Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii ya kimkakati iliyowasilishwa mbele yetu. Kwanza kabisa nianze kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango kwa kazi nzuri na bajeti nzuri, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, nimpongeze Naibu wake Mheshimiwa Eng. Masauni, Katibu Mkuu wa Wizara Ndugu Emmanuel Tutuba na watumishi wote wa Wizara kwa kutuwasilishia bajeti nzuri ambayo kwa kweli ni bajeti ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza Mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ametuletea bajeti ambayo inaonesha matumaini makubwa maana aimejielekeza katika huduma za jamii ambazo zinagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Ni bajeti nzuri ambayo kwa kweli, imeleta matumaini, wana-Muhambwe wameleta shukrani nyingi sana na mimi naziwakilisha kwa heshima na unyenyekevu mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kuna maeneo ambayo naona yanaweza yakafanyiwa kazi zaidi ili tuweze kuongeza kipato maana ni ukweli usiopingika tunahitaji kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Nitachangia upande wa maliasili na utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo lango la Muhambwe linayo hofadhi ya Moyowosi, hifadhi hii ni hifadhi kubwa sana ambayo ina wanyama wote wakubwa watano, lakini pia ina wanyama ambao wanapotea kama vile statunga, lakini pia kuna ndege ambao ni adimu kama vile shubiri. Hifadhi hii inafanya utalii wa uwindaji tu, tunavyo vitalu sita, tumekodisha vitalu vinne, lakini viwili bado havijakodishwa. Hifadhi hii ina ardhi oevu, lakini pia ni ardhi yenye majimaji inachangia pato la Taifa sana kama tunavyojua maliasili inachangia takribani asilimia 17 ya pato la Taifa, lakini inachangia asilimia 25 ya pesa za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hifadhi hii haijatumika inavyotakiwa kwa sababu ya miundombinu. Kama nilivyosema hifadhi hii ina maji, barabara hazipitiki kabisa, hakuna vyombo vya usafiri katika hifadhi hii, hii inachangia kwamba, vile vitalu vingine visiweze kupata, lakini watu wasipende kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali zile hifadhi zinazofanya vizuri ina maana kuna nguvu iliwekwa ndio zikafanya vizuri, ili ukamue maziwa vizuri kwa ng’ombe lazima huyu ng’ombe umtunze. Naomba Serikali iangalie vizuri Hifadhi ya Moyowosi, bado ina vivutio vikubwa ituwezeshe kutuletea magari, ilituahidi kutuletea trekta na boti, ituletee ili na sisi pato likipanda katika halmashauri automatically wananchi mmoja-mmoja watafaidika maana watapata ajira mahali pale, pato litaongezeka, lakini na nchi itafaidika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo tu hifadhi il eina mito mingi ambayo ina samaki bado inaweza ikatumika kwa kufanya uvuvi wa hapohapo, spot fishing, lakini pia tunaweza tukaweka utalii wa picha. Hii yote ni kujitahidi kuitumia hii hifadhi kwa kiasi kikubwa, ili tuweze kujiongezea pato. Tuilee hii hifadhi, mtusaidie tupate vyombo hivi vya usafiri, tuitangaze maana vitalu viwili kukaa bila wawekezaji hii ni hasara kwa halmashauri yetu ya Kibondo, lakini pia kwa nchi nzima; tunaomba tuitangaze Wizara itenge bajeti kabisa rasmi kwa ajili ya kutangaza hivi vivutio ili tuweze kuongeza kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naishukuru Serikali kwa sababu, inaendelea kuonesha jinsi gani inawekeza katika kupanua biashara za ujirani mwema. Jimbo langu la Muhambwe limebahatika tuna ujirani mwema na Burundi. Tunaishukuru Serikali ilitujengea soko katika Kata ya Mkarazi hii ni kati ya Mabamba na Gisulu, Burundi, lakini bado hili soko halijatumika ipasavyo ndio yani kama kila siku kama linaanza, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna vitu muhimu. Hatuna TRA pale, hakuna polisi, hakuna mambo ya ndani, ina maana Warundi pia wanaona hofu kuja kufanya pale biashara. Soko hili likiwezeshwa tukaweka One Stop Centre pale ina maana biashara pale zitafanyika tutajiongezea pato la Taifa, wananchi watafanya biashara zao pale, mazao yetu yataenda pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kabisa Jimbo langu la Muhambwe tunalima sana mihogo na wanunuzi wakubwa