Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Husna Juma Sekiboko

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuweza na mimi kuchangia kwenye mjadala huu muhimu wa bajeti ya Serikali, lakini kabla ya kwenda kwenye mchango wangu moja kwa moja nitumie fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan. Bajeti ambayo imewasilishwa mbele yetu ni bajeti ambayo imeonesha nia ya dhati ya Mheshimiwa Rais ya kuendeleza kazi ambazo zilikuwa zimeshaanzishwa katika Awamu ya Tano, lakini ya kuweka mkazo katika utekelezaji wa miradi na majukumu mbalimbali ambayo yana tija kwa Watanzania kwa kipindi hiki cha Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii pia kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Hotuba hii mbali na uwasilishaji wake ulikuwa wa tofauti na hotuba nyingine ambazo nimeshuhudia zikiwasilishwa humu, lakini ni hotuba ambayo imebeba mawazo, maono na michango ya Waheshimiwa Wabunge waliokuwa wanajadili katika kipindi chote tangu tumekuja kuanza Bunge hili la bajeti. Hii imeleta matumaini, imeleta ari, lakini inatuongezea nguvu kuona namna gani ambavyo tunaweza tukachimbua mambo zaidi kwa ajili ya kuishauri Serikali kwa imani kwamba haya ambayo tunayazungumza ndani ya Bunge Serikali inachukua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimshukuru na kumpongea sana Naibu Waziri, Mheshimiwa Masauni; wanafanya kazi nzuri na kwa kweli, combination yao watu hawa wawili, Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, itatuletea tija na matunda makubwa sana katika kipindi hiki cha Awamu ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Bajeti Kuu ya Serikali; bajeti ambayo ina mambo mawili makubwa, jambo la kwanza ni ukusanyaji wa mapato, lakini jambo la pili ni matumizi ya mapato ambayo yanakusanywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukusanyaji wa mapato chombo chetu, mamlaka ambayo tunaitumia katika ukusanyaji wa mapato nchini ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), lakini katika michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi ambao walikuwa wanazungumza tangu mjadala huu umeanza umeonesha kuna upungufu mkubwa wa watumishi TRA na hii inawezekana ndio sababu tunasuasua katika ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa ushauri kwa Serikali. Kutokana na upungufu huo wa watumishi na taarifa niliyonayo ni kwamba tuna uhitaji wa watumishi 7,406 nchi nzima kwa Mamlaka ya TRA peke yake, lakini watumishi waliopo ni 4,733 na upungufu ni 2,673, lakini ukiangalia hali halisi ya watumishi kwenye maeneo yetu hususan kwenye Wilaya zetu unakuta Ofisi ya TRA ya Wilaya ina mtumishi mmoja kwa maana ya Meneja wa TRA wa Wilaya au wawili, yeye na msaidizi wake jambo ambalo kwa kweli linazorotesha sana ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya nyingine ina kata zaidi ya 30, lakini yuko meneja mmoja tu, I mean mtumishi ambaye ni Meneja tu wa TRA, ndio anafanya kazi ya kutoa elimu, kukagua, kutoa tathmini, kwenda kuhamasisha na kuelimisha watu watumie mashine za EFD na kadhalika ili aweze kukusanya mapato. Sasa ili tuweze kusaidia Serikali najua kwamba, hatuna uwezo wa kuwaajiri watu 2,600 TRA peke yake kwa wakati mmoja na wala simaanishi kwamba, hao watu wasiajiriwe, lakini nafikiri tunaweza tukaitumia Mamlaka ya Serikali za Mitaa tukaondoa hili ombwe la upungufu wa watumishi katika ukusanyaji wa mapato kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mfumo wetu wa utawala nchini umeanzia kwa Mjumbe wa Nyumba Kumi, umeenda kwenye Kitongoji, unaenda kwenye Kijiji, unakwenda kwenye Kata mpaka kwenye Wilaya na ngazi ya Taifa. Na huko kote kuna viongozi na watumishi wa Serikali, viongozi ambao wangeweza kutoa taarifa za ukusanyaji wa mapato wakazipeleka kwa Meneja wa TRA wa Wilaya akapata taarifa ni duka gani jipya limefunguliwa, ni duka gani limefungwa, ni kwa namna gani watu wanakwepa kodi. Tayari ikawawezesha hawa watumishi wachache wa TRA kuweza kufanya kazi yenye ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi ningeishauri sana Serikali tuwatumie watendaji wa kata, tuwatumie watendaji wa vijiji, tuwatumie Wenyeviti wa mitaa, tuwatumie Wenyeviti wa vitongoji na wajumbe wa nyumba kumi-kumi na namna nzuri ya kuwatumia ni kuwatengea kibajeti kidogo tukawawezesha sasa kama ambavyo tumeona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri kwamba wanakwenda kulipa posho ya madaraka kwa Watendaji wa Kata. Tushuke twende mpaka kwa Mtendaji wa Mtaa au wa Kijiji, twende mpaka kwa Mwenyekiti wa Kijiji na kitongoji watusaidie na tuwa-task hii kazi ya kutoa taarifa ya walipa kodi, ili kurahisisha hili suala la ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna ombwe kubwa kati ya Serikali za Mitaa na Mamlaka ya Mapato – TRA. Unakuta wanakwenda kufanya ukaguzi eneo hilo hilo moja, pengine duka hilo hilo moja watu wa TRA, lakini hawezi kukagua lile jambo ambalo limekuwa tasked kwa halmashauri labda ya Wilaya au ya Jiji. Akienda mtu wa jiji ameenda kukagua labda anataka kwenda kukusanya service levy, lakini hana muda kabisa wa kuangalia kama je, kodi ya mapato imekwenda TRA. Sasa hawa watu tukiwa-link ikawa mtumishi wa Halmashauri akienda kukagua masuala yanayohusu Halmashauri akapewa na kazi ya kuangalia masuala mengine ya Serikali kwa sababu hawa wote ni watumishi wa Serikali, wote wanalipwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wote wanawajibika kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nini watengane? Kwa nini wasifanye hizi kazi kwa pamoja kukapatikana mazingira ya ufanisi mwisho wa siku tukapunguza hili ombwe la watumishi katika Mamlaka ya TRA?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huku TRA zamani tumezoea, ukimuona mtu anafanya kazi TRA utaona ana gari zuri, anaishi kwenye nyumba nzuri, tofauti na mazingira yalivyo sasa. Maeneo ya pembezoni hawa watumishi wa TRA wanaishi kwenye mazingira magumu mno, nyumba zimechakaa, hazijakarabatiwa, magari yamechakaa na ndio ambao tunawategemea waende wakakusanye mapato kwa ajili ya Serikali yetu. Kwa hiyo, ningeomba sana na wao waweze kutizamwa, nyumba zao ziweze kufanyiwa ukarabati maeneo ambayo hamna nyumba waweze kujengewa, ili waweze kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo ningependa kulizungumza leo ni upelekaji wa fedha kwenye maeneo ya matumizi. Huko nyuma palikuwa na maelekezo na ninashukuru kwa kweli ilitekelezwa vizuri kwenye baadhi ya maeneo kwamba ikiwa mradi unajengwa kwenye shule, basi fedha ya mradi hata kama ni ya darasa iende moja kwa moja kwenye shule husika ili kuondoa ile process ndefu ya kuweza kutoa fedha kwenda kwenye ngazi moja iende kwingine iende kwingine mpaka ikifika kule inachukua muda mrefu sana. Sasa ili kupunguza hiyo bureaucracy hela iende moja kwa moja kwenye eneo la matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeweza kufanya hivyo kwenye shule, tumeweza kufanya hivyo kwenye zahanati, lakini tuna shida kwenye hela ya matumizi mengineyo (OC). Ofisi