Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa siku ya leo. Awali ya yote niipongeze sana Serikali kwa kuleta bajeti ambayo ina matumaini makubwa sana kwa Watanzania. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada anazozifanya za kuijenga nchi yetu kwa vitendo, tumeshuhudia miradi mingi mikubwa ambayo anaizindua ikiwa ni muendelezo wa yale ambayo aliahidi kuwatumikia Watanzania hasa pale alipoahidi kwamba ataendeleza kazi zilizoachwa na mtangulizi wake, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ambayo imekuja ni bajeti ambayo inaweza ikatusaidia sana Watanzania. Hata hivyo tuna ushauri kwenye bajeti, yapo mambo ya msingi ambayo Serikali kupitia Wizara ya Fedha ni vyema ikayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia suala la kilimo. Watanzania wengi wanajihusisha sana na shughuli za kilimo ambazo ndizo zinawapatia kipato. Watanzania wengi wanajihusisha na shughuli za uvuvi na ufugaji. Sasa ukitaka kuutengeneza uchumi wa nchi lazima kwenye maeneo hayo ambayo yamewashika wananchi walio wengi mtenge fedha na muwezeshe kwa kiwango kikubwa. Na unapotenga fedha kwenye sehemu ya kilimo umewasaidia Watanzania wote. Kilimo kina mahitaji mengi kwanza kinahitaji uwezeshaji wa zana za kilimo, lakini pili kinahitaji mbegu za kisasa ambazo mkizisambaza wananchi watazalisha kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado, lingine ambalo Serikali halifanyi kwenye sekta ya kilimo ni kutokutafuta masoko. Mazao yanapozalishwa wananchi wengi wanakosa masoko; na wanapokosa soko tunawajengea uwezo duni wakulima. Niiombe sana Serikali, katika mwaka huu wa fedha Wizara ijitahidi sana kuhakikisha mazao yale ya biashara na mazao ya chakula mnatenga fedha kwa ajili ya kutafuta masoko ambayo yatawasaidia wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kwenye kilimo hasa cha zao la mahindi jirani zetu wa Kenya ndio wanaozalisha mbegu wanatuletea sisi. Ni kitu cha ajabu, kwamba jirani anakuzalishia mbegu, unanunua na baadaye unaenda kumuuzia malighafi kutoka kwako. Ni vyema sasa Serikali itenge fedha kwa ajili ya kukuza vituo vya utafiti, na wale wanaozalisha mbegu tuwapate kwa wingi kwenye maeneo haya ili yaweze kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linguine ambalo hatujalifanyia kazi zaidi ni kwenye sekta ya uvuvi. Mwenyezi Mungu alitujalia tukawa na Bahari ya Hindi yenye eneo kubwa sana la uvuvi. Tunaipongeza Serikali kwamba ina dhamira sasa ya kununua meli za uvuvi kwa ajili ya bahari ya hindi. Sasa tunaomba na kwenye Maeneo ya Maziwa Makuu Ziwa, Tanganyika pamoja na Ziwa Victoria tupeleke meli ambazo zitaanza shughuli za uvuvi sambamba na kutafuta mazao ya uvuvi ambayo masoko yake yatakuwa na uhakika. Hili litasaidia sana kuongeza tija kwa wananchi na wavuvi wa kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali kwa kuja na hoja ya kuongeza tozo ya simu na kuongeza fedha kiasi kwa ajili ya mafuta ili ziweze kuja kutatua kero ya Watanzania walio wengi, hasa wenye barabara za vijijini na barabara za mijini. Wakala wa TARURA ilipoanzishwa Serikali iliianzisha huu wakala tulikuwa hatujakuwa na maandalizi mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA ilipoanza haikuwa na fedha iliyotengwa kutoka Hazina, ilitegemea Mfuko Mkuu wa Barabara ambao wao walikuwa wanapewa asilimia 30 na asilimia 70 wanapewa TANROADS; na kazi yake kubwa ilikuwa ni kufanya matengenezo ya barabara kwa zile barabara zilizojengwa. Kwa bahati mbaya sana TARURA ina kilometa zaidi ya 100,000 ambazo zinahitaji kuhudumiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa amekuja na pendekezo, na tumeangalia kwenye kitabu chake; Waheshimiwa Wabunge wengi walileta mapendekezo, niombe sasa fedha itakayotokana na ukusanyaji wa hiyo tozo tunaomba uziwekee mfuko maalumu kwa ajili ya kujenga barabara za mijini na vijijini, kuliko ilivyo sasa fedha hizo ambazo mmezitenga hazikuoneshwa kwamba zitalindwa vipi, huo mfuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini kero ya Watanzania walio wengi wanaoishi mijini na vijijini ni barabara. Na Watanzania wakishajua kwamba hizi fedha tunazochangia zinaenda kutatua barabara za mijini na vijijini hata kulalamika hakutakuwepo. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri zitenge hizi fedha ili ziwe na mfuko maalum kama ulivyo Mfuko wa Barabara; itatusaidia sana kuwa na uhakika wa kutengeneza miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilikuwa napenda kuishauri Serikali ni kwenye sekta ya maliasili. Nchi yoyote ile ambayo ina watalii wengi iliwekeza fedha nyingi za kutangaza utalii. Zipo kampuni nyingi za wakala ya utalii ambazo ziko nje ya nchi. Sasa kwa nchi yetu bado hatujawekeza kwa kiwango kikubwa. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri tutenge fedha za kutosha ili tuwezeshe mawakala wa kutangaza vituo vya utalii nje ya nchi. Hii itatusaidia sana kuwa na idadi kubwa ya watalii kuliko ilivyo sasa. Nchi yetu ina vivutio vingi lakini idadi ya watalii wanaokuja hapa nchini ni wachache sana. Naomba hili tukawekeze kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine, kwenye sekta hiyo ya maliasili, Serikali inapata mapato madogo sana kupitia misitu. Nchi nyingine kwa sasa zinanufaika sana kupitia misitu kuliko ilivyo sisi, tunategemea sana kuvuna misitu na kwenda kuuza magogo. Nikuombe Waziri mwenye dhamana mkishirikiana na Waziri wa Fedha, kipo chanzo ambacho mnaweza mkapata fedha nyingi sana wekeni mikataba na mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kuvuna hewa ya ukaa. Eneo hili linatoa fedha nyingi mno. Mkisimamia uvunaji wa hewa ukaa sisi tuna misitu mingi ambayo inaweza ikatoa fedha itawanufaisha wanavijiji wanaolinda hiyo misitu, itanufaisha halmashauri na itanufaisha Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano, kwenye halmashauri yangu tumejipanga. Halmashauri ya Tanganyika miaka ijayo tunaweza tusitegemee kabisa Serikali Kuu kwa sababu tunaweza tukapata mapato kwa mwaka kati ya bilioni 30 kwa ajili ya utunzaji wa misitu. Sasa eneo hili halijafanyiwa kazi kwa kina. Serikali imejielekeza zaidi kuvuna ile misitu, na mahala ambapo panavunwa misitu huwezi ukalipwa fedha kwa ajili ya hewa ya ukaa na mashirika ya kimataifa. Naomba hili mkae mliangalie kwa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunaishauri Serikali ni kuwekeza kwenye teknolojia, hasa za mawasiliano. Ninaamini Serikali ikiwekeza hapo tunaweza tukapata ajira kwa vijana na tukapata mafundi vijana ambao watakuja kufanya shughuli nyingi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante.