Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon Munira Mustafa Khatib

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi kwa kuweza kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa niweze kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mwigulu Nchemba, lakini nimpongeze sana Naibu Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Engineer Hamad Masauni, lakini niweze kumpongeza sana Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na timu yake yote kwa pamoja kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kutuletea bajeti ambayo inaenda kumgusa mwananchi mwenye kipato cha chini moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Mama yangu Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa aliyoifanya ndani ya miezi mitatu, hakika natuheshimisha wanawake wote wa kitanzania, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kuangalia suala la Liganga na Mchuchuma kwa sababu ndani ya Bunge hili limeongelewa kwa muda mrefu toka sijawa Mbunge mpaka nimekuwa Mbunge, hiki ni kipindi changu cha pili, awamu zote mbili kwa sasa yeye ndio at least ameamua kuliingilia suala hili. Na suala hili litakapofanikiwa kufufua Liganga na Mchuchuma vijana wataweza kupata ajira kwa wingi, lakini tutaweza kununua pembejeo kwa wakulima wetu, lakini pia tutaweza kutengeneza barabara zetu kwa pesa zetu za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumpongeza pia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kufuta tozo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu asilimia sita, lakini kama mimi ni Mbunge wa vijana kama sijawasemea vijana wenzangu nitakuwa sijawatendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kiukweli juzi alituonesha upendo wa dhati Jijini Mwanza siku ya tarehe 16 na alituahidi mambo mazuri ambayo kwa sisi kama vijana atatupatia. Niseme ahsante sana, lakini naomba niyanukuu mambo machache kwa ufupi ambayo ametuahidi kama vijana; kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyia biashara, kuwapa ujuzi, mazingira bora ya kufanyia kazi ya uzalishaji, lakini kubwa zaidi kusubiria mkeka wa ma-DC, ma-DAS na Wakurugenzi ambao wengi wao watakuwa wanatokana na vijana. Nimuahidi Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa sisi vijana tuko nyuma yake na hatutamuangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali kwa kumaliza tatizo la kuunganishwa kiuchumi kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kutunga sheria ya kuondoa kodi kulipia mara mbili. Nishukuru sana Serikali yangu, lakini bado kumekuwa na changamoto kuhusu wafanyabiashara wa Kizanzibari wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu sasa kuhusu mfumo wa kodi uliokuwepo sasa hivi. Niiombe Wizara ya Fedha iweze kuangalia upya kuhusu mfumo wetu wa kodi kwa wafanyabiashara wetu wa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala Wabunge wengi hasa kutoka Zanzibar, wameliongelea na mimi nikiwa mmojawapo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu tukae tuangalie Zanzibar na Tanzania Bara ni nchi moja, lakini sijui kwa nini kumekuwa na ukiritimba katikati ambao haueleweki kati ya wafanyabiashara wetu kutoka Zanzibar kuwa-charged tena mara mbili kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania Zanzibar tayari wameanza kufanya marekebisho ya Sheria ya VAT kwa kuondoa tozo mpaka kufikia asilimia sifuri, lakini kwa bidhaa za viwandani peke yake. Hii haijaidia kwa mfanyabiashara ambaye hana bidhaa za viwandani na niishauri Serikali hata ikiwezekana kuiruhusu sukari yetu ya Zanzibar kuuzwa Tanzania Bara kama itawapendeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mheshimiwa Waziri wa Fedha amependekeza kodi mpya inayotokana na simu pamoja na mafuta ili kuweza kupata fedha kwa miradi ya kimaendeleo. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri wa Fedha wa Tanzania Bara, je, amewasiliana na Waziri wa Fedha Tanzania Zanzibar kuhusu mgawanyo wa miamala na matumizi? Kwa sababu kwa upande wa Zanzibar bado sijaona kitu chochote kuhusu kodi hii inayotokana na mafuta na simu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa mwaka tutakusanya zaidi ya shilingi trilioni mbili kwa tozo zinazotokana na sim una mafuta. Hizi fedha ni nyingi sana, ili Watanzania wawe na imani ya kuchangia fedha hii ni lazima Wizara iweke wazi jinsi ya kutumia fedha hii, lakini nataka niishauri Serikali kwanza kuwa na uwazi jinsi miradi itakayotumika kwa fedha za tozo hii ya mafuta na simu, lakini pia kuwe na ukaguzi wa CAG tena wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Mheshimiwa Waziri, hivi karibuni tumemuona Mheshimiwa Waziri Mkuu akitumbua wafanyakazi wa Wizara ya Fedha, aliwasimamisha kazi kutokana na matumizi mabaya ya fedha ambayo yalikuwa yanatumika bila ya mpangilio maalum. Ndio maana nimesema hizi fedha ambazo zitakusanywa zikaguliwe na CAG tena ikiwezekana mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu upungufu wa wafanyakazi wa TRA. Nimemsikia Mheshimkiwa Waziri kuwa tutaweza kuajiri wafanyakazi 40, lakini niseme jamani wafanyakazi 40 ni wachache sana. Mimi binafsi nilikuwa katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira nimeona jinsi watu wa TRA wanavyolalamika kuhusu wafanyakazi wao, tunapoteza sana mapato ya Serikali kwa sababu watumishi ni kidogo. Niiombe Serikali iweze kutoa kibali cha kuajiri wafanyakazi wengine wapya tena wenye weledi na uelewa wa jinsi ya kuweza kukusanya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2020/2021 tumekusanya shilingi trilioni 14.52 sawa na asilimia 82 tu; bado malengo ya Serikali hatujafikia. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kuajiri watumishi wa TRA ili kuweza kupata fedha zaidi kwa sababu sasa hivi wamekuwa hata wananchi zamani ilikuwa kuna elimu mwananchi aweze kudai risiti ya kielektroniki, lakini sasa hivi mwananchi mfanyabiashara hawatoi risiti za kielektroniki na tunaweza kupoteza kodi kubwa ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie, nimeona matairi ya pikipiki tayari yameongezewa charge ya VAT, lakini sasa hapa Tanzania tunakiwanda chetu cha General Tyre ambacho tulikuwa tunazalisha matairi. Niiombe Serikali kama kweli tuko tayari kuwasaidia vijana na ajira tungeangalia suala la kufufua kiwanda hiki cha General Tyre kilichopo Arusha. Toka mimi sio Mbunge kiwanda hiki cha General Tyre kinapigiwa makelele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekunde 30; naomba nipongeze sana Wizara hii na niseme inaenda kufufua uchumi wa mwananchi, vyuma vinakazuka chini ya Rais mwanamke Mama Samia Suluhu Hassan. Naunga mkono hoja. (Makofi)