Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa wasaa huu niweze kuchangia bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza kabisa pamoja na ushauri wa mambo mengi nitakao shauri hapa niunge kabisa mkono bajeti hii ni nzuri na Mheshimiwa Waziri wa Fedha hongera sana. Lakini tumpe hongera sana mama yetu Samia Suluhu kwa sababu ndiyo Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hongereni sana kwa kuja na bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini masikitiko yangu kidogo tu kabla sijaanza kuchangia Waheshimiwa Wabunge tunaposema tunachangia bajeti ya Serikali bajeti kuu nilitegemea Mawaziri wote wawepo humu ndani. Hapa nawaona Mawaziri watano na kwa sababu nawaona Mawaziri watano, nitachangia kwenye hoja zangu kutokana na Mawaziri ninaowaona kwa sababu lazima wanisikie na wasikie ushauri wangu huwezi kuwa unachangia sehemu ambayo Waziri hayupo halafu inakuwaje. Bajeti Kuu ya Serikali siyo kwa ajili ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu peke yake Bajeti Kuu ya Serikali ni bajeti kuu yote pamoja na Mawaziri wote. Kwa hiyo nilikuwa nataka kwanza kutoa hiyo scenario tunaomba Mawaziri wawepo Bungeni…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo subiri kidogo nitoe ufafanuzi Waheshimiwa Wabunge nimeshasema mara kadhaa humu ndani leo nitazungumza kwa kifupi Serikali iko Bungeni.

Kwa hiyo, msiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mlugo kama huwaoni hapa ni kama vile ambavyo viti vingine vya Wabunge vipo huko nje vikizungumza na hawa Waheshimiwa Mawaziri kwa hiyo lazima wawasikilize Wabunge lazima kazi zote zifanyike kwa pamoja. Na wakati huo huo hii bajeti tunayojaribu kuijadili hapa Wabunge mmeshatoa mawazo mengi ambayo mengine yanatakiwa kuanza utekelezaji mara moja hayo yote lazima Serikali ikayafanyie kazi.

Mheshimiwa NaibU Spika, kwa hiyo, usiwe na wasiwasi Mheshimiwa Mulugo changia hata zile Wizara ambazo unaona Waziri hayupo hapa kwa sababu Serikali ipo ndiyo maana wewe unazungumza na mimi ujumbe kwangu wataupata usiwe na wasiwasi wowote Mheshimiwa Mulugo.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, unilindie dakika zangu, nianze na Wizara ya Madini Mheshimiwa nchi hii ingekuwa na fedha nyingi sana nchi hii kwa jinsi unavyoiona hata Mheshimiwa marehemu Mhe. Dkt. Magufuli alikuwa akisema Mungu amlaze mahali pema peponi. Lakini ni kutokana na watumishi wetu wa Serikali wanakuwa ni legelege katika kufanya mambo mengine ambayo unaona kabisa fedha zile pale unaziona.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano mmoja kwenye jimbo langu kule kwangu kuna sehemu kunaitwa Ngwala toka mwaka 2010 kuna kampuni inaitwa Heritage Tanzania imefanya utafiti wa madini, madini adimu duniani yanaitwa rare earth madini hayo kama yangeazwa kuchimbwa Serikali ingeweza kukusanya kodi nyingi sana zaidi ya bilioni 25 Serikali ingepewa kodi mwaka mmoja. Zaidi ya bilioni 83 zinakwenda kwenye gharama za uendeshaji, zaidi ya bilioni 7 mrahaba wa Serikali na mambo mengine ajira peke yake karibuni watu 1300 kule kwangu wangepata ajira na nchi nzima kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini toka mwaka 2010 wanazungushwa kupata leseni special mining nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Biteko nakuomba kwa unyenyekevu mkubwa wapatieni leseni hawa Ngwala Peak Resource waweze kuchimba madini hayo ni madini ambayo hayapo Tanzania hii, hayapo Afrika hii yapo kule Songwe na Mheshimiwa Waziri unajua nilikuwa nakuomba ikiwezekana mwezi wa saba usiishe uwape leseni wale watu wanataka kukata tamaa wanataka kuondoka nchini kama walivyoondoka watu wengine ambao walikuwa pale Mbangala wameondoka mafuta yamepatikana pale ukingoni mwa Ziwa Rukwa wamefanya utafiti Serikali imekuja imesema hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mlikuwa mnafanya utafiti wa gesi mmepata mafuta mmepata na gesi lakini kabla hamjapata mafuta wamekutana na madini ya helium. Baada ya hapo TPDC wamekuja wamesema hapana tufanye pamoja wameshindwa wamekasirika wameondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, inauma sana. upande mwingine ambao ningeweza kuishauri Serikali naomba nirudi kwenye Wizara…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dotto Biteko Waziri wa Madini.

