Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii, ambayo ni nzuri na inatia moyo sana Watanzania. Nichukue nafasi hii kumupongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, kwa kuchukua mawazo ya Wabunge kwa kiasi kikubwa sana na kuyaweka kwenye bajeti hii. Hili linafanya hata sisi tunapochangia, tunakuwa na moyo kwa kuamini kwamba Serikali inatusikia. Kwa hiyo, nimshukuru sana kaka yangu Mwigulu na ukizingatia ni Jirani yangu pale Jimboni, basi najisikia furaha sana kwa jinsi kazi nzuri anayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, tunarudia kukazia pale ambapo tunaona ni muhimu zaidi pia na kwa sababu jambo likisemwa na wengi linakuwa pia ni sauti ya Mungu, naomba tu nijikite kwenye suala la elimu haswa ya Sekondari. Nishukuru kwamba Serikali sasa inaenda kutujengea shule moja kwenye kila Kata, shule kamili hasa katika kata mpya na zile kata kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kuikumbusha Serikali kuziimarisha shule zetu za Kata ambazo tumezijenga pamoja na wananchi nchi nzima. Shule hizi zilianza kwenye wakati mgumu, lakini zimeendelea kuimarika mpaka zimetoa wataalam wakubwa katika nchi hii. Hata hivyo, bado shule hizi zina changamoto kubwa. Kama tunavyofahamu kata zetu hazina tofauti na baadhi ya wilaya, kata zetu ni kubwa sana na shule hizi zimejengwa katika maeneo ambayo iweze kuhudumia angalau vijiji vya kwenye kata hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nchi yetu hii kijiji hadi kijiji kuanzia kilometa 10, 15 mpaka 20 ni jambo la kawaida kabisa. Kwa hivyo, watoto wetu wa kike na wa kiume wanatembea mwendo mrefu sana mpaka kufika shuleni. Huko wanakutana na majanga mbalimbali, watoto wa kike wanabakwa, watoto wa kiume wanajiingiza kwenye vitendo viovu mpaka kuvuta bangi. Hii inapelekea mpaka wazazi wanaamua sasa kuwapangishia vyumba watoto wao, karibu na maeneo ya shule katika mazingira magumu sana, vyumba vinaitwa mageto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa Mkuu wa Wilaya ya Chemba, nimefika nakutana na watoto wanakaa geto. Sasa mtoto wa Form One, anaenda kusoma anakaa geto, ajitegemee, mazingira magumu, hakuna umeme, halafu tunategemea kwamba mtoto huyu apate elimu bora, ni jambo gumu sana. Hata Walimu wenyewe, inabidi wakatafute mahali pa kuishi mbali sana na shule. Wanatumia usafiri, wengine wanatembea kwa miguu, wengine wana pikipiki, anafika shuleni amechoka, atoe elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa naomba nitoe ushauri kwamba, pamoja na hii nia nzuri ya kuanza kujenga shule mpya. Niombe Serikali iangalie jinsi ya kuimarisha hizi shule zetu, sasa tuzijengee mabweni ya wasichana na wavulana ili watoto wetu wakae shuleni. Kwa sababu, Serikali inalipa ada, mzazi tukimwambia alipie chakula kwenye hosteli atalipa. Atampa mtoto wake chakula kile ambacho angekula nyumbani, sasa atakipeleka hosteli ili mtoto akae shuleni aweze kula chakula kile kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali ijenge nyumba za Walimu ili Walimu wakae shuleni. Ni kweli tunalalamika kwamba, elimu yetu ina tatizo, watoto wetu wana akili sana, lakini mazingira tuliyowapa ni magumu. Shule hizi tulizianzisha, zimetusaidia, lakini tuendelee kuziimarisha. Naamini kabisa fedha ambayo inayotumika kujenga shule kila kata, ingetumika kuimarisha hizi shule kwa kujenga hosteli na mabweni, impact yake ingekuwa kubwa zaidi pengine kuliko hata hii shule moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikatai shule ni kitu kizuri, lakini kama ningeambiwa kipaumbele, ningeona ni bora tujenge hosteli kwanza kwenye hizi shule za wasichana na wavulana, ili shule hizi za kata zilizopo ziimarike. Kwa sababu, hata aliyepo mbali, hata aliyopo kwenye kata mpya kama shuleni kuna hosteli atakwenda kukaa kule na atapata elimu bora. Kwa hiyo, niiombe Serikali yangu hizi shule tusizisahau, tukaanza kujenga shule mpya kubwa kubwa, wakati kuna shule ambazo tukiziimarisha tutakuwa na impact kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihame niende kwenye suala la mikopo ya hawa vijana. Kwa kweli, Serikali yetu ina nia njema, imetenga fedha kwa ajili ya vijana, halmashauri hata kwenye Wizara, imetenga fedha kwa ajili ya akinamama, lakini, urejeshaji wa hii mikopo umekuwa mgumu sana. Vijana wamechukua fedha, miradi imekufa, halmashauri inashindwa kuwapeleka mahakamani na hata ukiwapeleka dhamana zenyewe hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ile fedha inapotea na vijana wengine