Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi hii kuwa miongoni mwa watu ambao watachangia bajeti kuu ya Serikali, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha. Kwanza nianze kuipongeza Serikali, nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, kwa muda mchache ameleta bajeti yenye matumaini makubwa kwa wananchi, kwa sababu wananchi wetu walikuwa na kero kubwa sana juu ya maendeleo yao sasa hata kodi zetu ambazo tunakwenda kuzilipa zitaleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachi walitaka hatima ya maboma ambayo wanayaanzisha yaweze kukamilika, pia kwenye bajeti hii imejipambanua wazi kabisa kuwa maboma yetu yanakwenda kukamilika na watu wataanza kupata hudama, hongereni sana Serikali. (makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watanzania wanahitaji kulipa kodi, lakini waione kodi yao inafanya kazi. Leo tumeleta mpango wa kufuta baadhi ya kodi na kuongeza baadhi ya kodi, lakini inahitajika elimu iongezeke zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunaishukuru Serikali kwa kupunguza tozo au faini ambayo ilikuwa ilikuwa inatozwa kwa watu wa boda boda wanashukuru sana, na tumekuwa tunapokea simu hasa mimi kutoka jimboni wanasema mmetupunguzia faini lakini mmeongeza fedha kwenye mafuta, ukiangalia uhalisia fedha kwenye mafuta haijaongezwa ni utaratibu wa kawaida ambao ulikuwa tangu zamani, na wananchi wanaona mafuta yamepanda zaidi kwa kipindi hiki kifupi, basi wanajua fedha sasa Serikali imepunguza faini imekuongeza kodi kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, tunapokuwa tunafanya hivi vitu basi tuongeze na wingo wakutoa elimu. Kwa mfano watu wa mamlaka inayohusika na upandishaji wa bei za mafuta, basi wanapokuja kupandisha au kushusha wanatakiwa watoe taarifa kwa wananchi ili waweze kujua tumeongeza kwa sababu gani au tumepunguza kwa sababu gani, ili tuweze kupunguza haya mengine ambayo wananchi wanashindwa kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze kwa kupunguza faini kutoka shilingi 30,000 mapaka shilingi 10,000, mmewasaidia sana boda boda na Mheshimwia Waziri ulisema hapa unahitaji boda boda wasiwe ndio chanzo cha mapato ya Serikali, unahitaji Polisi wafanye kuwaelimisha boda boda ili wesiwe miongoni mwa wavunja Sherika. Nikupongeze sana, maana Polisi walibadilika kuwa mungu watu. Sisi kwetu kule boda boda ndio ambulance ya kupeleka wangojwa, ili mgonjwa aweze kukaa vizuri kwenye pikipiki lazima ubebe na mtu mwengine wa kumshikilia, ukikutana na Polisi anawaza tu yeye kutoza faini, sasa ilibadilika kuwa ni kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kuipunguza hii imetusaidia sana. Na mimi niiombe na nimuombe Waziri wa Mambo ya Ndani, Polisi wetu watusaidie sana kuwapa watu elimu. Unajua kuna mazingira mengine hayahitaji hata faini, unaweza kukutana na mtu amevunja taa kwa bahati mbaya wakati huo huo umekutana naye anakwambia gari lako bovu, ukumwambia nimevunja sasa hivi anakwambia hamna lete nikupige faini, wakati ilikuwa ni kitendo cha kuweza tu kumwambia, changamato hii nenda kairekebishe, hilo litatusaidia sana na litatupunguzia malalamiko kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa Madiwani, niipongeze Serikali kwa kulibeba jukumu hili ambalo lilikuwa ni kero kwa madiwani wetu. Madiwani kero kubwa ilikuwa ni kupata ile stahiki yao kwa wakati, ilo sasa Serikali mtakwenda kulifanya kwa utumilifu, kwa uhakika mkubwa kwa sababu Serikali ikipanga jambo lake na likiingizwa kwenye bajeti basi haliwezi kukwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani walikuwa hawahitaji kulipwa ile pesa kwa wakati tu, bali walikuwa wanaomba waongezewe posho, kiukweli sisi wenyewe tunajua tukirudi kule majimboni tunakuwa sisi wenyewe ni madiwani, wananchi wote wakiwa na matatizo basi kabla hawajaenda sehemu yoyote basi wanamkimbilia Diwani, wanamkimbilia Mbunge, wanakimbilia sehemu zengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali. Kwa kuwa tulimebeba hili jukumu basi tuone namna gani ya kuwasaidi hawa Madiwani. Na pia tumepata changamoto nyengine, kuna muongozo ulikuja kule kuna Madiwani wamekuwa wakikatwa posho zao, leo tunakwenda kulalamika kumkata Diwani shilingi laki moja na ishirini eti kwa sababu anakaa Makao Makuu ya Halmashauri, hiyo imeleta changamoto sana, majukumu ya Diwani ni yale yale, ni sawa sawa na mbunge anaetoka Kongwa, anaetoka Bahi ukamkata usimlipe per diem, hiyo sasa siyo sawa kwa sababu wale wadiwani wanaposafiri kwenda pale wamebeba dhamana ya wananchi wao kutoka kwenye kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali, tuwaangalie madiwani wanamajukumu makubwa sana kama tulivyo sisi, tunapokwenda kuwapunguzia posho zao. Kwanza posho ni ndogo, unaenda kupigana nae kwa shilingi laki moja, anafanya kazi kubwa, anapitisha mapato yote ambayo yanatekelezwa katika halmashauri. Kwa hiyo, niombe Serikali itusaidie hili nalo litoe muongozo, kwa sababu wamekuwa wakigombana na wakurugenzi, wakurugenzi wanaosimamia sheria, inakuwa imeleta tabu. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kutusaidia katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lengine kuhusu tozo za simu. Serikali imekuja na nia njema sana katika kukusanya kodi kwa kupitia simu zetu, niiombe Serikali. tumekuwa tukifanya miamala tunalipa mara mbili mbili, leo ukitaka kutuma milioni moja kwanza wewe unaetuma unakatwa shilingi elfu nne, yaani unatuma kwa mtu akapate hela wanakatwa elfu nne, akifika tena yule mtu kabla hajaitoa anakatwa elfu nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kama mnataka kuitoza vizuri hii kodi, wale makampuni tunahitaji waendelee ku-survival katika ufanyaji wa biashara, basi kama inakatwa ile ya kutumia iwe ya Serikali, ile nyingine iwe ndio iwe makato ya kampuni na wale wengine watoa huduma, kwa sababu unakuta milioni kuituma na kuitoa zaidi ya shilingi 12,000. Serikali inaenda kupata haifiki hata elfu tatu, sasa zingine zote zinapotelea hewani hewani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali. Tumekuja na mpango mzuri lakini kuna sehemu kuna linkage hasa hii mitandao ya simu, imekuwa kero kwa sababu wanaongeza tu yaani makato yamekuwa yanaongewa kiaina aina tu hata haieleweki. Leo wanakwambia kufikia 5599 ikifika tu na kamili ile wanaongeza tena 300 zaidi ya ile kilichokuwa. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie hili suala, na ndio maana tulikuja hapa kwenye uchangiaji wa sekta ya mawasiliano, tulisema tuimarishe shuirika letu la TTCL, haya yote hayatokuwepo, lile shirika ni la Serikali asilimia mia moja, haya makampuni mengine yapo kibiashara na hii tukiimarisha shirika letu linaweza kutusaidia hata tozo zenyewe za makato yakapungua, watu wakapiga simu vizuri, Serikali ikapata fedha zake vizuri bila ya hata kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali, kwa kuwa imekuja na mpango huu mzuri tuangalie na sehemu zinapo-link haya matatizo yanayotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, nakushkuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)