Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nimshukuru Mungu sana kwa kutupa uhai ili leo tuweze kuzungumza machache kuhusu Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwape pole sana vijana wa timu ya Mwadui kwa namna walivyoonewa jana na lile goli la offside, kwa kweli lile goli halikuwa goli, Yanga walibebwa sana, lakini Insha Allah tutawalipia tarehe 3 Mungu akipenda. Vijana wasilie, wanyamaze tutawalipia tarehe 3. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba pamoja na Engineer Masauni Masauni kukaa kwenye Hazina Kuu ya Nchi kwenye Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kitendo cha kuaminiwa tu na Mheshimiwa Rais, nasi hatuna mashaka na uelewa na uchapakazi wa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Eng. Masauni, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha pamoja na watendaji wengine wote. Mimi ni miongoni mwa Wabunge wanaotoka kwenye familia masikini. Kitendo alichokifanya Mheshimiwa Rais cha kutupa Shule ya Sekondari kila jimbo, cha kutupa shilingi milioni 500 kila Jimbo, kimetugusa masikini wengi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amegusa nyoyo za watu masikini wa nchi hii kwa sababu maeneo anayoyagusa ni yale yatakayoinua sana uwezo wa watu masikini wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Shule moja ya Sekondari itazalisha watoto wengi sana kwenda kwenye ufaulu wa kati na kwenda kwenye kujitegemea na kupata ajira. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais amepanda mbegu njema kwenye mioyo yetu, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine watasema tuna Shule za Sekondari kila Kata; kweli, chukulia mfano katika Kata yangu ya Mvumi Mission, watoto waliopo Darasa la Saba mwaka huu ambao ndio wanategemewa kwenda Kidato cha Kwanza mwakani wapo 450. Utawapeleka shule gani hata kama una shule? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kitendo cha Rais kutupa tu shule moja hii, popote tutakapoiweka itasaidia sana wakazi wa Jimbo la Mvumi kuweza kupata elimu bora na kuendelea, lakini watu hawajaelewa sawa sawa, hii shilingi milioni 500 ilizungumzwa vizuri sana na Mheshimiwa Mama Kilango pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine. Mwaka 2020 tulipata mvua nyingi sana. Mmvua zile ziliharibu sana barabara za vijijini. Sasa Mheshimiwa Rais kuliona hili na kutupatia hii fedha, sisi hatusemi kidogo. Asiyeshukuru kwa kidogo hata kwa kikubwa hawezi kushukuru. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa tendo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tu wenzetu wa TARURA, zikatengenezwe barabara za kiwango cha Mheshimiwa Mama Samia. Tumemwona, mama hacheki katika mambo mabaya. Likitokea jambo ambalo halimfurahishi, hapo hapo anakula kichwa cha mtu. Kwa hiyo, tusije tukaanza kushuhudia maumivu. Tusifikiri ametoa tu kama zawadi, atataka baadaye aone kazi iliyofanywa kutokana na fedha hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tuishauri Serikali kuendelea kutanua wigo wa walipa kodi. Hili jambo ni jema sana. Unajua tunawezaje kuwapata walipa kodi wapya? Kama tutaboresha kilimo chetu kwa nchi nzima, tutatengeneza wakulima wa chini kupanda kuwa wakulima wa kati na hivyo kilimo chao kuwa kilimo cha biashara. Hapo tutapata walipa kodi wapya tusiendelee na wale wale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine jipya, tumekuwa tukishauri sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Dodoma tukitengeneza bandari kavu hapa tutapunguza mafoleni yote kuelekea Dar es Salaam, mizigo mingi inayokwenda kanda ya ziwa inayokwenda nchi za Kongo, Burundi na Rwanda itatokea Dodoma badala ya kutokea Dar es Salaam. Kwa hiyo, tunashauri tu kwamba mkitengeneza bandari kavu hapa Dodoma, mtarahisisha sana uchumi wa hapa Dodoma pamoja na Kanda nzima ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali kwa kupunguza kodi ya pikipiki, lakini kuja jambo wamelisahau pale. Siyo pikipiki pekee inayobeba abiria mmoja, hata taxi inabeba abiria mmoja, lakini bado faini yake ni shilingi 30,000. Vile vile taxi zimebanwa sana, ujio wa bodaboda pamoja na bajaji umeua kabisa madereva taxi wengi, hali zao ni mbaya. Sasa tukiwaacha na faini kuwa ile ile shilingi 30,000, kwani taxi inabeba watu wangapi jamani? Taxi siyo daladala, inabeba mtu mmoja anayekodi, akipigwa faini ni ile ile shilingi 30,000. Kwa hiyo, Waziri alitazame hilo nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina maeneo mengi ambayo yanategemewa kuzalisha. Tumesikia hapa watu wanazungumza habari ya biashara katika Soko Kuu la Kariakoo, kwamba imepooza. Ni kazi ya Serikali kwenda harmonize biashara pale, kwa sababu pale tulikuwa tunapokea wageni wengi. Nchi nyingi wamekuwa wakija Kariakoo pale wanalala kwenye hoteli zetu, wananunua bidhaa hapa kwetu. Sasa tuiangalie ile kodi ya wafanyabiashara, ikiweza kupunguzwa kufikia kiwango ambacho wafanyabiashara wengi watalipa, itasababisha Serikali ikusanye mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina mashaka na Mchumi daraja la kwanza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na Engineer, hebu nendeni mkae mwangalie namna ya kulifanya lile soko lirudie ubora wake kama ambavyo lilikuwa Dubai ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimeona na nimpongeze sana kwa habari ya kuweka kodi kwenye michezo ya kubahatisha, hizi betting. Ushauri wangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, kwanza niwapongeze sana Sports Pesa wamekuwa wakidhamini timu ya Simba, Yanga na Namungo. Taasisi nyingine nazo zichukue, tuweke walau hata sheria ya lazima, hawa wanaoendesha michezo hii nao wadhamini club nyingine ili hizi clubs ziweze kupata wadhamini, ziweze kucheza michezo ya kibiashara na baadaye kukuza mpira wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaona soko kubwa, tuna wachezaji wa nje hapa wanalipwa fedha nyingi sana na wachezaji wetu wa ndani viwango vyao vimeongezeka. Unaweza kuona katika ukanda huu wa East Africa sasa hivi hakuna forward kama John Raphael Boko. Sasa tukizalisha akina Boko wa kutosha, maana yake ni nini? Maana yake Tanzania nayo itauza wachezaji nje, tutanufaika na uchumi wa michezo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Halafu mimi nikichangia huwa kengele inawahi. (Kicheko)

Mhehsimiwa Naibu Spika, kazi tuliyonayo nimesema kwanza ni kuhakikisha kwamba tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais katika kazi njema anayoifanya katika nchi hii, lakini tuelewe kwamba Rais anaandika historia yake na kuna vitu vya tofauti huko mbele ya safari vitatokea ambavyo havikuwahi kutokea katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kuna wengine hawalitazami, sisi tumekuwa tuna uchaguzi tofauti kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwenye chama chetu, uchaguzi unatangulia wa Zanzibar, halafu baadaye tunakuja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mungu akimpa uhai, akaendelea mpaka miaka
10 ijayo Mheshimiwa Samia, atakutanisha Uchaguzi wa Zanzibar na Uchaguzi wa Jamhuri, vyote vitakutana pamoja chini ya uongozi wa Samia. Sasa tumuache huyu mama aandike historia hiyo, yaani atakuwa Mwenyekiti wa Chama
2030 anayetafuta Rais wa Zanzibar na wakati huo huo anatafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo jipya kabisa halijawahi kutokea, lakini litatokea 2030. Kwa hiyo, hapa katikati mimi sioni kama kuna mtu yeyote katika nchi hii ambaye atasema anaweza kushindana na mama. Katika jambo gani? Maana mama anapiga hii mitano, anapiga mitano ya mwisho, halafu anaunganisha pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)