Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon Salim Mussa Omar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gando

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuchangia machache katika Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu wa Azza wa Jalla, kwa kutukutanisha leo hapa tukiwa wazima na tukiwa na akili timamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nakishukuru chama changu cha Mapinduzi kwa kuniamini na kuniteua na leo ni Mbunge wa Jimbo la Gando ndani ya Bunge hili Tukufu. Kipekee nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawashukuru wananchi wa Jimbo la Gando walionichagua kwa kishindo kunileta katika mjengo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua tu fursa hii kuwaambia kwamba sitawaangusha na kama ilivyo sasa hivi mambo yanarindima, Suluhu Cup inaendelea Jimbo la Gando, karibuni sana. Mimi nina mambo matatu ambayo nataka nichangie katika hotuba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kama walivyotangulia Wabunge wengi ndani ya Bunge hili kumshauri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Wizara yake kuhusiana na Bureau De Change; mimi ni Mbunge kutokea Pemba. Wafanyabiashara wengi waliopo Dar es Salaam ni wapiga kura wetu au ni ahali, au ni ndugu wa wapiga kura wetu. Sasa nisipolizungumza suala hili, kidogo nitakuwa sijawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kutokea Pemba tumejikita sana kwenye biashara. Unapofunga moja kati ya component za biashara, unatuua kiuchumi. Unapoweka kizingiti katika biashara kama ya Bureau De Change unaua kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hainiingii akilini mwangu hata kidogo kuwekwa kwa shilingi milioni 300 mtaji wa kufungua Bureau De Change. Binafsi kama Salim, naiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha iliangalie tena jambo hili…(Makofi)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Omar Salim kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jesca Msambatavangu.

T A A R I F A

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji. Capital requirement ya kuanzisha bureau kwa mujibu wa regulation ya 2019 ni shilingi bilioni moja na siyo milioni 300 kama alivyosema. Hiyo ilifutwa. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Omar Salim, unaipokea taarifa hiyo.

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, hicho ni kichakaa. Kule kwetu tunaita kichakaa, yaani balaa. Hilo ni balaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi, mpaka namaliza Chuo Kikuu pale UCC kuchukua Diploma yangu ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano sikuwahi kufikiria kuajiriwa na Serikali; na huu Ubunge haikuwa ndogo yangu kabla, umekuja tu kwa sababu nilihisi ninao uwezo wa kuwasemea wananchi wa Gando Bungeni baada ya kumaliza chuo. Nilikuwa nategemea sana kujiajiri, lakini sasa kama kutakuwa kuna vingiziti kama hivyo, sidhani kama wale ambao hawajabahatika kuwa Wabunge kama Salim watakuwa na uwezo wa kujiajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lipo serious ndani ya Dar es Salaam. Mimi binafsi nilikuwa na rafiki zangu ambao waliokuwa na Bureau De Change wanafika hata 125 kwa ambao ninawafahamu, leo hii wamekaa dormant. Sio hao tu, hata wale ambao walikuwa ni wafanyakazi wao, wamerudi Pemba wengine na ndio hao wanaoshika mabango kuitukana Serikali pale wanapoambiwa waandamane na wale watu ambao hawaitakii mema Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke huko nielekee katika dirisha la kupeleka claims kwenye masuala ya business dispute. Narudia tena kama nilivyoungumza siku ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Wako vijana ambao wamepewa nafasi kubwa, nami leo ni-declare interest, nilikuwa ni mfanyabiashara na ni mmiliki wa Kampuni kubwa ndani ya Taifa hili katika wamiliki wa kampuni hiyo (shareholder). Unafanya kazi na Serikali lakini mwisho wa siku anatokea mtu, kwa sababu tu ya cheo chake na nafasi yake, anatengeneza mazingira ya kuwakwamisha bila kujali kama akikuangusha wewe…; na inawezekana tu ana personal conflicts na mmoja wa director katika Kampuni, anatengeneza namna ya kuizuia kampuni hiyo kutokuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni hii inawezekana ina wafanyakazi zaidi ya 300; ni familia 300 hizo ambazo ni nyingi katika Taifa letu hili; lakini anatengeneza mazingira, anaikwamisha, inashindwa kufanya progress zake za utendaji na mwisho wa siku kampuni ile ina-collapse na inaanguka. Sijui sasa anamlaani nani? Mwisho wa siku ukiwa unamiliki kampuni kama hii na mtu anakutengenezea mazingira kama hayo kwa sababu ya nafasi yake kubwa, unashindwa kuamua: Je, umshitaki au uende wapi? Maana yake unaenda kumshaki sehemu ambayo wewe ndipo unapatia riziki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mimi nafanya kazi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Kampuni yangu. Akinitengenezea mtu mazingira, nashindwa kulishtaki Bunge kwa sababu nafikiria kesho itakuweje? Inawezekana lile tatizo likatatuliwa lakini kwa sababu nililipeleka Mahakamani Bunge lako, litashindwa kuweza kuniamini kwamba labda nitakuwa sina imani nalo. Kwa hiyo, unakuta makampuni yanafanya kazi na baadhi ya taasisi za Serikali, lakini mkandarasi yule anashindwa kwenda Mahakamani kuishtaki taasisi ya Serikali na mwisho wa siku anajikuta anarudi mtaani.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri atutengenezee dawati la Claim la chini kwa chini…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Salim, unaweza kusimama kawaida, bado utasikika. Maana mpaka ukimaliza kuchangia unaweza ukawa unaumwa mgongo. Kwa hiyo, utaweza kuchangia ukiwa umesimama na bado utasikika. (Kicheko)

