Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Santiel Eric Kirumba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SANTIEL E. KIRUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote napenda kuipongeza Wizara ya Fedha kwa bajeti hii ambayo imekuwa ni rafiki kwa maendeleo ya nchi hii, bajeti ambayo ieonesha dhima nzima ya Mheshimiwa Rais ambayo siku ile alikuwa ana hotubia hapa. Pia, bajeti hii imelenga hasa katika suala kamilifu la kutekeleza kuboresha mazingira ya kibiashara. Tumeona kwamba katika bajeti hii kodi nyingi zimefutwa. Mama amejitahidi kwa kiasi kikubwa kuonesha nchi hii ni sehemu salama kwa kwa ajili ya watu kuja kuwekeza. Viel vile bajeti hii imeweza kurahisishwa ulipaji wa kodi. Kwa hiyo, napenda kuipongeza sana Awamu ya Sita kwa kazi kubwa inayoifanya na Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchangia kwenye kitu kingine na kutilia mkazo katika Halmashauri zetu. Halmashauri zetu zinafanya kazi vizuri, lakini kuna nyingine ambazo makusanyo yake ni madogo. Sijui Wizara ya Fedha imejipangaje katika kwa Halmashauri ambazo vipato vyake ni vidogo, makusanyo hayo ambayo yanakwenda kuathiri zile asilimia 10 ambazo tumewaahidi wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukulia mfano kama Halmashauri ya Shinyanga Vijijini, Ushetu, kwa kweli kwa mwaka hawa watu mapato yao ni madogo. Unakuta makusanyo kwa mwaka ni shilingi milioni 137, watu waliokopeshwa unakuta ni vikundi 10. Sasa fikiria kwa haraka haraka, ni vikundi vingapi vitakuwa vimefikiwa ili kuwezesha hawa vijana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaona huku kwenye Serikali ajira bado ni ngumu kupatikana na pia huku tumeweka katika Ilani yetu kwamba tutawezesha vijana, wanawake na walemavu kupata mikopo. Ukija huku nako bado mapato yanayopatikana ni machache kiasi kwamba hawawezi kukopesheka na hawawezi kupata fedha za kutosha kwa ajili ya kutenga ile asilimia 10, vijana wote na wanawake wote wakaweza kufikiwa. Licha ya hivyo, bado fedha nyingi zipo mikononi. Sijaelewa kwa jinsi gani Wizara ya Fedha itaweka msisitizo katika hizi Halmashauri zile fedha ziweze kurudishwa ili zikawasaidie wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuja kwenye suala lingine la TRA. Mmeona kabisa tulivyokuwa kwenye semina imeonesha kwamba walipa kodi ni 5% katika nchi hii ambayo ina watu milioni 60 ambapo walipa kodi almost milioni tatu. Utafikiria kwamba kwa kiasi kikubwa wananchi hawalipi kodi. Vilevile Serikali haijaweka mazingira rafiki kwa ajili ya watu kulipa kodi. Unaweza kufikiria kwamba kwa kipindi kilichopita kuna watu walikuwa wanabambikiziwa kodi kitu ambacho kinaweza kikawafanya wale wafanyabiashara wakaingia hofu na kutufanya tupoteze mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali itaweza kujipanga na ituoneshe kwamba katika bajeti hii imejipangaje kwa wale watu ambao walibambikiziwa kodi? Maana kuna watu walibambikiziwa kodi mpaka wamefunga maofisi. Je, haioni kwamba ni wakati sahihi sasa hivi ya kukaa tena na wale wafanyabiashara na kuzitoa zile kodi ambazo zilikuwa siyo sahihi? Wali-double charge kwenye VAT katika mapato yao ya kipindi cha nyuma. Naona Wizara ya Fedha ingekuja na mkakati mpya wa kupitia wale wafanyabiashara ambao walikuwa wamefanyiwa huo mchezo. Nami nakuomba Mheshimiwa Waziri, nakuona hapo, mimi nitakufuata kwa sababu nami ni muhanga wa suala hili, kwa sababu hiyo inamfanya mtu akwepe kabisa kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, kuna hizi Agency Notice zinawekwa. Unakuta kuna wafanyabiashara wanafanya kazi on credit bases; thirty days, sixty days of invoice. Sasa unakujakuta hata yale malipo hajayapata, ameshatumiwa Agency Notice kwa mteja wake. Ile inamfanya huyu mlipaji kodi ashindwe kulipa hii kodi. Kwa hiyo, naomba kabisa Wizara ya Fedha ifanye mkakati wa kufanya hii Taasisi ya TRA, walipa kodi walipe kwa hiari, siyo kwa kutumiwa task force, siyo walipe kodi kwa kulazimishwa. Mtu afike mahali aone ni hiari kuichangia Serikali yake, siyo Serikali itumie nguvu kum-force mtu alipe kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nataka kuchangia sehemu nyingine ambayo ni ya mwisho, nayo ni sekta ya afya. Nimeona kwenye sekta ya afya mmetenga bajeti kwa ajili ya kumaliza maboma 8,000. Hiki ni kitu muhimu sana. Haipendezi tena tunaporudi kule kwa wananchi wetu tuwakute tena wanalalamika na wameweza kupandisha mabomba maboma hayo 8,000 mpaka kufika hapo. Serikali inabidi sasa mkafanye mpango kama mlivyofanya kwenye barabara na pia kujenga shule. Mheshimiwa Ummy umefanya jambo moja zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuomba sana, wanawake wakasaidiwe kupata sehemu salama za kujifungua kwa sababu haya maboma 8,000 yanaweza kufanya ushawishi mkubwa sana kwenye Sekta ya afya, itafanya mapinduzi makubwa sana kwa sababu kuna yale maeneo ambayo kweli yana mwendo mrefu mtu kukuta Kituo cha Afya. Nina imani kwamba hili nalo likitekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sisi Wilaya ya Kishapu ina maboma 20 ambayo hayajakamilika. Ukienda Wilaya ya Shinyanga Vijijini, ina maboma 39 ambayo haijakamilika. Sasa utaona kwa jinsi gani kukiwa na mama mjamzito atapata shida, ambao ni wanawake wenzangu; kuna Watoto na wazee ambao wanaenda mwendo mrefu kupata huduma ya afya. Nina imani hilo nalo linaenda kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, hayo ndiyo yangu, naunga mkono hoja. (Makofi)