T A A R I F A

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa tu taarifa ndogo kwa Mheshimiwa Mulugo najua anachangia kwa hisia kubwa na angetamani uwekezaji ule utokee naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba Kampuni ya PLG itapatiwa leseni ya uchimbaji mkubwa kwa mujibu wa sheria na tuko kwenye taratibu za mwisho za kuwapatia leseni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili kuhusiana na utafiti wa mafuta pamoja na gesi ya helium naomba kumpa taarifa vilevile kwamba kampuni ya helium one tayari imeshapewa leseni ya kufanya utafiti kwenye eneo hilo na taratibu zinaendelea.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana; Mheshimiwa Mulugo unapokea taarifa hiyo?

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepata furaha ya ajabu sana hawa ndiyo Mawaziri wanaotakiwa katika nchi hii nimefarijika sana na huo ndiyo unapelekea kwamba kweli mimi naongea ubunge. Ubunge lazima uongee halafu Waziri a take reaction ndiyo maana nilikuwa nimekwambia mara ya kwanza kwamba kuna Mawaziri ukiongea wanakuwa hawapo nilishawahi kuongea mwaka juzi kuhusu…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo ngoja ngoja tuelewane vizuri Waheshimiwa Wabunge nimesema hivi Serikali iko Bungeni na Waziri hapa angeweza kunyamaza wala siyo kazi yake yeye kutoa taarifa angeweza kuja kuchangia na yeye kama Mbunge mwingine na ndiyo maana Wabunge wengine ambao pengine Waziri hajasimama kujibu kwenye hoja yako haimaanishi wewe hujachangia sawasawa ama hajakusikia.

Nadhani tuelewane vizuri hilo Mheshimiwa Mulugo wewe ulikuwa Serikalini unajua zaidi mambo haya kuliko watu wengine ambao hawajawahi kuwa Serikalini. Mheshimiwa Mulugo malizia mchango wako.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba dakika zangu zilindwe nimalizie mchango wangu kwa amani. Nije upande wa elimu, ni mwalimu na declare interest kwamba nilikuwa Serikalini kweli kwa kutumikia Wizara ya Elimu kama Naibu Waziri, lakini vilevile nina shule binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo jambo lazima tulichangie lakini na dada yangu Mheshimiwa Prof. Ndalichako pale unanifahamu wewe ni rafiki yangu tunaongea mengi na ninakushauri mengi naomba ushauri huu uupokee vizuri. Wakati Mheshimiwa Rweikiza akichangia jambo moja hapa ulisimama ukatoa na mwongozo lakini binafsi sijakuelewa Mheshimiwa Waziri naomba nikushauri kama mwalimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema darasa la mitihani darasa la nne, darasa la saba, form two, form four, form six kwa mwaka husika hakuna popote duniani ambapo madarasa hayo yanaweza yakawa hayana mkakati wa kufaulu mitihani hakuna na wote hapa Wabunge tumetoka kusoma wote tumetoka form four huko tumetoka form six tulikuwa darasa la saba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa darasa la saba mwaka sijui tisini na ngapi huko lakini Mheshimiwa Waziri nilikuwa nasomea koroboi mpaka nikafaulu mitihani ni mkakati wa kusoma usiku zinaitwa prepo hata mchana sasa watu wameanzisha June program shule zimeanzisha June program na mfano mzuri ni kwa Mheshimiwa Mtaka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na mpaka Mheshimiwa Rais alikuwa anamsifia namna alivyoanzisha academic June program wakati wa likizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii Mheshimiwa Waziri unasema kwamba hapana watoto warudi nyumbani, darasa la saba mtoto yule akirudi nyumbani saa hizi na mtihani wa Taifa ni mwezi wa tisa watafeli mitihani ndiyo maana Watoto wanafeli lakini sababu ni viongozi nyie mnakataza zile program. Angalia shule binafsi wanavyofanya Watoto wanasoma usiku, wanasoma March program, wanasoma June program, wanasoma September program. Madarasa ya mitihani lazima yawekewe program check it walimu kwenye shule za Serikali tunakosa walimu wa mathematics, tunakosa walimu wa physics tunakosa walimu wa chemistry wakati shule zimefunga, tunasema darasa la sita walimu kwa sababu watoto wameenda nyumbani wale walimu wanaofundisha darasa la sita masomo ya sayansi waweze kuwasaidia kaka zao pale walimu wanajitolea wazazi wameamua kwa pamoja wamelipa fedha ya chakula wamelipa fedha ya malazi, wamelipa fedha za stationary wameamua wenyewe watoto wao wabaki shuleni waweze kujisomea kwa ajili ya mitihani…

