Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi niweze kuchangia kwenye bajeti hii ya Serikali. Binafsi napenda kutumia fursa hii kumpongeza Rais Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kuanza vizuri katika uongozi wake wa Awamu ya Sita tunampa pongezi nyingi sana. Pia nimpongeze kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa kuteuliwa kwenye wadhifa huu katika Wizara hii nyeti ya Fedha. Nitoe pia pongezi kwa Mawaziri wote wanaofanya kazi kwenye Serikali hii, wanafanya kazi nzuri, hongereni sana Mawaziri wote pamoja na Manaibu Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze vile vile Serikali kwenye bajeti yake hii iliyowasilishwa, tumeweza kuona bajeti ambayo inaenda kuendeleza miradi ya kimkakati ambayo tumekwishaianza, tumeweza kuona fedha zikitengwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linakwenda kuzalisha umeme megawatt 2,115. Hongera sana Serikali kwa maana bwawa lile mpaka sasa hivi limeshafika zaidi ya asilimia 52 ya ujenzi wake. Kwa hiyo ni hatua nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze kwa kuwekwa fedha kwenye kuendeleza ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ambapo juzi tumekwenda kuzindua kuweka jiwe la msingi ujenzi wa reli kutoka Mwanza kuja Isaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze pia kwenye bajeti hii kutenga fedha za kupeleka umeme vijijini tumeona fedha mlizotenga 1.2 trillion kwa ajili ya kusambaza umeme vijiji vyote Tanzania, hongera sana kwa Serikali, inaenda kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kuona fedha walizotenga kwa ajili ya kujenga barabara na madaraja katika nchi yetu. Ni bajeti ambayo inakwenda kumkwamua mwananchi na kulisogeza Taifa letu mbele. Kwa kweli ni bajeti ambayo imezingatia viwango, ni bajeti ambayo imekuwa ya kihistoria na ni bajeti ambayo inakwenda kutoa tafsiri katika wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia kwenye bajeti hii; tumeweza kuona katika bajeti hii sehemu zenye upungufu katika baadhi ya Wizara. Sehemu ambayo napenda kuchagia ni kwa Wizara ya Kilimo. Wizara ya Kilimo imetengewa bilioni 200. Wizara ya Kilimo ni Wizara Mama na ni Wizara ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa letu. Tukiwekeza fedha kwenye kilimo tutauinua uchumi wa Taifa letu. Leo tunahangaika kutafuta fedha za kodi mbalimbali kwenye maeneo mbalimbali, lakini tukiwekeza kwenye kilimo, mzunguko utakuwa mkubwa kwenye uchumi wetu. Mfano tu, tumetenga bilioni 200, hizi haziendi kujenga skimu wala mabwawa, ni maeneo machache sana ambayo tunaweza kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tungeweka trilioni moja kwenye sekta ya kilimo, tukaenda kujenga mabwawa, tukaenda kujenga skimu za umwagiliaji, tutaweza kuzalisha mara mbili ya tunavyozalisha sasa hivi. Tukizalisha mara mbili maana yake tunainua uchumi wa watu wetu na wataweza kufanya biashara. Nataka nitoe mfano, pale Igunga tuna bwawa moja, skimu tulizonazo ni nne. Kata ya skimu hizi nne, tatu zinafanya kazi kwa kutegemea mvua, skimu moja inafanya kazi kutegemea mvua na maji yaliyopo kwenye Bwawa la Mwanzugi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bwawa hili linatusaidia kuzalisha mpunga mara mbili kwa mwaka na uchumi wa Igunga kwa kiwango kikubwa sana pale Mjini tunampunga mwingi ambao watu kutoka Rwanda wamefungua kiwanda pale cha kuchukua mpunga, lakini pia na kuuchakata kupata mchele, wanafanya packaging wanapeleka kuuza kwao. Kwa hiyo unaweza kuona kwamba hizi skimu zetu tukiziwekea mabwawa kwenye maeneo yetu sio tu Igunga, maeneo yote nchini, tukajengwa mabwawa, tutalima mara mbili na tutazalisha mara mbili, wananchi wetu watapata fedha na Serikali itapata fedha zitakazoweza kuinua uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri bajeti yake ijayo atenge fedha za ujenzi wa mabwawa kama kweli tunataka tuinue au tukomboe uchumi wa wananchi wetu, tujenge mabwawa. Pale Chomachamkola tunahitaji tujenge bwawa kubwa, tuna wakulima, tukienda Ziba kunatakiwa kuwepo na bwawa, Nsimbo panatakiwa pawepo na bwawa na Buwekelo tunatakiwa tuwe na mabwawa. Mabwawa haya tukiyajenga katika maeneo mbalimbali nchini, bajeti ya Mheshimiwa Waziri ita- shoot. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri bajeti yetu sisi ni trilioni 36, lakini bajeti hii tukilinganisha na nchi jirani kama Kenya ambayo tunahitaji tuwe washindani wetu, ni mara mbili yake yaani Kenya iko zaidi chukua trilioni 36 mara mbili maana yake wao wao trilioni 70 na ushehe. Kama kweli tunahitaji tushindane katika ukanda wa Afrika Mashariki tuwe giant bajeti yetu lazima i-shoot.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kuchangia upande wa mgao wa fedha tunaopatiwa. Nimeweza kuona kwenye bajeti hii tumekuwa tukipata fedha kwa kila jimbo kupewa wakati mwingine zahanati mbili mbili, kupewa vituo vya afya kimoja kimoja kila Jimbo na sasa hivi tumeona tumepewa milioni 500 kila Jimbo. Nawashukuru sana kwa kutupa hizi fedha, lakini niwaombe, sikatai na sisemi wasiwape lakini wawe wanaangalia mahitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Majimbo ya Vijijini au ya Halmashauri hayalingani na Majimbo ya Mijini. Wanavyotuambia wanatupa milioni 500 sawa na Majimbo ya Mjini hawatutendei haki. Wawape milioni 500 lakini sisi wa vijijini watupe bilioni moja. Wakitupa bilioni moja angalau tutaweza, kwa sababu mijini kuna miradi mikubwa tunaweza tukaiona katika miji na Manispaa, kama vile miradi ambayo inakuja kwa ajili ya kuendeleza miji, lakini kuna mradi ambao umemalizika ule wa TSCP, tumeona mikoa yote barabara za lami zinamwagika, lakini kwenye halmashauri zetu kwenye majimbo yetu hakuna lami za kutosheleza. Kwa hiyo niwaombe Wizara waliangalie hili, safari ijayo kwenye migao yetu wawape lakini sisi watupe mara mbili ya wanayowapa wao. Kama kwenye afya wakitupa vituo viwili, kila jimbo au kituo kimoja kila jimbo, basi majimbo ya vijijini watupe vituo viwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu katika Wilaya wana Hospitali ya Wilaya, wana fedha za kuboresha kila kitu, kijijini hospitali ya wilaya hatuna, vituo vya afya hatuna, zahanati tuna maboma, halafu wanatupa mgao wa kufanana na Majimbo ya Makao Makuu ya Wilaya, wanatupa mgao wa kufanana na Manispaa. Hili jambo ni lazima waliangalie vizuri. Kama Serikali inataka kuboresha maisha ya wananchi wa vijijini, lazima iwekeze sana kwenye vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie hata kwenye elimu ni hivyo hivyo na nimeona wanatupa fedha ya kujenga shule moja moja katika kila jimbo kwa nchi nzima. Nawashukuru sana na tunaenda kujenga shule 1,000 nchi nzima.

Naomba mgao huu wauangalie, kuna majimbo ya mjini yenyewe yameshamaliza shule, sasa wanataka wajenge maghorofa wakati kwenye kata zetu tuna kata saba hazina shule kabisa. Kwa maana hiyo, wakitupa shule moja maana yake tutegemee mpaka miaka saba ndio tumalize kujenga hizi shule, haiwezekani! Watupe kulingana na mahitaji, tuna mahitaji makubwa ya ujenzi wa shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi jimboni kwangu Kata nane hazina sekondari za kata. Kwa hiyo wakinipa moja na mwakani wakanipa moja, nahitaji nikae miaka nane humu Bungeni ndio nikamilishe zile shule, wakati tumepata shule 1,000, kwa hiyo watuangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine katika hizi fedha wanazotoa, wanatoa fedha hizi wanatoa pamoja na fedha za kwenda kusimamia mradi wenyewe. Mheshimiwa Ummy nimemwona, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kwanza nampongeza dada yangu, anafanya kazi nzuri, ameanza vizuri. Nimeona anafuatilia mapato ya halmashauri, kule na penyewe kuna mchwa, lazima tukubaliane kule kuna mchwa. Tena kula wanatafuna sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe mfano, Mheshimiwa Waziri, katika halmashauri zetu, chukulia sisi Wilaya yetu ya Igunga ambapo tumejiwekea tu tukusanye bilioni 3.1, sio fedha nyingi ni Bilioni 3.0 na hizo bilioni 3.0 tukienda tukasema tuzikusanya, asilimia 40 ya bilioni 3.0 tunapeleka kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 60 kwenye matumizi mengineyo. Tukidhibiti kwenye matumizi tunaweza tukasimamia miradi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)