Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ambaye amenipa afya njema na kuweza kusimama kwenye hili Bunge Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Fedha pamoja na viongozi wote wa Wizara kwa namna ambavyo wameiongoza na kusimamia bajeti hii ya Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais katika Taifa letu hili la Tanzania. Mheshimiwa Rais wetu ni mama msikivu, mwenye busara, ana hekima, ni mama ambaye anastahili sifa zote. Napenda kuwashukuru Watanzania wote kwamba wamemkubali sana mama tangu pale ambapo ameapishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia bajeti hii na kuipongeza sana vile ambavyo imeandaliwa hasa kwenye kipengele cha vijana wetu wa bodaboda. Naipongeza sana kwani wameondola mzigo mkubwa sana maana faini ya shilingi 30,000/= ilikuwa ni kubwa sana. Pamoja na kuipongeza kwa kazi nzuri hii waliyoifanya, napenda sana kuishauri pia Serikali, vijana ni nguvu kazi ya Taifa, tunawategemea sana na tunawapenda. Napongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwani ilifanya utaratibu wa kuondoa viroba ambavyo viliendelea kulinda uhai wa vijana wetu wa bodaboda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kwa yafuatayo: kuhusu watu wa Usalama wa Barabarani, nilikuwa napenda kusimamia haya. Vijana wetu wa bodaboda kama nilivyoanza kwa kusema tunawapenda, hatutaki kuwapoteza. Naomba sana ufuatiliaji wa sheria na taratibu za kupita barabarani hizi bodaboda zetu. Bodaboda zilizo nyingi zinapita barabarani zikiwa hazina taa ya breki ya nyuma ambayo inaonesha kwamba ile ni bodaboda inapita. Pia usiku wakati fulani unapishana na bodaboda haina taa yoyote, ukizingatia zenyewe hazina sehemu ya kuweka reflector. Sasa hiyo ni hatari sana ambayo inaweza kupoteza uhai wa vijana wetu hawa wa bodaboda. (Makofi)

Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Jeshi la Usalama wa Barabarani kuwaita vijana wa bodaboda kuweka vikao na wao kuwaelimisha, kuwapa semina, namna ambavyo sheria za barabarani zinavyotakiwa kuwa. Naliongea hili maana kipindi cha kwanza bodaboda zilivyokuwa zinaanza, kulikuwa na utaratibu; wanakuja wilaya kwa wilaya, wanakalishwa vikao vijana wa bodaboda kuwapa elimu. Hapa katikati bodaboda zimeingia kwa wingi sana, sijawahi kuona semina inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, naomba tuzijali sana afya za hawa watoto wetu. Hawa vijana hawavai sana helmet ambayo inazua kupasuka kwa kichwa endapo watapata ajali. Pia kuna kitu kinaitwa chest coat la kuziba kifua, havijazingatiwa kabisa. Vijana wengi wanaendesha bodaboda bila kukinga kifua. Sasa imeanza kuleta athari ambapo hofu yangu tutapoteza vijana wengi katika Taifa letu hili Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewashuhudia vijana wanne ambao waliathirika na mapafu. Wengine walifanyiwa upasuaji wakapona, lakini wawili walipoteza maisha. Sasa hapo ni hao nimefanikiwa kuwaona, ambao hatujawaona! Hili naliona ni tatizo kubwa sana ambalo tunatakiwa tuwasimamie vijana wetu wa Taifa hili la Tanzania. Pia napenda kuishauri Serikali, naipongeza kwamba wamepunguza hizo faini, lakini vituo vingi vya Polisi vina bodaboda nyingi sana. Nilikuwa naomba sana Serikali yetu hii ni sikivu, hao watu ambao bodaboda zao zimekamatwa wawaruhusu kwenda kufuata bodaboda zao ambazo hazina makosa ya jinai wakalipe faini ya hiyo hiyo shilingi 10,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, wakati fulani nilikuwa nimechangia kuhusu elimu kwa ajili ya mlipa kodi wa Tanzania. Naomba sana, narudia kusema, elimu ya mlipa kodi wa Tanzania ni muhimu sana. Naomba kwa mara nyingine, elimu itolewe kuanzia Shule za Msingi, Sekondari, Vyuo na Vyuo Vikuu ili vijana hawa wanapokua siku zinavyozidi kwenda, inakuwa inawajenga kwamba kulipa kodi ndiyo uendeshaji wa Taifa letu ya Tanzania. Hivyo napenda sana kuliombea hili lizingatiwe. Naomba sana hawa viongozi wa TRA kuweka mikutano na vikao na wafanyabiashara kuwapa elimu na semina ili wasione kwamba wanaonewa katika kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongee lifuatalo; kipindi cha Awamu ya Tano, naomba sana mpango na hali ile ya Awamu ya Tano iendelee hata hii Awamu ya Sita. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan. Sisi ni wanawake, naomba sana kasi ile ile iliyokuwa ya Awamu ya Tano iwe ni hiyo hiyo mpaka kipindi hiki cha Awamu ya Sita. Ofisi zote za Umma za Serikali zinaongozwa kwa kutumia Ilani ya Chama cha Mapinduzi na ofisi zote zinazo. Naomba Watumishi wa Umma tusilegelege, ile kasi na mori ya kufanya kazi kama ilivyokuwa Awamu ya Tano iwe hivyo hivyo na awamu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi baada ya Bunge la Bajeti hili kwisha narudi Mbeya, naomba ofisi vile ambavyo alikuwa akijituma akijihimu asubuhi kwenda kazini na iwe hivyo. Nitapita maofisini kuangalia kama mambo yanakwenda sawa. Naomba sana, vile ilivyokuwa, mtu kama hajafika ofisini kwa wakati, maana yake kipindi cha nyuma ilikuwa tukifika unasubiri, mtu anaambiwa bosi sasa hivi ametoka amekwenda breakfast. Unasubiri, ikifika saa 5.00 anasema hajarudi, basi nifanye kazi mbili tatu, unarudi saa 8.00, wanasema ooh, amekwenda lunch. Naomba hilo lisirudiwe tena . Vile ilivyokuwa Awamu ya Tano na iwe hivyo mpaka sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba sana; amani na upendo uliokuwepo Awamu ya Tano uendelee na sasa.

Maana tumesikia sasa vibaka wanaanza, wizi wizi unaanza. Tanzania inajengwa na sisi wenyewe Watanzania. Haya ninayoongea ninamaanisha. Nalipenda sana Taifa letu la Tanzania, nawapenda sana Watanzania wote na ninaomba amani. Utendaji kazi ndiyo iwe ngao yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)