ambao hawakupata mkopo wanakosa. Kwa hiyo, ningeshauri, tufike mahali tubadilishe mbinu ya jinsi ya kutoa hii mikopo. Serikali itengeneze mradi, mradi ukamilike. Kama ni mradi wa nyuki inunue mizinga, itundike, ikusanye vijana, iwape elimu jinsi ya kufuga nyuki, inawakabidhi, ni rahisi kuwa-monitor ili waweze kurudisha ile fedha. Kama ni ufugaji wa kuku inunue incubator, ijenge mabanda, itoe elimu kwa vijana, wanakabidhiwa pale, ni rahisi kuwa-monitor na kurudisha ile fedha na wengine wapate. Hii kuendelea kutoa cash tunapoteza fedha na hakuna impact tunayoiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba, tubadilishe huu mtindo, kuliko hii fedha ziendelee kupotea, tutengeneze miradi. Kwanza hii njia italeta ajira ya uhakika, kwa sababu ukitengeneza mradi unachukua vijana wote kuanzia wa darasa la saba mpaka wa chuo kikuu. Mle kutakuwa kuna watenda kazi, kuna mameneja, kuna kila kitu kwa sababu ule mchanganyiko unakuwa ni wa kutosha. Kwa hiyo niombe, Serikali ibadilishe mtindo, ili tupate impact ya hizi fedha za kukopesha vijana wetu. La sivyo, tutakuwa tunapoteza ajira bado hakuna na fedha zinaendelea kupotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia niende nikawasemee Madiwani. Kwanza niishukuru Serikali kwa kuwahamisha tu mahali pa kulipiwa fedha, kutoka kwenye halmashauri kwenda kwenye Mfuko Mkuu. Kilichopatikana hapo ni uhakika na kutokucheleweshwa na heshima, lakini kiukweli tatizo hasa kubwa bado, hawa Madiwani wanafanya kazi kubwa sana. Ule usumbufu wa matatizo ya wananchi tunaoupata sisi Wabunge kwenye Jimbo zima wao wanaupata pia, kwenye kata zao. Kwa hivyo, ni watu ambao wanahitaji wawe na angalau na peace of mind, hii posho ya Sh.300,000 ni ndogo mno. Ningeomba kwa sababu, Serikali Kuu imebeba mzigo wa hii shilingi 300,000, tuwaagize halmashauri, sasa Wakurugenzi wawaongeze hata shilingi 100,000 kama posho ya madaraka ili ukichanganya angalau ziwe shilingi 400,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walikuwa wanaweza kuwalipa shilingi 300,000, sasa kama Serikali kuu imechukua, tukisema wawaongezee hata shilingi 100,000 utakuwa ni mzigo mwepesi. Angalau bado hazitoshi, lakini angalau itapunguza hata kidogo. Kwa hiyo, tutakuwa tumewapa heshima ya kuwalipa kwenye Mfuko Mkuu lakini pia, tuwaongezee chochote, kiweze kupatikana. Hawa ni wenzetu na wana-deal na wananchi na wote tunaelewa, jinsi wananchi wanavyotegemea Wabunge, wanavyotegemea Madiwani na sisi ndio watu wa kutatua shida zao. Wenzetu hawa na wenyewe wakiwa katika hali nzuri na hata huko majimboni patatulia. Tukiwa huku na sisi tunapumua. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla naomba hili liangaliwe, ni jambo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwa Madiwani sasa hivi, hii posho ya vikao, vikao vyenyewe vya Baraza la Madiwani ni kama vinne tu kwa mwaka, lakini sasa kuna hii posho hii ya kikao inaitwa nyingine sijui ya kujikimu, Diwani inabidi akae kwenye kikao sijui mpaka kwenye saa 9.00 au saa 10.00 ndio alipwe ile fedha. La sivyo, siku nyingine anaambiwa wewe wa karibu, itabidi ulipwe nusu usipate night. Fedha yenyewe ndogo, bado ametoka huko Mheshimiwa Diwani amesafiri mwingine na pikipiki, anafika inabidi akae kwenye kikao walazimishe mpaka ifike saa 9.00 ndio ile fedha iingie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, hii shilingi 100,000 ukiachana na ile Sh.40,000/= ya sitting, hii shilingi 100,000 iitwe tu fedha ya kikao, ili hawa walipaji waweze kulipa hii fedha bila matatizo, lakini unapoita night sijui mpaka ifike saa 9.00, sijui mpaka saa ngapi kunakuwa kuna double standard, kuna vurugu kila wakati. Madiwani wangu wa Mkalama juzi wamekaa hapa wengine wamelipwa night, wengine hawajalipwa, mchanganyiko na naamini hii iko katika maeneo yote ya Wabunge wote. Hebu tuiite tu shilingi 100,000 ya kikao, shilingi 40,000 sitting, vikao vyenyewe mara nne kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na dada yetu Waziri wa TAMISEMI, wapeleke waraka. Waraka wamepeleka ule, wenzangu wa TAKUKURU kwa sababu, wenyewe wanafanya kazi yao, wakaingia nao pale kama hamjafika saa 9.00, fedha haitoki. Sasa inasababisha hata mambo mengine hayapiti, wanakwamisha tu Madiwani ili angalau ifike saa 9.00. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu niombe hii fedha ya shilingi 100,000 na shilingi 40,000 ya sitting utoke waraka, ni fedha ya kikao, ieleweke katika maeneo yote…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)