Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Amour Khamis Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah kwa kuwa yeye ndiye aliyetuumba kuwa wanadamu na hakutuumba Wanyama, kwa hiyo, ametuumba wanadamu tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu Alhamdullilah. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana na kumshukuru sana Rais wa nchi hii ya Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan, mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kuwa Rais na ninampongeza pamoja na wote wafuasi wake wanaomsaidia Dkt. Mpango, Makamu wa Rais na Mawaziri wote na Naibu Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza kwa pongezi za kipekee kwa kutuletea hotuba hii au bajeti hii ambayo ni nzuri sana. Bajeti hii imewachukua mpaka wale ambao ni wachache kwenye Bunge hili wakadiriki kusema kwamba ile yaani inawasababisha kupata raha mpaka wanasema kwamba inawatekenyatekenya, inawafinyafinya, kwa kweli mimi nilijisikia faraja sana. Namuomba Mwenyezi Mungu ampe nguvu sana Mama yetu Mama Samia, nguvu za kipekee za kutuongoza kule tunakokuhitaji na amuepushe kabisa na maadui na mahasidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ndio itaenda kutekeleza Ilani yetu ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 na ninaimani kwamba mwaka 2025 Bunge hili linaweza likawa la Chama cha Mapinduzi peke yake kwa sababu reference mama yetu Mama Samia alivyokuwa Makamu wa Rais wakashauriana vizuri na Mheshimiwa Magufuli ambaye ni Hayati sasa hivi, walitekeleza ilani ipasavyo wakatufanya hata sisi Wabunge kutoka Pemba wa CCM tukawepo hapa. Leo tunajivunia sana kuwa Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kuwemo ndani ya Bunge hili kutoka Pemba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tabia tu kama alivyokuwa akilalamikia hapa Mbunge kutoka upinzani hapo, alikuwa akilalamikia kwamba, hakuna haki, lakini inavyoonekana kwamba haki lazima wapate wao ndio tatizo lao pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza pia mama kwa kutupatia zile shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo, namshukuru sana na watu wasiwe na wasiwasi jamani, hizi zilivyotajwa zilitajwa kwamba kila jimbo. Unapofanya wasiwasi kwamba sisi wapemba, sijui sisi Wazanzibari hatutapewa, maana yake una wasiwasi kwamba kule hakuna majimbo. Hizi fedha zitatoka jamani, msiwe na wasiwasi, haya maneno kasema mama, mna wasiwasi na mama? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Hatuna.

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sasa kuhusiana na hii nyongeza ya shilingi 100 katika mafuta, lakini pia katika mitandao ya simu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi 100 hizi mimi najiuliza hivi zitakuwa na alarm? Yaani zitakuwa na sauti zitakapoingizwa? Kiasi kwamba ikifika kwa mfano saa 6:00 ya usiku itamueleza Waziri wetu Mheshimiwa Miwgulu Nchemba kwamba leo kumeingia kiasi fulani cha fedha? Kwa sababu mwenzangu aliyepita kuchangia sasa hivi alikuwa anasema kwamba Waziri Mkuu alitumbua watu kwenye Wizara ya Fedha kwa sababu ya matumizi mabaya, sijui wanajilipa shilingi milioni 400 kwa siku na hizi zitakuwa na usalama gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuomba Waziri ajue kwamba yeye ndio kaka yetu katika familia hii ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini katika Chama cha Mapinduzi na ajue kwamba yeye ndio kaka mwenye fedha anatakiwa awe makini sana na mfuatiliaji sana na msimamizi sana wa hizi fedha. Kwa sababu wananchi wetu wako tayari kuchangia tena kwa heshima ya Serikali hii tukufu, lakini kwa heshima ya Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na sisi Wabunge tunalipa baraka jambo hili ila tunaomba kile kilichokusudiwa kitendeke. Na si eneo hili tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha kuna eneo lingine ungeweza kulitumia vizuri lingeweza kutusaidia sana hata katika tiketi za mabasi makubwa yale yanayokwenda mikoani ingetusaidia kama utafanya kifungu kidogo, kwenye tiketi za usafiri wa ndege, kwenye tiketi za boti; unaweza kuongeza hapo, lakini je, kweli itakwenda kuwanufaisha Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hicho ndio kitu cha kuzingatia. Kadri tutakavyokuwa tukilichangia jambo hili tuhakikishe kwamba, kile kichokusudiwa ndio kinaenda kutendeka kwa sababu nina imani kwamba Tanzania hii tukishatandika barabara zote hizi kodi zitapunguzwa pia, wananchi wetu watapungua kwenye kulipia kodi. Kwa hiyo, tunaomba sana Serikali ifikirie namna gani ya kuzisimamia kodi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi hizi zikikusanywa vizuri tutaondokana kabisa na madeni nje kwa sababu tunavyokopa au kadri tunavyopewa misaada hata wanafunzi wa darasa la sita najua plus minus is equal to minus, kwa maana sisi kadri tunavyokuwa tunapokea misaada ndio tunatoa yaani tunapoteza. Ni logic ndogo ambayo inatumiwa na wanafunzi wa darasa la saba, darasa la tisa, darasa la kumi, kwa hiyo ninaamini Mheshimiwa Waziri anaijua hii hajaisahau kwamba plus minus is equal to minus kwa kadri tunavyokuwa tunapokea misaada ndio tunavyokuwa tunatoa. Kwa hiyo namwomba sana Waziri wetu, kiongozi wetu, kaka yetu katika familia hii, atuongoze katika jambo la kujitegemea na si kuendelea sana kukopa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niishauri Serikali kwamba katika mikakati iliyowekwa kuhakikisha bajeti hii inapatikana inayosimamiwa sikuona, inawezekana imo lakini sikuona kwamba kunahitajika kuwe na usalama wa nchi. Nilimsikia Mheshimiwa Noah hapa akieleza orodha ya matukio ya ujambazi ambayo yapo, ambayo yangeweza kufanya wafanyabiashara kama walikuwa wanafanya biashara mpaka saa sita ya usiku, sasa wataogopa kwa sababu kuna ujambazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili naomba sana Serikali ilifanyie utafiti ni muhimu sana kufanyia utafiti. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)