Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ameir Abdalla Ameir

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

House of Representatives

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi, ambaye leo ameniwezesha kupata afya njema nami kuwa miongoni mwa Wabunge watakaochangia hotuba hii ya bajeti ya mwaka 2021/2022. Napenda kumpongeza sana Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Fedha na Naibu wake, kwa bajeti hii ambayo imeweza kupanga matumizi yake kwa kuyapa kipaumbele maeneo muhimu ambayo yanakwenda kukuza uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo, bajeti hii haijaacha pengo hata moja. Hii ni bajeti ya wananchi, kwa maslahi ya wananchi na kwa neema ya wananchi wa Tanzania wote. Bajeti hii imegusa wananchi wote; imegusa wakulima, wavuvi, wajasiliamali, watu wa makundi maalum, walimu, waendesha bodaboda, akina mama kwa asilimia kubwa sana, mama ntilie na kadhalika. Kwa hiyo, naipongeza sana bajeti hii kwa asilimia kubwa sana na Inshaallah Mungu atatuweza kwamba Taifa letu la Tanzania litapiga hatua kubwa katika maendeleo ya uchumi katika sekta mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nitachangia katika maeneo machache sana kwa sababu maeneo mengi Waheshimiwa Wabunge wameyazungumza kwa ufafanuzi mzuri na kutoa mapendekezo mazuri, na ushauri mzuri ambao una manufaa makubwa kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mimi nitatoa ushauri nikijikita zaidi kwenye ongezeko la kodi katika suala zima la utalii wa watu wenye mahitaji maalum; vile vile nitaongea kuhusu suala la umuhimu wa kuwekeza viwanda vyetu hususan katika suala la mbolea na jambo lingine ni suala la ajira kupitia lugha sanifu ya Kiswahili na mwisho nitazungumzia kuhusu mahusiano mazuri baina ya sekta ya kilimo na sekta ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya utalii kuna jambo hatujaligusa kwa undani zaidi na tumeliacha kidogo, lakini kama Serikali italitilia mkazo na kulipa kipaumbele suala hili basi litasaidia sana kuongeza thamani na ongezeko la mapato katika utalii wetu. Nalo ni suala la kujikita katika utalii wa watu wenye mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye mahitaji maalum sasa hivi duniani wanafika takriban bilioni tatu. Ni robo tatu nzima ya population ya watu duniani. Kwa maana hiyo, Serikali kama tutajikita zaidi huku, basi Tanzania itakuwa ni nchi ambayo inapokea watalii mbalimbali duniani katika kundi hili na kwa asilimia kubwa itaongeza thamani kubwa ya pato la nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kukibidhaisha na kufanya lugha ya Kiswahili kama ni sehemu ya ajira. Kiswahili kinapaa duniani; Kiswahili kinasomeshwa katika Vyuo Vikuu mbalimbali duniani hivi sasa, lakini cha kushangaza maeneo mengine, Wazungu kwa Wazungu ndio wanafundisha hicho Kiswahili kwa sababu sisi hatujapanua zile fursa za kufika katika hayo maeneo mbalimbali tukakieneza Kiswahili na walimu wetu ambao wanasomesha Kiswahili Tanzania kule Zanzibar na Tanzania Bara wakapata fursa hii kwa undani. Kwa hili sasa, namwomba sana Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi (ameshageuka) ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, atutengenezee mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani sana, nimekosea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri anahusiana na mambo ya Nje, aweze kututengenezea mazingira kupitia balozi zetu ambazo zinatuwakilisha nchi za nje. Kila balozi atengeneze fursa za lugha ya kishwahili kwa watanzania jamani, naomba sana tusaidie sana kwa kila balozi hata kama hakuna mazinga hayo lakini atengeneze kuhakikisha kwamba walimu wanaofundisha kiswahili Tanzania wanapata fursa katika balozi zetu hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine napenda kuhangia katika sekta ya maendeleo ya kilimo na viwanda, hatuwezi kuendelea katika sekta ya viwanda bila ya kufanya mageuzi na mapinduzi ya sekta ya kilimo. Bajeti hii inakuja na mageuzi hayo, bajeti hii imeelekeza wakulima wazilishe kwa wingi mazao ya biashara na mazao ya chakula, tukizalisha kwa wingi mazao ya chakula kwa wingi, maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba tutaongeza population ya idadi ya watu, na tukiongeza population na idadi ya watu maana yake tutakuwa na soko la uhakika la ndani ya nchi na bidhaa zetu zitauza ndani ya nchi na nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nilizungumzie katika suala la kuwekeza katika viwanda vya mbolea. Tanzania tumejaaliwa kuwa na aina ya madini fulani ambayo yanatumika katika kutengenezea hizi mbolea ambazo nchi nyengine hakuna, na madini haya tukiyatumiwa viwili ambayo yanatumiwa katika mikoa miwili tu, basi ni vyema tukawa na madini haya ambayo yanatuwezesha kuzalisha mbolea zetu sisi wenyewe, na kuondoa ule utegemezi mkubwa wa kuzalisha au kuagiza mbolea kutoka nchi za nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na mbolea zetu wenyewe hapa nchini, basi sekta ya kilimo itakuwa na kuimarika kwa hali ya juu zaidi. Lingine niipongeze sana bajeti hii na Serikali kwa ujumla, kwa kuondoa tozo ya nyasi bandia, jambo hili linaisababishia nchi yetu kukuza sekta ya michezo, hususan mchezo wa mpira wa miguu, na leo hii nataka ni– declare interest, kwamba mimi ni mfuasi wa Simba tangu miaka 12. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bajeti hii ya kaka yangu Mwigulu Nchemba, bajeti ya wananchi, kwa maslahi ya wananchi, kwa ajili ya wananchi, natangaza rasmi ni mwana Yanga rasmi. Natangaza rasmi kwamba i leo ni mwana Yanga rasmi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwamba, aah! Ukitoa taarifa unanitatiza kidogo niache. Eneo lingine ni kwamba tuna miradi ya kimkakati na nashukuru kwamba mama bajeti imetuhakikishia kwamba hakuna mradi wa kimkakati hata mmoja utakaosita, miradi yote ya kimkakati itaendelezwa, namshukuru mama na naishukuru bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri hapa katika miradi ya kimkakati, tuwekeze rasilimali watu ambao wataweza kuiendesha vizuri miradi hii, lazima tuhakikishe tunasomesha vijana wetu, na tunasomesha raia wetu wa Tanzania katika zile sekta au taaluma ambazo zina ugumu ndani yake, ili kupunguza utegemezi wa kuajiri wataalam kutoka nje ya nchi mara kwa mara, na tuwe na waalamu wetu kwa asilimia zote ikiwezekana kama siyo asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache naipongeza sana naiunga mkono bajeti hii na ninaimani leo na mimi nitaalikwa chako ni chako, ahsante sana. (Makofi)