Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mhehimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa fursa ya mimi kuchangia Wizara hii muhimu sana ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na data za Wilaya yangu ya Uyui kwamba kuna kata 30, vijiji 156, vitongoji 688. Data za afya ni Hospitali ya Wilaya inatakiwa iwepo moja hakuna, vituo vya afya vinatakiwa 30 kipo kimoja na zahanati mbovu mbovu zipo 45. Eneo hili lina ukubwa wa kilometa za mraba 11,804 na wakazi 404,900. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti kabla ya yote, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya amenisaidia sana kunipitishia zahanati moja kuwa kituo cha afya, kwa hiyo, theoretically nina viwili. Pia nitoe pongezi kwa kijiji kimoja kinaitwa Chambola ambacho kimepigana na kuondoa kabisa vifo vya akina mama, kwa muda wa miaka kumi sasa hakuna mama hata mmoja aliyekufa akijifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kituo cha Afya cha Upuge, kituo hiki kimejengwa kwa mkopo wa hela za ADB. Kituo hiki kina mitambo yote ya kisasa, kuna mitambo ya kutengeneza oxygen inaweza kujaza hospitali zote za Kanda ya Magharibi, kuna seti ya kisasa kabisa ya vitanda viwili wanaweza kufanyiwa operesheni akina mama wawili. Mitambo hii ina miaka miwili tangu ilipokamilika na kufungwa lakini haijafanya kazi hata siku moja. Mheshimiwa Waziri naomba aje na jibu zuri la suala hilo kwa sababu wananchi wote na hata ADB waliotupa hizo hela wakija leo watatushangaa sana. Tulienda kuomba mkopo kwamba ni jambo muhimu sana lakini mpaka sasa mitambo mwaka wa pili haijafanya kazi. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri aje na mambo mazuri kuhusu suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati nyingine, kule kwetu Unyamwezini, kule Uyui hakuna dawa. Zahanati kilometa 50, 100 mtu anakwenda hakuna dawa. Matokeo yake waganga wa kienyeji kina Maji Marefu wangekuja kule wangetengeneza hospitali. Hakuna hospitali kule, kuna majengo mabovu mabovu ya zahanati hakuna dawa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napata taabu sana ninaposikia hapa kuna bajeti imeandaliwa ya Wizara ya Afya, nimepitia hii bajeti sioni utashi wa Serikali kunijengea vituo hivi ninavyovidai. Kama Uyui nzima ina kituo kimoja cha afya vinatakiwa 30 ningeona kwenye bajeti hapa Uyui tumeongeza vituo hata viwili, bora kuanza kuliko kukaa pale pale. Mimi ningeshukuru sana kama Mheshimiwa Waziri atakuja na majibu kwamba katika Wilaya ya Uyui hii mpya inakusudiwa kujengewa kituo. Bahati nzuri Naibu Waziri wa Afya anatoka vilevile Tabora na anajua hii hali. Kwa hiyo, ningetegemea kwamba nitapata upendeleo maalum lakini mambo haya yananipa taabu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maradhi kuondolewa ilikuwa ni ajenda ya kwanza tulivyopata uhuru kwa maana ya maadui wale watatu ilikuwa maradhi, umaskini na ujinga. Kule kwetu Jimbo la Uyui Kaskazini na Wilaya nzima ya Uyui sioni kama kweli ipo kisiasa nia ya kuondoa umaskini pale au nia ya kuondoa maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ndugu yangu Waziri, kwanza ni mtani wangu namshukuru sana ananisaidia lakini aje na dawa ya H5 yaani aje aseme natibu, hakuna maji H ya kwanza, H ya pili hakuna umeme kwenye kituo changu cha Upuge hicho, H ya tatu hakuna wataalam, atibu na H ya nne hakuna gari la wagonjwa, atibu na H ya tano hakuna vifaa vya tiba katika zahanati nyingine zote. Mimi nitamshukuru sana Mheshimiwa Waziri akija na mambo hayo ambayo nimeyataja hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ajaribu kutatua tatizo la dawa. Kila siku nasikia Medical Store au MSD tunavyoiita wanachoma tani 30, 40 za dawa ambazo zimepitwa na wakati, zime-expire. Dawa hizi wakiona kama bado miaka miwili zigawanywe bure badala ya kuzichoma zitumike kwa sababu kuna watu wanataka dawa leo hawangoji za mwaka kesho. Kama Medical Store wanachoma tani tatu au 10 za dawa, inagharimu kuchoma dawa lakini dawa zimenunuliwa na mahitaji ya dawa katika nchi hayajapungua hata siku moja. Uwepo mpango mzuri Mheshimiwa Waziri wa kuzuia kuchoma dawa badala yake zigaiwe bure maana kama mnazichoma wapeni watu bure hizo dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la Community Health Fund. Huu mfuko ulikuwa kimbilio yaani kule kwetu waliposikia kuna huu mfuko wamepapatikia kweli kweli lakini badala yake mzee mwenye nyumba anafariki amekamata kadi, ameenda hospitali hakuna dawa au kafiwa mama na kadi yake mkononi ya CHF hakuna dawa. Kadi zile watu walifikiri labda watapata dawa, lakini kadi zile hazitumiki na zikitumika hakuna dawa Mheshimiwa Waziri. Hii ni reality tuje tuangalie, unajua leo naongelea serious issues hapa hakuna kipepeo wala kupeperushana nasema ukweli kwamba CHF imekuwa kama mchezo fulani. Nakushukuru sana kwenye hotuba yako hii Mheshimiwa Waziri umesema utaileta iwe sheria na mimi naahidi nitawanunulia kadi kaya 2,000 ili mradi kuwepo na dawa, watu wapate kadi ambazo watapatia dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kata moja inaitwa Igulungu ilijengwa zahanati kwa mchango maalum ikafikia mpaka linta, ikaambiwa zahanati hiyo imejengwa karibu na hifadhi ikatelekezwa, huu mwaka wa 15 jengo lipo vilevile. Mimi wakati napiga kampeni nikasema nitalimalizia wakasema huwezi. Mimi nina uwezo wa kulimalizia jengo hilo lakini kuna stop order kwamba lipo karibu na Hifadhi ya Wanyama sasa nini bora wanyama au watu? Naomba Serikali itoe mwongozo kuhusu zahanati hii iliyojengwa karibu na wanyama. Watu hawatakwenda kwenye wanyama, kwanza wagonjwa watakimbizaje wanyama, hawawezi kukimbiza wanyama, watakuja kununua dawa au kutibiwa pale kwenye zahanati. Serikali iingilie kati ili tumalizie hiyo hospitali kwani hatutakwenda kukamata wanyama au kuingia kukata misitu, watu wagonjwa hata shoka hawana wanasogeleaje misitu! Hawa watu wana hatari gani, hawana hatari yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda sana kuwa mkweli, naipenda Serikali yangu, nampenda Waziri na Waziri mdogo ni ndugu yangu, mwanangu lakini katika suala hili wamenituma wananchi nije nidai hospitali na zahanati zijengwe. Tumepiga kura kumpa Mheshimiwa Rais kwa ahadi hiyo kwenye Ilani na mimi nimetangaza na mtu mzima kama mimi kuonekana muongo kwa wapiga kura hairuhusiwi. Nimewaambia tutaleta zahanati na kutakuwa na dawa sasa naonekana mimi muongo. Mimi sipendi naomba Mheshimiwa Waziri aje na dawa yangu ile ya H5. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana niachie wengine, naunga mkono hoja hii, ahsante sana.