MHE. SALIM MUSSA OMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, usijali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri Mheshimiwa Waziri atutengenezee dirisha la kutusikiliza chini kwa chini kwanza. Kuna baadhi ya Kampuni zinaonewa na hili liko wazi. Ukweli tuuseme. Hata mimi ndani ya Chama changu cha Mapinduzi niliapa kwamba nitasema ukweli daima, fitina kwangu mwiko. Sasa kama niliapa hivyo na nimeapa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni lazima ukweli tuuseme. A spade, call it a spade, not a big spoon. Pauro libaki kuitwa pauro, tusiliite kijiko kikubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kutakuwa na window ya kupeleka claims zetu ndani ya Wizara ya Fedha, basi itatusaidia wafanyabiashara wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoke hapo, niseme tu, maana yake imefikia mahali mfanyabiashara anatega teuzi zinazokuja za Rais atachaguliwa Waziri gani? Je, namjua? Sasa ole wako achaguliwe mtu ambaye alikupigia simu hujapokea. Unaanza kufikiria, eeh, nirudishe tena ile missed call yake ya jana. Yaani tunaenda katika mazingira ya kumtegemea mtu kwa sababu ya nafasi yake sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui nafahamika! Yaani akiteuliwa mtu, unafikiria huyu nitamfikiaje? Hakuna ule mfumo uliowekwa kwamba hapa mimi nitafanya biashara zangu na nitakuwa salama na sitoathiriwa na awamu itakayokuja. Hili lipo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na crew yako tafadhalini sana tuokoeni kwenye hili, mambo ni mengi na wafanyabiashara tunaumia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema pia nichangie katika suala la special number/plate number. Ni kweli, nakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na crew yako kwa kupunguza kiwango kile cha shilingi milioni 10 mpaka kikaja kuwa milioni tano. Bado tunaomba hebu tupunguzieni kidogo hadi ifikie shilingi milioni tatu. Vijana wengi wataweka majina yao ndani ya plate number, itatusaidia kuweza kufanya accumulation ya hizo fedha nyingi sana watakazolipa na pia itasaidia katika vyombo vya usalama kuweza kugundua kwa haraka zaidi pale ambapo tunamtafuta mtu ambaye ana gari ambalo limeandikwa jina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nielekee katika kuchangia kidogo kwenye masuala ya utalii. Next year, inshallah tutakapofika hapa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na crew yako pamoja na Waziri wa Utalii hebu tutengenezeeni kifungu cha kutafuta fedha kwa namna ya kuwekeza katika digital tourism. Tuwe na fedha ambazo zitatuwezesha kumpata mkandarasi duniani atuwekee digital tourism ambayo itaweza ku-display hata katika slogans za kule kwenye airport. Mfano Dubai pale, tuweze kuona swala wetu wa Tanzania, Mlima Kilimanjaro, popo wetu wa Pemba ambao hawawezi kupatikana sehemu yeyote duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vivutio vya Utalii ambavyo haviwezi kuonekana sehemu nyingine yoyote isipokuwa Zanzibar au Tanzania Bara. Tunao Kima Punju, tuweze kuwa na display kule katika airport; watu wanaposubiri ku-connect ndege kutoka sehemu moja kwenda nyingine waweze kuona Zanzibar kuna nini? Tanzania Bara kuna nini? Tuweze kuongeza wigo mpana wa kupata watalii na kupata fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache niliyochangia, naomba niunge mkono hoja, niwaombee kila la heri Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wote, Ishallah tutafika. Ahsante sana. (Makofi)