za Wakuu wa Wilaya hawapelekewi fedha moja kwa moja mpaka ipitie kwa Katibu Tawala wa Mkoa. Fedha yenyewe unakuta ni milioni tano, milioni sita, milioni mbili, imeshindikana kwenda kwa Accounting Officer wa wilaya pale (DAS), inapita kwa Accounting Officer wa mkoa, ana miradi mingapi ya kuweza ku-manage hiyo fedha? Ana watu wangapi anaokwenda kuwalipa hiyo fedha? Lakini hiyo fedha ingeenda moja kwa moja ingerahisisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Niliwahi kuuliza humu swali pia kwamba, kuna haja gani ya fedha ya matumizi ya kituo cha polisi, Mkuu wa Polisi wa Wilaya, ipitie kwa Mkuu wa Polisi wa Mkoa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni urasimu ambao kimsingi hauna sababu, kwa sababu yule aliyeko pale kwenye kituo cha kazi akiipata ile fedha kwa wakati maana yake ataweza kutatua changamoto zake kwa wakati. Na ndio sababu tunaona maeneo mengine unampigia OCD kuna ajali, kuna janga, kuna nini, anakwambia sina mafuta, mipira ya gari imechakaa, fedha bado haijaja, lakini fedha imepelekwa mkoani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa mujibu wa taratibu za wenzetu hawa huwezi kum-question RPC kwamba niletee fedha ukiwa wewe ni OCD uko chini yake kwa mujibu wa taratibu zao za kijeshi. Sasa ili kuondoa huo urasimu wote ni vyema sasa Mheshimiwa Waziri tuone umuhimu wa kupeleka fedha hizi moja kwa moja kule kwenye maeneo ya matumizi ili kuwasaidia wenzetu kuweza kufanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini napongeza pia namna ambavyo mmeamua kupeleka fedha za Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata, lakini Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie, sio jambo jipya sana huko nyuma limefanyika, lakini halijafanyika kwa usahihi sana kwa sababu zinapitia kwenye ofisi nyingine. Mimi nikiwa DAS unaniletea milioni tatu, unaweza kukuta pale umepita mwenge umeniachia deni, wamepita pale viongozi wameniachia deni, sikumbuki kupeleka fedha kwa Afisa Tarafa naitumia palepale Wiayani inaisha, lakini kama mmeipeleka moja kwa moja kwa Afisa Tarafa maana yake ni kwamba, siwezi kwenda kuichukua kule tayari atakuwa amepata ile haki yake na kazi zake zitafanyika vizuri. (Makofi)

Kwa hiyo, nashauri sana fedha ziende huko moja kwa moja badala ya kupitia kwenye mamlaka nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo ningependa kulizungumza; siasa,uendeshaji wa nchi kwa akili yangu ya kawaida kabisa kila jambo linakwenda kwa wakati. Siasa yetu ya sasa kwa kauli mbiu ya mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan tunaendeleza kazi ambazo tulizianza katika Awamu ya Tano, lakini kwa namna ambavyo mama anaenda kufanya kazi anataka kuacha legacy kama mama wa kwanza kuiongoza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa mwenyekiti, ili aweze kuweka legacy lazima tumsaidie katika eneo la maji tufanye vizuri, bajeti ya maji iende vizuri akamtue mama ndoo kichwani. Lazima tumsaidie katika eneo la afya, vituo vya afya ambavyo vimejengwa vipelekewe vifaa tiba, akinamama waweze kujifungua salama na wajifungue kwa mazingira ambayo yanatakiwa, lakini lazima tupeleke bajeti na ifike ile ambayo inalenga kuwawezesha akinamama kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiyafanya haya mambo matatu tutakuwa tumemsaidia mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, kuacha legacy katika nchi hii katika muda wake wote ambao atakuwa amekuwa madarakani. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)