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa!

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cosato David Chumi.

T A A R I F A

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mulugo kwamba mimi pale Mafinga shule ya Changarawe haijawahi kuwa na mwalimu wa physics. Kwa hiyo, Juni hii tunachukua walimu kutoka Mafinga Seminary ili waje pale watusaidia kuwa-brush wale Watoto naomba kumpa taarifa. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mulugo unapokea taarifa hiyo?

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa miguu miwili na mikono miwili, naongea jambo ambalo mimi naishi huko niko kwenye field mimi ni mwalimu nafundisha economics Form V na VI wakati wa mitihani lazima tuwawekee wanafunzi program, na wewe ulikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale ndivyo ilivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri leo naomba nikatae kabisa program zako eti watoto darasa la saba leo warudishwe nyumbani wakienda kule watakuwa wanatumwa sokoni, watakuwa wanacheza cheza acheni wakae shuleni wasome ni jambo zuri naomba sometime Serikali muwe mnasikia mawazo ya wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine la mwisho kipo kitu lazima tukifanye kwenye elimu kinaitwa PPP, naomba nitoe takwimu ambayo ukiyapata hayo unaweza ukaona nini naongea mwaka kesho Serikali itashindwa kuwapeleka watoto form one kwenye shule za Serikali kwa sababu gani. Mpango wa elimu bure ulianza miaka sita iliyopita watoto waliopo leo darasa la sita wako takribani 1,800,000 wanakwenda wapi? Serikali ina uwezo wa kuchukua kwenye darasa yao na madawati Watoto 750,000 tu kwa hiyo ni asilimia kama 100 kwa mwaka kesho lazima Serikali ijenge shule zaidi ya hizi zilizopo shule za Serikali sijui kama tutaweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Rais ametoa shule moja moja kila Jimbo lakini bado tuko moja ya mia moja. Serikali naomba ije na mpango wa PPP shule za private zina madarasa, zina madawati zina walimu lakini zinakosa wanafunzi. Nchi ni yetu wote watoto ni wetu wote twendeni tukakae pamoja watu wa shule za binafsi tukae na Serikali tuone namna gani watoto hawa wengine waanze kwenda kwenye shule za private wakajaze madarasa huko halafu Serikali ianze kuwalipa mishahara kule mbona ni kitu kile kile kama ambavyo mlifanya kwenye afya ni jambo jema mno naiomba sana Serikali isikilizage ushauri huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nasema naunga mkono hoja lakini naomba mawazo yangu yachukuliwe na Waziri wa Elimu ahsante sana. (Makofi)