyumba ya mtu asijulikane yupo hapo na ameingia lini na anaondoka lini; na hata kwa usalama wa nchi itatusaidia sana. Zamani ilifanikiwa sana, hata kwa mabalozi, balozi alikuwa anajua ni nani ameingia kwenye eneo hilo na anatoa taarifa kwa nini haya tumeyaacha. Hivi, vyama vingi ndivyo vinatakiwa kuondoa hayo? Mimi ningeomba turudi huko tufanye mambo makubwa nchi yetu ipo kwenye eneo zuri na inaenda kuzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kwenye mapato ya simu. Tumesema sana na Serikali inategemea kupata kama 1.2 trillion kutoka kweney simu. Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri, hebu kaa na watoa huduma wa simu wakuhakikishie uwezekano wa kupata kiasi hiki. Kwa sababu kuna sehemu kuna kuwa kama inaonekana haiwezekani ikapatikana hii. Sasa ili kuweka vizuri mimi nikuombe hebu fanya utafiti zaidi ili pesa hiyo ipatikane. Maana katika utafiti wangu nimegundua kwenye GSM na kwenye M-Pesa au Tigo Pesa pato lote la wao ni takriban bilioni 700. Sasa je, sisi tunaendaje hapo juu? Mimi ningeomba Mheshimiwa Waziri lifuatilie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la polisi. Tunahitaji kuwatunza sana polisi. Kuna sehemu tunasahau kuwasemea, na bahati nzuri Mheshimiwa Mwigulu na Mheshimiwa Masauni wote mmepita huko. Ninawaomba nendeni mkawaboreshee mafao hawa, hawa jamaa ndugu zetu wanalala nje kila siku na tunawategemea sana.

Naomba sana polisi tuwaangalie kwa jicho linguine. Lakini pia ningeomba nikutafutie chanzo kingine ambacho kinaweza kikawa ni privilege, lakini pia inaweza ikaonyesha uzalendo hata kwa Wabunge hapa hapa. Hebu tengeneza plate number za Wabunge halafu wawe wanalipia kidogo kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, plate number za Wabunge tu zinaweza zikalipa. Hebu angalia hata huko kwenye Serikali sehemu ambazo tunaweza tukatafuta, zikawa na Karangi kazuri kabendera yetu, tukawa tunalipia kwa mwezi au kwa mwaka itakwa vizuri zaidi na tutaongeza mapato. Unapokuwa Dodoma huwezi kupeperusha bendera, lakini ili ujulikane huyu ni Mbunge usijifiche ile plate number inaweza ikakusaidia, lakini iende kwa uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba kusema nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ninawaombe tu viongozi wetu wote wa Tanzania waendelee kumuenzi Mungu na waendelee kumkumbuka Mungu, kwamba tupo hapa kwa sababu Mungu ameichagua Tanzania kuwa Paradiso yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)