Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uteuzi mzuri wa Baraza la Mawaziri, wameteuliwa majembe ambayo kwa hakika tunaamini yatatufikisha katika safari yetu hii ambayo tunayo. Niwashukuru tena kwa mara nyingine wananchi wangu wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa kuniamini na kunileta humu na mimi ninaamini kwamba sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla kwa kazi nzuri wanayofanya katika Wizara hii kwa kuimarisha hospitali yetu kubwa ya Taifa, Hospitali ya Muhimbili lakini Hospitali ya Saratani ya Ocean Road. Kuna changamoto kadhaa ambazo tunatakiwa tuzione na Serikali ichukue hatua za haraka kuhakikisha wagonjwa wote hawaendi katika hospitali hizi kubwa na ili wagonjwa wasiende katika hospitali hizi kubwa lazima tuimarishe hospitali za kanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya 2011/2012 hivi, Serikali ya Awamu ya Nne kuna hospitali ilizipandisha hadhi kuwa Hospitali za Rufaa ikiwemo Hospitali ya Mtakatifu Gasper ya Itigi ambayo inatoa huduma kwa wananchi wa Itigi lakini kwa Kanda nzima ya Kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ile ina gharama kubwa sana kutokana na Serikali kuachia wananchi kuhudumiwa kwa gharama za Wamisionari wale ambao kwa wakati fulani kule nyuma walikuwa wakipata dawa kutoka kwa wahisani wao lakini baadaye Serikali iliwazuia wakawa wanatakiwa wachukue dawa kutoka MSD, ruzuku wanayopata ni kidogo, matokeo yake hospitali ile imekuwa na gharama kubwa sana sasa na itapelekea hospitali hizi kubwa za Muhimbili, KCMC na nyingine kupata mzigo mkubwa kwa sababu hizi Hospitali za Kanda na za Rufaa hazifanyi kazi vizuri. Gharama zile ni kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni katika uchaguzi uliokwisha. Wananchi wale ni waaminifu walikipa chetu Chama cha Mapinduzi kura nyingi sana na Mheshimiwa Rais walimpa kura nyingi lakini moja ya ahadi yake ilikuwa kwamba atatoa ruzuku ya Serikali kwa Hospitali ile ya Mission ili iwasaidie wananchi wa maeneo yale ikiwemo wananchi wa Jimbo langu la Manyoni Magharibi hususani wananchi wa Mji wa Itigi na vijiji ambavyo vinaizunguka takribani kata 13 ikiwemo Wilaya nzima ya Manyoni watu wanakimbilia pale wanaposhindwa katika Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kupeleka Madaktari Bingwa pale lakini kuongeza ruzuku na kutoa mgao kutoka MSD. Tukilifanya hili tutakuwa tumewasaidia wananchi wa Jimbo langu na watakuwa wameendelea kumuamini Mheshimiwa Rais wetu na ahadi zake zitakuwa endelevu kwa sababu aliyasema haya katika mkutano wa hadhara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili wagonjwa wafike katika hospitali hizi kubwa wanatokea katika vituo vya afya. Katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi kuna kata 13 lakini tuna vituo vya afya viwili na kimoja ndiyo tuko katika kuhangaika kujenga na mafungu yenyewe ndiyo haya ya taabu. Kwa hiyo, niombe sasa Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kupitia Mawaziri hawa, madaktari na maprofesa watusaidie sasa wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi kwa kuhakikisha tunajenga kituo cha afya kwa kila kata lakini na hospitali kila kijiji na sisi tutasaidia pale ambapo tutapaswa kuwajibika katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna janga kidogo hapa katika vituo vidogo hivi vya zahanati za vijiji hazina matabibu wale kwa maana ya Clinical Officers hawapo kabisa. Baadhi ya zahanati kama Gurungu, Njirii, Ipande, Kitopeni, Ukimbu na hata Kintanula. Kuna nesi mmoja huyo huyo ndiye anaenda kukuandikia dawa, anakupatia tiba na baadaye anakutolea dawa. Sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuyafanya haya yawe mepesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya ahadi zetu katika chaguzi ilikuwa ni pamoja na kusogeza huduma hizi lakini kusaidia wazee na kwamba watapata matibabu haya bila usumbufu, lakini bure. Hii imekuwa changamoto kubwa, matibabu ya bure yamekuwa na udhia sana kwa wazee hasa wanapofika hospitali. Kama nilivyokwishatangulia kusema mimi katika Jimbo langu watu wangu wanatibiwa katika Hospitali ya Wamisionari. Jambo hili wamekuwa hawalitambui sana, sasa si vibaya Serikali ikaingilia kati iwasaidie wananchi wale ili wazee nao wanufaike na mpango huo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine ni bima ya afya, kuna huu Mfuko wa CHF umekuwa na changamoto nyingi. Wakati mwingine watu wanachangia zile fedha lakini anapofika katika kituo cha afya au zahanati anakuta dawa hazipo. Niombe sasa juhudi za makusudi kwa Serikali hii kushirikiana na TAMISEMI, Wizara ya Afya wayafanye haya yawe mepesi ili wananchi wetu kule vijijini waendelee kuwa na imani hii ambayo wanayo sasa ya kutuchagua sisi viongozi tunaotokana na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo nimetaka kulizungumzia kidogo, tumeweka nguvu sana kwenye matibabu ya moyo katika hospitali hizi kubwa. Niipongeze Serikali kwa juhudi hizi ilizochukua kuhakikisha sasa magonjwa haya makubwa yatatibiwa katika Hospitali yetu ya Taifa. Hata hivyo, kuna janga lingine la magonjwa haya yasiyoambukiza ukiwemo ugonjwa wa kisukari, tumekuwa hatuchukui hatua za kutosha na sasa watu wengi wakiwemo Waheshimiwa Wabunge ni wagonjwa wa ugonjwa huu wa kisukari. Ni vyema sasa Serikali nayo ikatafuta matabibu wazuri, Madaktari Bingwa aidha watu wetu wakaenda kusoma kwa nchi ambazo tayari zinaonyesha kwamba zina maendeleo mazuri juu ya tafiti na kugundua tiba nzuri ya magonjwa ya kisukari. Watu wetu wamekuwa wakifa kwa kupewa dawa ambazo pengine si sahihi au utaalamu ambao hautoshi. Niiombe Serikali yangu Mawaziri hawa ambao mimi nawaamini kwa asilimia mia moja kutokana na ushirikiano wanaotupa sisi Wabunge basi na hili jambo walichukue, walifanyie kazi ili baadaye ugonjwa huu usiwe tatizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki kupigiwa kengele, naomba kumalizia hapa na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.