ni Warundi. Kwa hiyo, tukiweka soko zuri pale tukaliboresha hili soko la Mkarazi ambalo Serikali imeshaweka pesa, lakini haikuwekwa kwa utimilifu kwa sababu, haikukamilisha kuweka mambo muhimu ili biashara iweze kufanyika. Basi tunaamini ikifanya vizuri katika lile soko basi tutakuwa na biashara nzuri ya ujirani mwema na hivyo, kipato kitaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuboresha barabara maana mazao ili yaweze kufika pale Mkarazi lazima barabara ziwe nzuri. Barabara zile hazipitiki kabisa wakati wa mvua kwa hiyo, mazao yanaharibika shambani. Tuinaiomba Serikali itusaidie kwa sababu, halmashauri ikiongeza mapato basi pato la Taifa moja kwa moja litaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pia kuishukuru Serikali kwa jinsi inavyoona kuboresha miundombinu ya shule kwa ajili ya vijana hasa kwa kuongeza bajati kwenye vyuo vya ufundi stadi. Zipo VETA nchini, lakini kuna sehemu nyingine hatuna VETA ila tumebahatika kuwa na vyuo vya wananchi ambavyo vilianza miaka mingi sana, kama Jimbo langu la Muhambwe chuo kimeanza mwaka 1975 kwa hiyo, kwa picha ya kawaida unaweza ukaona hiki chuo kiko katika hali gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali ilituletea pesa milioni 500, tulifanya ukarabati kwa kiasi. Ili tuwasaidie vijana wa Jimbo la Muhambwe tunaomba chuo hiki kiangaliwe vizuri kwanza wakati tukijipanga kwenda kwenye VETA. Tuongezewe pesa ili tukiboreshe zaidi, tuongeze mabweni, tuongeze madarasa, tuongeze vifaa, ili vijana nao wa Muhambwe waweze kupata ujuzi mdogomdogo ili waweze kujiajiri kwa ajili ya kufanya biashara, ili tuweze kuongeza kipato kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali kwa tozo hizi ilizoleta tozo ya line za simu, tozo za miamala, tozo mbalimbali ambazo hizi zitatusaidia kupata kipato, tutaendelea kupata kipato kwa watu wengi kidogo kidogo kipato ambacho ni kodi ambayo si ya moja kwa moja kwa hiyo hii haimuumizi sana mwananchi, ombi langu kwa Serikali fedha hizi zikipatikana basi siende kule tulipozielekeza, hasa kwenye TARURA maana sisi wa vijijini hasa tunalilia kwanza barabara zipitike, barabara hazipitiki kabisa, vijiji haviunganishwi kama vijiji haviunganishwi Pato la Taifa litaongezeka vipi wakati watu hawawezi kuingiliana barabara ya kwenda kijiji kingine hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini cha kusikitisha bajeti ya sisi tunaotoka tunaitwa pembezoni kama Jimbo langu la Muhambwe bajeti ya TARURA inapingua kila mwaka tulianza na one billion 2017/2018, lakini 2021/2022 Milioni 800, nilidhani kwa kuwa ni pembezoni basi tutaongezewa ili na sisi tuwasiliane japo vijiji, lakini inaendelea kupungua kwa hiyo naishauri Serikali sisi wa pembezoni pia tuna uwezo wa kuchangia pato la Taifa kama mta- invest kwenye Wilaya zetu ili tuweze kufanya vizuri, tusitolee macho tu kule kulikofanya vizuri tuanzishe na huku ambako kunaweza kukafanya vizuri zaidi, japo ni pembezoni lakini bado kuna fursa nyingi ambazo hatujazitumia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali kwa miradi ya maji ambayo tumeona kabisa fedha hizi tutakwenda kuzipata na zitaisaidia miradi ya maji. Ushauri wangu kwa Serikali miradi ya maji jamani ni mingi hata jimboni kwangu ipo lakini Jimbo la Muhambwe ni Jimbo ambalo Kibondo Mjini nikikuonyesha maji yake ni aibu ni tope, japo ukiuliza unaambiwa kuna mradi wa kwanza wa pili na wa tatu, miradi ya maji ambayo haizai matunda sielewi utafiti haufanyiki tunapoanzisha mradi, sielewi usimamizi haufai sijui vizuri naona wataalam wa maji watusaidie kwa nini tuna miradi lakini hii miradi tunaisoma kwenye makaratasi haitoi maji? kama Kata yangu ya Kibondo Mjini ni tatizo maji hakuna na yanayotoka ni tope. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi tunaishauri Serikali fedha hizi ambazo tutawakata walipa kodi kwenye lane zao za simu kwenye miamala zitumike inavyostahili miradi waione hii itawafanya wananchi waendelee kuwa na moyo na ari ya kutoa na hizi kodi hazitawaumiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kuipongeza Serikali pia kwa posho ya Madiwani, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)