Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nivunje utaratibu kidogo, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Ameir Mohammed, kwa uamuzi wake wa busara, kwa leo kutamka ndani ya Bunge lako tukufu, kwamba anakuwa mwananchi na hii ifungue milango kwa waheshimiwa wabunge wengine waweze kufuata mfano mzuri kama huu na namuombea Mwenyezi Mungu majaze busara zaidi Mheshimiwa Ameir Mohammed. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo...

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Taarifa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Rashid Shangazi.

T A A R I F A

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayezungumza hapa ndio Mwenyekiti wa wabunge wa Simba hapa mjengoni, na katika makabrasha yetu hatujawahi kuwa na mwanachama anayeitwa Ameir Abdalla Ameir, ahsante. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba taarifa unaipokea.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ananipotezea muda na naomba uulinde muda wangu ndio kwanza naanza, sasa ndio naanza. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi ambayo nitaitumia vizuri, katika kuhakikisha nachangia vizuri katika hotuba hii ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, na ninaweza kusema katika historia ya hotuba za bajeti, hotuba ambayo imewagusa wananchi kwa kiasi kikubwa sana ni hotuba hii, imejaa ubunifu na inanipelekea nimuombe Mwenyezi Mungu amjaalie Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, yeye na timu yake. Mawaziri hawa wakiwemo ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na wengine wote wanaomsaidia, Mwenyezi Mungu awajaalie afya, uzima na akili nyingi sana za kuwa wabunifu kama walivyofanya safari hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia katika eneo moja, na eneo lenyewe ni sera na mikakati ya kuongeza mapato na kama ilivyo katika Ibara ya 25 ya hotuba, kwa wale ambao wanacho hicho kitabu naomba wapeleke hapo macho yao. Na nikipata muda nitagusia jimboni kwangu Kinondoni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaenda kuchangia nawaombeni siku ya Jumanne, wabunge wote tuwemo ndani ya Bunge hili tuipigie kura ya ndio bajeti hii. Kama alivyosema ndugu yangu Mheshimiwa Shangazi kwamba Wabunge wote wawemo ndani ya ukumbi, siku ya Jumanne basi Mwenyezi Mungu awajaalie wote wawepo humu ndani, ili bajeti hii ipate kupigiwa kura ya ndio pamoja na wenzetu walio upande ule kule walio wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kusoma azma ya Serikali ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa kuweka mazingira rafiki kwa mlipa kodi, ili wawavutie wawekezaji na vile vile kundi la wafanyabiashara wadogo na wakati, ili waweze kupanua wigo wa kodi ni jambo zuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naisoma hii pamoja na ile azma nyengine ya kujenga uchimu shindani wa viwanda kwa maeneleo ya watu. Haya ni madhima mawili makubwa sana ambayo Serikali lazima iangalie kwa macho ya uangavu kabisa. Kwa sabau gani, kwa sababu hivi vitu vinakinzana na hali ya sheria zilizopo nchini pamoja na sheria za kodi hazionekani kabisa kuipa support hiyo azma ya Serikali ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeo ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niwape mifano miwili mikubwa kabisa, na hii inahusu watanzania ambao wamejaribu kujenga viwanda vya madawa hapa Tanzania, changamoto zao wanazozipata ukilinganisha na dawa zile ambazo zinazotengenezwa nje na kuletwa nchini, sasa hivi hapa Tanzania dawa ambazo tunazitegemea sana ni dawa zinazotoka nje, na kulifanyika utafiti August mwaka 2019, yupo bwana Dikson Pius Wande na wenzake, walifanya utafiti juu ya mahitaji ya dawa katika nchi hii, na wakaona kwamba katika mwaka 2021, dawa ambazo zinakwenda kuingizwa Tanzania ni karibu zenye dhamani ya dola milioni 906, sawa na katibu trilioni 2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo utakuta hizi ni dawa zinazoletwa na private sector peke yake, achilia zile dawa ambazo zinaletwa na Serikali. Sasa ukiangalia utakuta kwamba wanaojenga viwanda vya madawa nchini, wao wanapata misukosuko mikubwa sana kwa kuwa hali ya sheria za kodi haimpi nafuu mjengaji wa viawanda vya madawa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii utashangaa cough syrup, juzi nimenunua cough syrup kutoka Bangladesh shilingi 3,000 lakini cough syrup hiyo hiyo, ya in gradients hizo hizo ya Tanzania ni zaidi ya shilingi 3,000. Kwa kuwa tuna kasumba ya kuona kwamba dawa za nje ndio nzuri tunakimbilia kununua zile ambazo ni nafuu vile vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikwambie kitu kimoja, kwamba watafiti wale wanasema, katika mwaka mmoja unaokuja mahitaji ya dawa yataongezeka kwa asilima 28, maanda yake tunawasaidia wenye viwanda vya nje na wafanya biashara wa nje, kuendelea kuvuna fedha za Tanzania, wakati Tanzania tunaweza kutoa tukatoa unafuu mkubwa kwa wajengaji wetu wa viwanda, ili hata ile azma ya Serikali inayosema kwamba watu wajenge Tanzania ya viwanda iweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo mtu ambaye anatengeneza cough syrup Tanzania, pengine atahitaji kuleta zile chupa, angalia hapo akileta ile chupa anaambiwa lazima aweke na label moja kwa moja huko inakotoka, label zenyewe ni za karatasi, zikija hapa zinaingiwa katika mifumo ya kusafisha chupa zile, lebo zinaharibika, na wanaambiwa hivyo ili wapate msamaha wa VAT lazima watimize masharti kama hayo, sasa masharti gani hayo, tuweke masharti ambayo yataidia viwanda vyetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu yupo katika Serikali ambayo ni Sikivu, na wewe bahati nzuri Mwenyezi mungu amekujaalia kuwa mwananchi, na wananchi ni wasikivu. Hebu sikiliza kilio cha wananchi ambao wanajenga viwanda Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba twende sehemu nyengine, katika masuala yanayohusiana na unafuu wa kufanya biashara, wafanya biashara hasa upande wa TRA. Hebu angalieni dispute resolution ya makodi haya, Kamishna anapoandikiwa kwenye dispute resolution kama ilivyo kwenye sheria ya TAA katika part 7, utakuta kwamba kuna mlolongo mkubwa sana wa kuondoa haya matatizo ambayo yanatokana na decisions zinazofanywa na Kamishna, na zenyewe zinasababisha mashauri yazidi kule kwenye tax board appeal inafanya tukose kupata fedha za Serikali kwa sababu mashauri hayaendi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningekuomba katika hili Serikali ifanye utafiti iweze ikaangalia sheria zile kinzani ambazo hazitupi manufaa katika sera yetu ya Tanzania ya viwanda uzifanyie marekebisho, na hazi ni sheria zote mifumo ya licenses, mifumo ya usimamizi na mifumo ya kodi inahitaji kuangaliwa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niende Kinondoni. Nataka niseme kwamba bajeti hii imetufanyia kazi kubwa sana, na namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuja na bajeti ambayo wabunge wengi wameisifia, hasa upande pale tulivyopewa shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo. Nataka niwaambie milioni 500 kwangu hazitajenga lami lakini kuna barabara nyingi ambazo nitakwenda kuzitengeneza kwa kiwango cha changarawe, ili ziweze kupitika. Wananchi wa Kinondoni wanaonisikiliza, barabara ya Wibu, barabara ya Ufipa, barabara ya Chogo, barabara ya Wakulima, barabara ya Gulwe, Mkalama, Lalago, Sekenke, Mkunguni, Kiwanjani, Mapera kote huko tunakwenda kuzijenga hizi, angalieni bajeti ya wananchi inavyo kwenda ufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupongeze wewe pamoja na Serikali, kwa kuliona suala la kulitengeneza mto Msimbazi ambao ni kero kubwa sana, Dar es Salaam, na nataka niwambie kwa kutengeneza mto msimbazi sio tu Kinondoni inakwenda kufaidika Dar es Salaam nzima inakwenda kufaidika, kwa sababu mto Msimbazi ukifurika magari hayapiti Morogoro road, sasa hivi magari yatakuwa na nafasi ya kwenda kupita, daraja itajengwa, wananchi wa Kigogo, Mzimuni, Magomeni wote wanakwenda kupata nafuu ya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni fedha nyingi sana ambazo Serikali imeziweka, kutokana na hili nataka niwaambie wananchi wa Kinondoni kwamba wamuombee Mheshimiwa Rais, wamuombee Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwiguli pamoja na Serikali nziama, kwa sababu tayari..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante!

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, aaah! Unanitoa raha lakini nikushukuru sana na naunge mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)